Mwishoni mwa wiki Mchezaji nguli wa Manchester United na timu ya Taifa ya Uingereza Bryan Robson (pichani) amezindua rasmi kliniki ya siku nne ya kimataifa ya Airtel Rising Stars inayofanyika kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kuanzia Jumapili Oktoba 30 na kumalizika Alhamisi Novemba 3, 2011.

Kliniki hiyo ambayo inajumuisha washiriki kutoka nchi za Kenya, Malawi, Sierra Leone na wenyeji Tanzania ina lengo la kukuza vipaji vya soka vya vijana hao waliopatikana wakati wa mashindano ya Airtel Rising Stars katika nchi zao na kujumuisha wanafunzi wa shule za sekondari wenye umri chini ya miaka 17.

Ikiwa mwenyeji, Tanzania imepata fursa pekee ya kushirikisha wachezaji sita wakati Kenya imeleta washiriki wanne, Malawi na Sierra Leone zinawakilishwa na wachezaji wawili kila moja. 

Wachezaji kutoka Tanzania ni Dennis Richard, Seleman Mbovu, Samir Omar, Charles John, Graham Naftali na Kassim Jungu. 

Kutoka Kenya ni Naim Ashraf, Mzee Ali Rama, Naomi Njeri na Emily Auma. Washiriki kutoka Sierra Leone ni Patrick Gbinda na Hamza Kamarana kutoka Malawi ni Amidu Mapila na Chimwemwe Billy.

Mpango wa soka kwa vijana wa Airtel Rising Stars ulizinduliwa mwezi Julai kwa kushirikiana na moja ya timu kubwa duniani, Manchester United.Mpango huu unafanyika kuanzia katija ngazi ya mkoa na taifa na kuhitimishwa kwa kliniki za aina yake nchini Gabon na Tanzania chini makocha kutoka Manchester United.

Ufunguzi wa kliniki inayofanyika Dar es Salaam ulifanywa na mchezaji mahiri wa kiungo wa Manchester United Bryan Robson. Kapteni mstaafu wa timu ya Taifa ya Uingerza, Robson aliichezea Manchester United kwa mafanikio kwa misimu 10 alikuwa ni miongoni mwa wachezaji wa klabu hiyo aliyotwaa mataji mawili ya ligi kuu na matatu ya FA kuanzia msimu wa mwaka 1981-1982 hadi 1993-1994.

“Nina furaha kwamba mpango wa Airtel Rising Stars una lengo la kuwafaidisha wachezaji chipukizi wenye umri chini ya miaka 17, ambao kwa maoni yangu, ndiyo nguzo kubwa ya mafanikio ya mpira wa miguu”, alisema mchezaji huyo mstaafu wa Uingereza na kupongeza kampuni ya Airtel kwa kubuni na kuanzisha mpango huu aliouelezea kuwa muhimu kwa maendeleo ya mchezo wa mpira wa miguu barani Afrika.

Alisisitiza kuwa njia ya kuelekea kwa mafanikio ya kweli ya mpira wa miguu lazima ianze kwa kutilia mkazo programu za vijana kama mpango huu wa Airtel unavyofanya. “Mimi mwenyewe niliweza kufanikiwa katika soka kwa sababu nilianza kucheza soka nikiwa mdogo”, alisema.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Masoko wa Airtel Tanzania Cheikh Sarr alisema kwamba Airtel inajivunia kuwa sehemu ya programu hii yenye lengo la kurahisisha upatikanaji wa vipaji vya soka. “Sehemu hii ya Airtel Rising Stars pengine ni muhimu sana katika mashindano. Kambi hii itawapa vijana fursa ya kukuza ujuzi wao na kuwafanya kuwa wachezaji wazuri.” Alisema Sarr.
Aliipongeza Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF) na wadau wengine kwa kuikumbatia programu hii ya soka ya Airtel na kuahidi kwamba Airtel itahakikisha mikoa zaidi inashirikishwa mwaka ujao.

Akizungumzia kliniki hii, Mtendaji Mkuu wa Manchester United Bw. David Gill alisema; “Kliniki ya soka ya Airtel Rising stars inawapa vijana walioteuliwa kushiriki mazingira bora ya kujifunza chini mpango wa mashule wa Manchester United wenye lengo la kuzalisha wachezaji wazuri wanoweza kucheza mpira wa kuvutia”. 

Aliongeza ya kuwa kliniki hizi zinafanywa kulingana na program za Manchester United lakini zinafanywa kwa namna ambayo inawawezesha wachezaji chipukizi ‘kujifunza kucheza kama vile ambavyo Manchester United wanacheza’  
Mbali ya Airtel na Manchester United, AON, kampuni kubwa ya bima duniani vilevile imejitokeza kudhamini kliniki hii pamoja na michuano ya Airtel Rising Stars na itakuwa inatoa bima kwa washiriki.

Kliniki hii inahitimisha mashindano ya Airtel Rising Stars mwaka 2011. Programu hiyo ilizinduliwa Juni mwaka huu na mshambuliaji wa zamani wa Manchester United, Andrew Cole aliyeicheaea klabu ya Manchester United kwa misimu saba na kuisaidia kutwaa mataji matano kati ya 19 ya Ligu Kuu ya soka ya Uingereza iliyojinyakulia hadi sasa.

Programu ya Airtel Rising Stars ni mpango wa Afrika nzima wenye lengo la kuwajengea mawakala, makocha, mamlaka za soka na wadau wengine fursa ya kuona vipaji vya wanasoka chipukizi na kutumia fursa hiyo kuviendeleza ili kupata wachezaji wazuri kwa faida ya taifa hapo baadaye.




Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...