JKT RUVU, YANGA KUCHEZA SAA 12
Mechi namba 100 ya Ligi Kuu ya Vodacom kati ya JKT Ruvu na Yanga itachezwa kesho (Januari 28 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kwa mujibu wa ratiba ya ligi hiyo. Lakini mechi hiyo sasa itaanza saa 12 kamili jioni badala ya saa 10 kamili jioni.
Mabadiliko hayo ya muda yamefanyika ili kutoa nafasi kwa timu ya Taifa ya Namibia kufanya mazoezi kwenye uwanja huo saa 10 jioni kabla ya mechi yao ya Kombe la Afrika kwa Wanawake (AWC) dhidi ya Twiga Stars itakayochezwa Jumapili (Januari 29 mwaka huu) kwenye uwanja huo kuanzia saa 10 kamili jioni.
Kwa mujibu wa kanuni za mashindano ya AWC yanayoandaliwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), siku moja kabla timu ngeni ni lazima ipewe fursa ya kufanya mazoezi kwenye uwanja utakaotumika kwa mechi katika muda ule ule.
Pia kutokana na mechi ya Twiga Stars na Namibia, mechi namba 102 kati ya Moro United na Azam iliyokuwa ichezwe Januari 29 mwaka huu Uwanja wa Chamazi, Dar es Salaam, sasa itachezwa Januari 30 mwaka huu kwenye uwanja huo huo.
Mabadiliko hayo hayajaathiri mechi nyingine za mzunguko wa 15. Mechi hizo ni kati ya Villa Squad na Toto African (Januari 28 mwaka huu- Uwanja wa Chamazi), Ruvu Shooting na Kagera Sugar (Januari 28 mwaka huu- Uwanja wa Mlandizi), Mtibwa Sugar na Coastal Union (Januari 29 mwaka huu- Uwanja wa Manungu), African Lyon na Polisi Dodoma (Februari 1 mwaka huu- Uwanja wa Chamazi) na Simba na JKT Oljoro (Februari 1 mwaka huu- Uwanja wa Taifa).
Viingilio kwa mechi za Uwanja wa Taifa ni sh. 3,000 viti vya bluu na kijani, sh. 5,000 viti vya rangi ya chungwa, sh. 10,000 VIP C na B, na sh. 15,000 VIP A wakati Uwanja wa Chamazi ni sh. 3,000 kwa mzunguko na sh. 10,000 kwa jukwaa.
WAETHIOPIA KUCHEZESHA YANGA, ZAMALEK
Waamuzi kutoka Ethiopia ndiyo watakaochezesha mechi namba 7 ya Ligi ya Mabingwa Afrika kati ya Yanga na Zamalek ya Misri itakayochezwa Februari 18 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) limemteua Bamlack Tessema kuwa mwamuzi wa kati kwenye mechi hiyo wakati waamuzi wasaidizi ni Yilma Knife na Mussie Kindie. Mwamuzi wa akiba (fourth official) atakuwa Waziri Sheha wa Tanzania na Kamishna wa mchezo huo ni Charles Kafatia wa Malawi.
KOZI YA UKOCHA NGAZI PEVU FEB 12
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limeandaa kozi ya ukocha ngazi pevu (advanced level) itakayofanyika Dar es Salaam kuanzia Februari 12-25 mwaka huu.
Wakufunzi watakuwa Kocha wa Taifa Stars, Jan Poulsen ambaye pia ni mkufunzi wa Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA), Mkurugenzi wa Ufundi wa TFF, Sunday Kayuni ambaye pia ni mkufunzi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) na Kocha wa timu za Taifa za vijana Kim Poulsen ambaye pia ni mkufunzi wa Chama cha Mpira wa Miguu cha Denmark (DBU).
Mwisho wa kupokea maombi kwa makocha wanaotaka kushiriki kozi hiyo ambayo ada yake ni sh. 60,000 itakuwa Februari 5 mwaka huu.
Sifa kwa waombaji ni kuwa elimu ya kuanzia kidato cha nne, wawe wanafanya kazi hiyo ya ukocha na wamefaulu vizuri mafunzo ya ukocha ngazi ya kati (intermediate level). Pia wawe wamefundisha angalau kwa miaka miwili baada ya kupata cheti cha intermediate level.
Pia wanatakiwa maombi yao yawe yameidhinishwa na ama vyama vya makocha wa mpira wa miguu vya mikoa, vyama vya mpira wa miguu vya wilaya au vyama vya mpira wa miguu vya mikoa.
Kwa makocha watakaofaulu kozi hiyo watakuwa wamepata sifa ya kuhudhuria kocha ya ukocha ya Leseni C ya CAF.
TFF tiketi za mechi ya Twiga Stars na Namibia zinapatikana wapi??????!!!1
ReplyDelete