Mkuu wa wilaya ya Liwale, Victor Paul Chiwile (pichani),  amefariki dunia ghafla jana  katika Hotel ya Vision mjini Lindi. Mkuu wa Mkoa wa Lindi,Bw Ludovick Mwananzira amesema hapo leo mwili huo utapelekwa katika kanisa la Anglikana Dayosisi ya Lindi kwa ajili ya kuombewa na pia itakuwa fursa kwa wakazi wa Mkoa wa Lindi kutoa heshima zao za mwisho na baada ya hapo safari ya kuelekea wilaya ya Kibaha mkoani Pwani kwa ajili ya mazishi itaanza. Chanzo cha kifo chako hakijajulikana hadi sasa. 



Wakati huo huo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete amemtumia salamu za rambirambi Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Mheshimiwa Ludovick Mwananzila kufuatia kifo cha ghafla cha Mkuu wa Wilaya ya Liwale, Marehemu Paul Chiwile kilichotokea usiku wa kuamkia tarehe 23 Machi, 2012 Mkoani Lindi alikokuwa amekwenda kikazi kutekeleza majukumu muhimu ya kitaifa.

Marehemu Paul Chiwile alikwenda Mjini Lindi kuhudhuria Kkao cha Kamati ya Sherehe za NaneNane, Kikao cha Siku ya UKIMWI Duniani ambayo mwaka huu kitaifa itafanyika mkoani Lindi, Kikao cha Maandalizi ya Maonyesho ya SIDO ambayo Kikanda yanafanyika Mkoani Lindi, na Kikao kuhusu Wiki ya Watu wenye Ulemavu wa Ngozi ambayo pia kitaifa inafanyika Mkoani humo.

“Nimeshtushwa, nimesikitishwa na kuhuzunishwa na habari za kifo cha ghafla cha Mheshimiwa Paul Chiwile ambaye enzi za uhai wake nilimfahamu kama kiongozi hodari, shupavu na msaidizi muhimu katika kusukuma gurudumu la maendeleo katika nchi yetu hususan katika Wilaya ya Liwale alikokuwa akiwatumikia wananchi”, amesema Rais Kikwete katika katika salamu zake. Amesema kifo chake kimeacha simanzi na huzuni kubwa kwa wananchi wa Wilaya ya Liwale huku Taifa na hususan Wilaya ya Liwale ikiachwa na pengo kubwa la kiuongozi.

Kutokana na kifo cha Marehemu Chiwile, Rais Kikwete amemuomba Mkuu wa Mkuu wa Lindi kunfikishia salamu zake za rambirambi na pole nyingi kwa kwa familia ya Marehemu kwa kuondokewa na mpendwa wao na mhimili madhubuti wa familia.  Ameihakikishia familia hiyo kuwa yupo pamoja nao katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo.   Amesema anamuomba Mwenyezi Mungu, mwingi wa Rehema ailaze mahala pema peponi roho ya Marehemu Paul Chiwile, na awape wanafamilia moyo wa uvumilivu na ujasiri katika kipindi chote cha maombolezo.

Rais Kikwete vilevile ametoa pole nyingi kwa wananchi wa Wilaya ya Liwale kwa kumpoteza kiongozi muhimu aliyejitoa vilivyo kuwatumikia.  Amewataka hali kadhalika wawe watulivu na wavumilivu licha ya kumpoteza kiongozi wao kwani kazi ya Mungu haina makosa.

Mwisho.

Imetolewa na:

Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
23 Machi, 2012




Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...