Kamati ya muda ya kushughulikia madai ya madaktari nchini inapenda kuwajulisha madaktari wote pamoja na kada nyingine zote za afya nchini juu ya kile ambacho kimejiri katika siku ya leo ya tarehe 09.02.2012 ikiwa ni matokeo ya kikao wanataaluma wa kada za afya na Waziri Mkuu Mhe. Mizengo Pinda na baadaye kufuatiwa na kikao kati ya madaktari na kada nyingine za afya.

Ifahamike kuwa kama Kamati tulipata mwaliko wa kushiriki katika Mkutano huo ambapo ilitarajiwa kuwa Mhe, Waziri mkuu atafika kwa nia ya kutoa mrejesho wa madai ya madaktari yaliyowasilishwa mezani kwake mnamo tarehe 23.01.2012. Madai yetu yalikuwa manane na Mh Wazizri mkuu aliweza kutoa maelezo ya dai moja baada ya lingine.

Miongoni mwa madai ambayo mpaka sasa yamepatiwa majibu ya kuridhisha ni pamoja na;
  1. Kuwawajibisha watendaji wakuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, wakiwemo Katibu Mkuu Mama Blandina Nyoni , na Mganga Mkuu wa Serikali Dr. Deo Mtasiwa. Aidha Mh waziri mkuu alisema kuwa ameshalifikisha kwa Mh Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania suala zima la kuwawajibisha watendaji wa wakuu wa kisiasa wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ambao ni  Waziri Mh Hadji Mponda na  Naibu Waziri  Mhe. Lucy Nkya.
  2. Kama sehemu ya maridhiano, Mh Waziri Mkuu pia aliahidi mbele ya mkutano kuwa hakutawepo na unyanyasaji au vitisho vya aina yoyote ile kwa wale wote walioshiriki katika kushinikiza Serikali kutatua kero hizo. Aidha kama sehemu ya maridhiano, Mh waziri Mkuu pia alifuta zuio la madaktari kutokufanya mikutano. Lakini pia, Mh waziri Mkuu alisema kuwa Serikali haina kusudio la kumfukuza  kazi mtumishi yeyote wa afya yule kazi aliyeshiriki katika mchakato huu wa kuishikiniza Serikali kutafuta ufumbuzi madai ya madaktari nchini.
  3. Aidha, Mh waziri Mkuu amesema “Interns” wote waliokuwa wamehamishwa kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili wamesharudishwa bila masharti katika hospitali hiyo ili kuendelea na program kama kawaida. Hili pia linaambatana na kulipwa na kupewa stahiki zao zote.
  4. Pia suala la madaktari na familia zao kuwa na Kadi ya Bima ya Afya ya kijani( Green Card) limekubaliwa na kwa sasa tusubiri utekelezaji.
  5. Pia ilikubaliwa kuwa madaktari watapata fursa ya kukopeshwa magari kama watumishi wengine wa umma.
Mbali na madai hayo, pia Mh. Waziri Mkuu alitoa ufafanuzi juu ya madai yanayuhusu maslahi ya watumishi wa afya ikiwa ni pamoja na Mishahara na Posho na stahiki mbalimbali. Lakini hata, Mh waziri Mkuu hakutoa majibu ya moja kwa moja ya kiwango gani kitakachoweza kulipwa na Serikali kama mishahara, posho na stahiki mbalimbali kwa minajili kwamba bado zinafanyiwa kazi na kamati ya wataalamu aliyoiunda ili waweze kumshauri.

 Aidha, Mh waziri Mkuu alisema kuwa kwa wakati huu inaweza kupandisha “on call allowances” za kada mbalimbali za afya kutoka shilingi 3,000 – 10,000/= na kufikia kati ya shilingi 5,000 hadi 25,000. Madaktari bado wanaona ongezeko hili halilingani na ukubwa wa kazi ifanywayo pindi mtumishi wa afya anapokuwa “on call” na hivyo basi kuendelea kupendekeza kuwa “on call” allowance iwe ni 10% ya mshahara  wa mtumishi husika.

Pia Mhe, Waziri Mkuu hakuweza kueleza kinagaubaga mkakati kazi wa uboreshaji wa huduma za afya wapatayo wananchi wa Tanzania.

Baada ya tamko hilo la Serikali kumalizika, Mh Waziri Mkuu na ujumbe wake waliondoka, na Mkutano huo ukaendelea kwa Kamati kufanya Mkutano na madaktari wote, lengo ikiwa kujadili tamko hilo na kutoa maazimio.

