Muhidin,
Andy Swebe
Nimestushwa na kuhuzunishwa kwa viwango tofauti vya misiba na taarifa za misiba ya ndugu, jamaa na marafiki zangu wengi sana. Jana jioni Jumatano tarehe 28.12.2011 nilipokea ujumbe wa simu toka kwa rafiki yangu Allain Dekula Kahanga Vumbi ambao alikuwa ametumiwa na jamaa yetu mwingine Matei Joseph uliokuwa unasema:
 "Taarifa ya Msiba: Mwenzetu Andy Swebe amefariki leo saa 10 alfajir katika Hospitali ya Marie Stoppes baada ya kushikwa na pumu usiku wa jana. Taarifa zaidi baadaye...".

Ama hakika mstuko na huzuni nilioupata baada ya kusoma ujumbe huu siwezi na sina namna ya kuulezea. Sikujua cha kufanya wala kusema halafu sikuamini kabisa hata kidogo kama kweli Andy amefariki. 

Sikuamini hata kidogo hizi taarifa. Nikapiga simu kadhaa kwa jamaa zangu Tanzania ili kuthibitisha lakini bahati mbaya sikupata majibu. Nikaingia bloguni kwako kuangalia kama kuna taarifa nikakuta hamna. Nikaenda  kuangalia kwenye blog ya Kaka John Kitime nako nikakuta hamna taarifa zozote. Nikaingia mitandao ya JamiiForums, Bongocelebrity, Vijimambo na kwa Maggid nako sikukuta chochote kuhusiana na msiba huu. Kwa mtu wa nasaba ya Marehemu Andy siyo rahisi hata kidogo kwa mtandao kama wako au kwa Kaka John au JamiiForums au Bongocelebrity au kwa Maggid au Vijimambo kukosa kuiweka taarifa kama ya msiba wa Marehemu Andy kama Breaking News kwa hiyo ikaniwia vigumu kuamini. Nikawasiliana tena na Vumbi nikamuuliza kapata wapi hizi taarifa. Vumbi akaniambia ujumbe huo ametumiwa na Matei Joseph. Akaniambia anawasiliana kupitia Skype na jamaa wa Pride FM ya Mtwara na wao wamemthibitishia kwamba Andy amefariki. Baada ya muda Vumbi akaniambia Kaka Kitime amethibitisha kwenye ukurasa wake wa Facebook hapo nikaamini. Nikaangalia tena jioni kwenye blog yako na JamiiForums nikathibitisha kwa mstuko na huzuni kwamba ni kweli Andy amefariki. Machozi ya uchungu yakanitoka.

Niliitazama picha ya Marehemu kwenye blog yako mara kadhaa huku nikikumbuka mengi. Nikakumbuka miaka yetu ya utoto tukiwa Upanga hususani viwanja vya shule ya Muhimbili. Nikakumbuka alasiri na jioni za mwishoni mwa miaka ya 70 tulipokuwa tunakutana kituo cha basi cha Posta ya Zamani Andy akiwa na Martin Pundugu tukigombania kuingia kwenye Maikarus, Leyland na Scania za mabasi ya UDA ambapo Andy na Martin walikuwa wanaenda mafunzo na mazoezi ya muziki Chang'ombe kwa Mwalimu David Mussa na mimi nikienda Uwanja wa Taifa kwa Mwalimu Charles Gwamakuba kwenye mazoezi ya riadha ya Operesheni Bayi. Nikamkumbuka Marehemu Andy na guitar lake la kwanza la Bass lililotengenezwa Urusi kwenye gereji ya nyumbani kwao Mtaa wa Kalenga, Upanga akipiga nyimbo ya Stay the Night. Nikamkumbuka Marehemu Andy na rafiki yake kipenzi Mafumu Bilali wakivinjari mitaa ya Upanga huku wamevalia nadhifu sana na wamenyoa nywele zao kwa mitindo ya kupendeza. Nikakumbuka nilipokuwa nikimshabikia alipokuwa jukwaani na bendi mbali mbali alizowahi kupigia katika kumbi mbali mbali nilizopata kwenda kuona maonyesho yake. Nikawakumbuka na ndugu zake na marafiki zetu wengi sana.

