Uongozi wa Kampuni ya Reli Tanzania (TRL) una furaha kuwataarifu kuwa kuanzia leo Januari 04, 2012 imerejesha huduma zake katika reli ya kati . 

Ambapo treni 4 za mizigo zimepangwa kuanzia safari kutokea Mororgoro kwenda Tabora ! Mbili kati ya hizo zimeshaondoka Morogoro kati ya saa 7 na 9 usiku kuamkia leo wakati nyingine 2 zilitarajiwa kuondoka saa 2 na 5 asubuhi leo.

Wakati huo huo huduma ya usafiri wa treni ya abiria kutoka Dar kwenda Kigoma imepangwa kuanza tena hapo siku ya Jumamosi Januari 07, 2012 saa 11 jioni, na kwamba wananchi wote ambao wanapendelea kusafiri na treni hiyo wafike katika stesheni zilizokaribu yao kukata tiketi za safari kuanzia leo Jumatano Januari 04, 2012.

Uamuzi wa kuanza kutoa huduma unataokana na kukamilika matengenezo ya reli katika maeneo mbali ya reli ya kati kuanzia mkoani Dar es Salaam, Pwani na Dodoma na hasa maeneo ya Gulwe na Godegode mkoani Dodoma ambayo yaliathirika sana na mafuriko yaliyotokana na mvua kubwa zinazoendelea mikoani Pwani, Morogoro, Iringa na Dodoma.

Wahandisi na mafundi wa TRL walikuwa wanafanya kazi za ukarabati maeneo husika saa 24 bila ya kujali mapumziko na hivyo kuwezesha kukamilika kazi za ukarabati kwa wakati.Aidha ziara za viongozi wa ngazi za juu wa Wizara ya Uchukuzi(MoT) akiwemo Waziri(MoT) , Mhandisi Omar Nundu na Katibu Mkuu(MoT) Mhandisi Omar Chambo ziliwapa motisha wa kukamilisha kazi ya ukarabati kwa wakati.

Huduma za usafiri na usafirishaji zilisimamishwa rasmi katika reli ya kati kuanzia Desemba 20 mwaka jana ambapo Uongozi wa TRL ulilazimika kukodi mabasi yapatayo 25 siku ya Desemba 21, 2011 kuwasafirisha abiria 1834 wa treni waliokuwa wamekwama Dodoma wakitokea Kigoma
kutokana na eneo la reli ya kati ya Stesheni za Gulwe na Godegode mkoani Dodoma tuta lake kusombwa na mafuriko ya mvua zinazoendelea nchini.

Taarifa hii imetolewa na Afisi ya Uhusiano kwa niaba ya Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TRL
Mhandisi K.A.M.Kisamfu.

MIDLADJY MAEZ
MENEJA UHUSIANO - TRL

DAR ES SALAAM.
JANUARI 04, 2012

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 2 mpaka sasa

  1. Yiii mawee mimi Bidyanguze mwakei nitaingia Chigoma sasa ri tereni rimeanza!

    ReplyDelete
  2. Ndugu Mjengwa hivi Bara Mwanza haipo? Nawakilisha kilio cha wananchi wa Mwanza kuililia
    treni ambayo ilikuwa ni usafiri tegemezi haza kwa mwananchi wa kawaida. ina maana mwanza ndio hakuna tena treni au vipi?

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...