TWIGA STARS YAPANGIWA NAMIBIA
Timu ya Taifa ya Wanawake (Twiga Stars) imepangwa kucheza                                                                                                                     na Namibia katika mechi ya mchujo kuwania tiketi ya kucheza fainali za nane za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wanawake.

Mechi ya kwanza itachezwa jijini Windhoek, Namibia kati ya Januari 13, 14 na 15 mwakani wakati mechi ya marudiano ya raundi hiyo ya awali itachezwa Dar es Salaam kati ya Januari 27, 28 na 29 mwakani.

Iwapo Twiga Stars itafanikiwa kuitoa Namibia, katika raundi ya kwanza itacheza na mshindi wa mechi kati ya Ethiopia na Misri ambazo pia zinaanzia raundi ya awali.

Mechi ya awali ya raundi ya kwanza itachezwa ugenini kati ya Mei 25, 26 na 27 mwakani. Mechi ya marudiano itachezwa kati ya Juni 15, 16 na 17 mwakani.

Timu ambazo zinaanzia moja kwa moja raundi ya kwanza kutokana na kuwa juu katika viwango vya ubora ni Afrika Kusini, Cameroon, Equatorial Guinea na Nigeria.

Nchi nyingine zinazoshiriki mashindano hayo ni Guinea, Cote d’Ivoire, Kenya, Msumbiji, Zambia, Malawi, Morocco, Tunisia, Senegal, Burundi, Botswana, Zimbabwe, Uganda, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), Mali na Ghana.

SAFARI YA TAIFA STARS
Taifa Stars inaondoka leo saa 12.15 jioni kwa ndege ya Qatar Airways kwenda Morocco kwa ajili ya mechi dhidi ya wenyeji ambayo itachezwa Oktoba 9 mwaka huu.

Msafara wa Stars unaongozwa na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Wallace Karia na utakuwa na wachezaji 20, benchi la ufundi lina watu sita chini ya Kocha Mkuu Jan Poulsen. Naibu Mkuu wa Msafara ni Makamu wa Rais wa Chama cha Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFA), Alhaj Haji Ameir.

Wachezaji ni Juma Kaseja, Shabani Dihile, Erasto Nyoni, Idrisa Rajab, Aggrey Morris, Juma Nyoso, Nadir Haroub, Henry Joseph, Nurdin Bakari, Shabani Nditi, Jabir Aziz, Mrisho Ngasa, Ramadhan Chombo, Abdi Kassim, Mbwana Samata, Dan Mrwanda, Mohamed Rajab, John Bocco, Hussein Javu na Nassoro Cholo.

Mbali ya Poulsen, wengine kwenye Benchi la Ufundi ni Sylvester Marsh (Kocha Msaidizi), Juma Pondamali (Kocha wa Makipa), Dk. Juma Mwankemwa (Daktari wa Timu), Alfred Chimela (Meneja Vifaa) na Leopold Mukebezi (Meneja wa Timu).

Timu itarajea nchini Oktoba 11 mwaka huu saa 2 asubuhi.

Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...