Hayati Andy Swebe (wa tatu kushoto) akitumbuiza na King Kikii na wanamuziki wengine katika sherehe za miaka 50 zilizofanyika Dulles, Virginia, nchini Marekani wakati wa kilele cha mkutano wa DIASPORA 2011

Mwanamuziki wa siku nyingi nchini ambaye aliondokea kuwa mahiri katika gitaa la bezi Andy Brown Swebe aka ambasador (pichani) amefariki dunia leo baada ya kuugua kwa muda mfupi.


Kwa mujibu wa mwanamuziki Kitime aliyefika katika ofisi za HabariLeo majira ya mchana, Swebe alifariki majira ya saa 10 alfajiri katika hospitali ya Marie Stoppes ya Mwenge alipokuwa amekimbizwa kwa ajili ya tatizo la pumu.


Mipango ya maziko ya Andy Brown Swebe ambaye alianza kupenda gitaa kutokana na kumsikia baba yake mzee Mwalimu Brown Samson Swebe akifanya vitu vyake, inafanyika nyumbani kwao Sinza Mori.


Kama Miezi miwili iliyopita mwanamuziki huyo alikuwa katika safari ya kikazi nchini Marekani ambako aliambatana na King Kiki na Maneno Uvuruge.Kitime alisema zaidi kwamba mipango ya maziko inasubiri baba zake wakubwa kutoka Tukuyu, Mbeya.

Swebe ambaye alianza kujifunza kupiga gitaa huko Chang’ombe kwa David Musa wa Safari Trippers,bendi yake ya kwanza ilikuwa ni ya Oshekas ya Brian Shaka ambapo ilikuwa inapiga mara moja kwa mwezi Yatch Club.

kwa mujibu wa mkongwe John  Kitime, alipiga bendi hii mpaka alipomaliza kidato cha nne, ndipo alipopata kazi na kuhamia Morogoro, huko akawa anafanya kazi kiwanda cha ngozi.

Siku moja Orchestra Makassy ilifanya ziara Morogoro, na hapo rafiki yake aliyekuwa anapiga Keyboards katika bendi hiyo John Bosco akamuona na akakaribishwa jukwaani na akapiga nyimbo chache jambo ambalo lilifanya Mzee Makassy amwite katika bendi yake.

Alijiunga na Makassy Mei 25,1983 na onyesho la kwanza lilikuwa Mkirikiti Bar Msasani. Akiwa Orchestra Makassy alishiriki kurekodi nyimbo kama Olenge, Bembeya, Nono, Minachoka ya Masiya Radi. Wakati huo bendi ilikuwa na wakongwe kama Mzee Aimala Mbutu(Simaro), Fan Fan Mosesengo, Kassim Mganga na Dk Remmy.

Mwezi uliopita hayati Andy Swebe alikuwa Marekani na King Kikii na Maneno Uvuruge kuburudisha wakati wa sherehe za Miaka 50 ya Uhuru huko jijini Washington DC na vitongoji vingine vya Marekani. 

Globu ya Jamii inatoa mkono wa pole kwa familia ya Hayati Andy Swebe ambaye alikuwa rafiki wa karibu sana tokea enzi hizo akiishi Upanga kwa Mzee Brown Swebe, mmoja wa waasisi wa kiwanda cha kuungia magari aina ya SCANIA kule Kibaha. 

Mola aiweke mahali pema roho ya Marehemu
AMINA

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 8 mpaka sasa

  1. kweli kifo cha huyu kaka ni fundisho kwetu wote tuliobaki kuawa tayari muda wote,maana ni juzi tu alikuwa huku marekani mzima wa afya,leo kafa.inauma sana poleni sana wafiwa.

    ReplyDelete
  2. R.I.P Swebe!

    ReplyDelete
  3. RIP "Ambassador"

    ReplyDelete
  4. Poleni sana

    ReplyDelete
  5. Poleni sana kwa msiba.
    Andy Swebe R.I.P
    /Vumbi Dekula

    ReplyDelete
  6. Rest in peace Andi. Gone too soon! What went wrong at Stoppes? I can't believe this!

    ReplyDelete
  7. Nashangaa habari hii haipo kwenye blog ya Kitime muda huu ninapoandika maoni haya. Kama kuendesha blog kumemshinda atuambie.

    ReplyDelete
  8. Tunakupenda sana Andy, lakini Mungu anakupenda zaidi. Pumzika kwa Amani.Utakumbukwa daima

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...