Baada ya majadiliano ya muda mrefu, madaktari walikubaliana kwamba; kwa kuwa Serikali imeanza kuonyesha nia ya kutatua tatizo hili kwa kutekeleza baadhi ya maazimio yetu, wajumbe kwa niaba ya madaktari wote nchi nzima tulikubaliana na kuazimia yafuatayo;
  1. Kurudi kazini mara moja kuanzia kesho tarehe 10.02.2012 bila masharti yeyote.
  2. Kamati ya jumuiya ya madaktari kama sehemu ya MAT kuendelea kukaa mezani ya majadiliano na Serikali ili kuanza kupitia madai hasa yale yanayohusu maslahi.
  3. Kukutana tena tarehe 03.03.2012 ili kupata mrejesho wa kiwango cha utekelezaji wa madai hayo kwa mujibu wa vikao vya majadiliano na makubaliano na hatimae kuchukua hatua zaidi.
  4. Kujadili utekelezaji juu ya Kuwawajibisha Waziri na Naibu Waziri wa Afya na Ustawi na Jamii.
  5. Mwisho kabisa Madaktari wote kwa ujumla wake walilaani na kukemea kitendo cha Jeshi la Polisi kuwakamata na kuwahoji wanaharakati wa haki za kibinaadamu na mashirika ya kijamii wakiwemo Dr. Hellen Kijo-Bisimba na Mama Ananilea Nkya na wanaharakati wengine wote waliokumbwa na kamata kamata hiyo na hivyo basi tunalitaka jeshi hilo kuwaachilia huru mara moja bila masharti yeyoye.
Pamoja Tunaweza
Imetolewa na Kamati ya muda ya kushughulikia madai ya madaktari Tanzania
Dr, Ulimboka Stephen
Mwenyekiti.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 11 mpaka sasa

  1. KWANZA KABISA SHUKRAN KWA MUNGU BWANA, WAZIRI MKUU MADAKTARI WOTE KUWEZA KUFIKIA MUAFAKA KWA NJIA YA AMANI. TWASHAUKURU KUWA WAGONJWA WATAHUDUMIWA JAPO KUWA HASARA KUBWA YA MAISHA IMEPATIKANA, TUKUBALI KUSAMEHE ILI TUENDELEE MBELE, NAOMBA SERIKALI YETU IWE MAKINI KATIKA KUSIKILIZA MADAI YA WANANCHI WALIOWAWEKA MADARAKANI, KWA KWELI MADAKITARI WANAFANYA KAZI KATIKA MAZINGIRA MAGUMU SANA NA KAZI NI KUBWE MNO, MPAKA KUFIKIA KUGOMA NI KWAMBA WALIKUWA KATIKA HALI MBAYA SANA MAAN WAMEVUMILIA SANA, KUTOWASIKILIZA WANANCHI IKO SIKU TUTAKUWA KATIKA HALI MBAYA SANA, JIRANI YAKO AKINYOLEWA NYWELE ZAKO TIA MAJI, SHUKRANI TENA KWA MADKATARI NAWATAKIA KAZI NJEMA,

    ReplyDelete
  2. Tafadhali madaktari muibane serikali watoe majibu kuhusu ni namna gani wataboresha sekta ya afya..hongereni kwa hapo mlipofikia,ila kuweni makini na hii serikali kwani maneno mengi bila vitendo...walimu mnaona wenzenu wanavyodai haki??hakuna kazi ya wito dunia hii,lazima upate haki yako inayostahili..kama huipati dai kwa nguvu zote

    ReplyDelete
  3. Hatua nzuri hiyo kunusuru maisha ya watanzania,ila huyo kijobisimba na mwenzie nkya ni wanafiki walikwenda kuvuruga mkutano tu.kwanza inasemekana huyo nkya muda wake wa kuongoza hiyo NGO ulikwisha amelazimisha zaidi ya mara moja sasa anatuonyesha mfano gani kama kiongozi?huku amebeba bango la kutaka viongozi waondolewe,nyani haoni .....

    ReplyDelete
  4. Afadhali, uzi huo huo madaktari, maana hawa jamaa wanajiona kama wao si watanzania.

    ReplyDelete
  5. Kweli huyo nkya na kijobisimba kutoka mkoa wa kilimanjaro wana fujo hao ndio maana ndoa zimewashinda hao. Watoswe hao

    ReplyDelete
  6. Serikali bwana!! Watu mpaka wagome, nahao waliokufa mahospitalini kwa huu mgomo watafidiwa nini.
    Tatueni tatizo kabla halijawa kubwa, sio kutishia watu na professional zao.
    Alaaa!

    ReplyDelete
  7. Waalimu wanagoma kimtindo,ukitaka kujua we tizama tu matokeo ya darasa la saba, form four na six utaelewa

    ReplyDelete
  8. Tunashukuru kwa hatua ambazo serikali inachukua. Serikali inatakiwa kuheshimu watendaji katika fani nyeti kama udaktari. Kuwapa mishahara midogo na posho ndogo ni kuwadharau wakati vijana wadogo TRA wanawapita mishahara kwa mbali hii nini sasa. Mpaka afe mtu ndio serikali ichukue hatua?

    ReplyDelete
  9. Ama kweli, mtoto akilia mpe ziwa anyonye, akishiba atalala usingizi. Hivi yale madai ya msingi ya madaktari ya kuboresha vitendea kazi na huduma za afya kwa maslahi ya jamii yameishia wapi? Madaktari wanarudi kufanya kazi katika mazingira gani? Kweli ashibaye hamtabui mwenye njaa!

    ReplyDelete
  10. Mlipoharibu ni hapo kwenye Bisimba na Nkya tu. Mngependekeza polisi wawe wanawachapa bakora kila siku taarifa yenu ingekuwa 'MWAA'

    ReplyDelete
  11. Nawe 'Bwana' Ulimboka acha kujifanya mjuaji kupita kiasi! Hivi kuna kosa gani kwa wanausalama wetu kutekeleza majukumu yao ya kazi kwa kuwatia nguvuni hao wachochezi? Hayo mabango waliyokwenda nayo yalikuwa ya kazi gani kama sio kuvuruga amani? Hongera Polisi na tafadhali msirudishwe nyuma na hao wapinga kila kitu.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...