Miaka ya 70 upenzi wa muziki miongoni mwetu ulikuwa umegawanyika sana. Upanga ilikuwa imetawaliwa sana na upenzi wa miziki ya Tanzania, Kongo, KiMarekani na KiJamaica. Kulikuwa na bendi kadhaa za Upanga zilizokuwa zinapiga muziki wa Kimarekani au Kiingereza au Reggae. Marehemu Andy alikuwa na uwezo wa kupiga muziki wa dansi wa Tanzania na Kongo au pop za Kimarekani au Kiingereza au Reggae. Kwa ridhaa na mapenzi yake mwenyewe, Marehemu Andy alichukua mrengo wa mseto wa muziki wa Tanzania na Kongo. 

Nikimkumbuka Marehemu Andy nakumbuka jinsi tulivyokuwa tunamstaajabia kwa kuushadadia muziki wa dansi wa Tanzania na Kongo. Aliupenda na kuuenzi muziki wa dansi. Hakuwahi kuficha mapenzi yake kwa muziki wa dansi. Ustadi wake katika kupiga muziki wa dansi na Tanzania na Kongo unathibitika kwa kuwa mwanamuziki aliyepiga muziki na wanamuziki mashuhuri na bendi maarufu za muziki wa dansi wa Tanzania na Kongo: Aliwahi kupiga muziki na Trippers Imagination na Mwalimu David Mussa, Mzee Kintezogu Makassy na kundi la Orchestra Makassy, Bicco Stars kina Kinguti System, Kilimanjaro Revolution na kina Kanku Kelly na hatimaye wakati umauti unamkuta alikuwa katoka ziarani Marekani alipokuwa anapiga muziki kusherehekea miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania akiwa  na Nguli wa muziki wa dansi wa Tanzania na Kongo Mzee Kikumbi Muanza Mpango Mwema (Mzee Kikì), Lokassa ya Mbongo, Maneno Uvuruge na wengineo. Ustadi wake wa kupiga muziki ulimpeleka kupiga muziki sehemu mbali mbali ndani na nje ya Tanzania, Bara Hindi hadi Marekani wapo waliwahi kushuhudia Marehemu Andy akilivurumisha guitar la Bass kwa ustadi wake usiofananika na mpiga mwingine yeyote wa guitar hilo. 

Mara ya mwisho kumuona Marehemu Andy ilikuwa ni Julai mwaka huu walipokuwa wanafanya onyesho la miaka 50 ya Uhuru pale Selander Bridge Club. Matei Joseph pamoja na mpiga Bass mwingine mahiri Teddy Mbarak tulikuwa meza moja na tuliongea sana. Marehemu Andy alikuwa jukwaani wakati wote sikupata nafasi ya kusalimiana wala kuongea naye.

Nikimkumbuka Marehemu Andy namkumbuka kwa mengi zaidi ya hayo niliyoyasema. Naikumbuka hata sauti yake mathalani ya mlio wa mdudu dondora. Nakumbuka nidhamu, heshima, busara na hekima zake. Unadhifu wa akili na mwili na utanashati wa mavazi yake. Sijui kama yalikuwa ni maajaliwa au kilema chake kwamba katika maisha yangu yote ya kumfahamu Marehemu Andy sikupata kumuona kakasirika, kagombana, katukana, kadhulumu au kafanya jambo lolote lisilo la  kimaadili. Marehemu Andy alitunukiwa kipaji cha muziki, busara, ucheshi, upole na wema.

Sipati picha ni huzuni ya kiasi gani uliowaaachia Mama Bint Mkwawa, ndugu zako Makwaza, Mpeli, Tuti, Buli, Frank na wengineo. Rafiki yako Mafumu Bilali. Mzee wetu Kikumbi Muanza Mpango Mwema (King Kikì). Wanamuziki wote Tanzania na wengineo uliojumuika nao popote pale duniani. Mashabiki wako. Ndugu, jamaa, marafiki na washirika wako. Nina hakika kila atayekukumbuka atakukumbuka kwa mazuri na kukumbuku zako zitaamsha furaha, huzuni na simanzi. 

Tunakuombea Mwenyezi Mungu Akupumzishe kwa Amani Andy Brown Swebe 'Ambassador'. 
Amen.

Ni mimi nduguyo,
Fidelis M Tungaraza.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 10 mpaka sasa

  1. Sasa huu ujumbe angeupeleka kwa wafiwa ningemuona mtoamada ana maana, lakini kutuletea hapa sijui anataka tumsaidie nini. Mtu mzima ovyoo, PHEW!!!

    ReplyDelete
  2. Fide, nice one bro...umetoa kumbukumbu nzuri sana nawasifu wa marehemu. Ubarikiwe.

    ReplyDelete
  3. Mtoa ujumbe hajaomba msaada na wala si kila anayeandika ujumbe wake kwenye blog ya jamii anaomba asaidiwe. Huyu mwandishi anatumia haki yake kikatiba kuelezaeleza jinsi anavyojisikia baada ya kumpoteza rafiki yake na Ankal akaona hilo siyo tatizo ndiyo maana akairusha hewani.Vilevile unaweza kusoma mambo mbalimbali kwenye blogs na siyo lazima utoe maoni, kama hayakuhusu unayaacha na kuendelea na yale yanakuhusu. Ukufanya hivyo utajikuta unapata muda mwingi wa kufanya mabo ya maana ili kuleta maendeleo yako binafsi na nchi nzima. Salamu hizi ninazituma kwa mtoa maoni wa kwanza kabisa hapo juu.

    ReplyDelete
  4. mtoa ujumbe wa kwanza kabisa, huna nidhamu, utu na uzalendo. Hujalazimishwa kusoma, hii habari ya Msiba. Mimi mwenyewe si mfahamu huyu jamaa, lakini kupitia kwa Tungaraza, nimeona wasifu mzima wa huyu marehemu. Jitambue kwanza, ndipo uandike. Usikurupuke na kusonya watu mwanangu.

    ReplyDelete
  5. Mwenyezi Mungu amlaze mahala pema peponi, Amen

    Poleni sana Sekela, Tutty, Frank, Mpeli, Buli, Dada Salome na kaka mkubwa.

    Ahsante sana mleta habari, I was just trying to remember ni band gani kapiga maana nilikuwa mdogo sana pale Upanga...all I could remember ni Tancut Almasi nadhani.

    ReplyDelete
  6. Mtoa mada wa kwanza HUNA ADABAU! PWEW !! mwenyewe !

    Ahsante kwa uloleta wasifu wa marehemu , Nimekaa nasoma kwa taratibu na kumemorize jinsi gani posta ya zamani ilikuwa ikionekana! UDA na memories nyingi !

    NA mtoa mada wa tatu umesema vema kuwa ni bora kama jambo likiwa halikuhusu basi bora upite uwaache wenyewe yanayowahusu

    Poleni wafiwa !

    ReplyDelete
  7. Sioni kosan lolote la Bw,Fidelis,
    kwani hapa anachangia kutoa wasifa wa marehemu,hili wale wasio elewa historia ya marehemu japo nao waijue,lakini kumetokea watu wanaojiita wakosoaji na pia wana mtazamo vinyu wa kuandika maoni yasio na adabu,kwa sababu za chuki binasfi! tunajaribu kujirekebisha tabia,sio kila siku kupakana matope tu

    ReplyDelete
  8. #1 unaonekana bado uko analog na manual sana kiakili, humu ndio wafiwa weengi tumo pengine kuliko hata waliofanikiwa kufika physically nyumbani/msibani, sasa ukisema apeleke kwa wafiwa hufikirii kuwa hata wale waliofanikiwa kufika msibani nao pia hupita humu kuona mtu wao ameenziwa vp!!???

    Anyways, pole kaka Mtikubwa if at all u felt humiliated, allow me to quote one of your sayings "he/she is just a fly in a jar of milk"

    Best analysis!
    Chuwa

    ReplyDelete
  9. Poleni wafiwa wote,classmate wangu Sekela pole sana, Mungu awatie nguvu katika kipindi hiki kigumu, Bwana alitoa na bwana ametwaa,R.I.P kaka Andy.

    ReplyDelete
  10. HUU NI WASIFU WA MAREHEMU NDUGU YANGU KAMA ULIKUWA HUJAJUA. NEXT TIME FIKIRIA KABLA YA KUANDIKA ULICHO ANDIA (ANONYMOUS WA KWANZA)
    THANKS FIDELIS. WAFIWA NDIO SISI

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...