Mkuu wa Mkoa wa Arusha Magesa Mulongo akitoa hotuba ya ufunguzi wa Mkutano wa Wadau wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya mkoani Arusha.
Naibu Mkurugenzi wa NHIF,Hamis Mdee akitoa maelezo ya utangulizi kwa mgeni rasmi. 3. Mkurugenzi wa Fedha na Uwekezaji wa NHIF, Bw. Rutazaa akiwasilisha mada ya utekelezaji ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya kuanzia mwaka 2001.
Mkurugenzi wa Fedha na Uwekezaji wa NHIF, Bw. Rutazaa akiwasilisha mada ya utekelezaji ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya kuanzia mwaka 2001. 4.Wadau wa mkutano huo wakifuatilia mada.
Madaktari wakiendelea na uzoezi la upimaji kwa wadau waliohudhuria mkutano huo ikiwa ni moja ya shughuli zinazoambatana na siku za wadau.
Na Mwandishi Wetu, Arusha
WADAU wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF),wamesema hakuna sababu ya kuwa na uhiari katika suala la kujiunga na Mfuko wa Afya wa Jamii (CHF) na badala yake iwekwe sheria inayomlazimu mwananchi kujiunga.
Wamesema kuwa suala la afya za wananchi ni nyeti hivyo hakuna sababu ya kuendelea kuona wananchi wakipoteza maisha kwa kushindwa kumudu gharama za matibabu ili hali upo Mfuko unaomwezesha kutibiwa wakati wowote anapougua hata kama hana fedha kwa wakati huo.
Ushauri huo ulitolewa na wadau hao jijini Arusha wakati wa Mkutano wa wadau ambao ulikutanisha wanachama,watoa huduma, wabunge, madiwani na wawakilishi wa vyama vya wafanyakazi.
Akichangia mada zilizowasilishwa na Ujumbe wa NHIF,Mbunge wa Jimbo la Ngorongoro, Ole Telele, alisema kuwa haoni sababu ya kuwepo uhiari wa wananchi kujiunga ili hali asilimia kubwa ya Watanzania ni wagonjwa.
"Jamani inasikitisha tunapoona kuna Mfuko kama huu ambao una uhakika wa matibabu unakuwa na uhiari wa wananchi wenyewe kujiunga, mtakumbuka kipindi cha Babu wa Samunge au Babu wa Loliondo watanzania wengi walimiminika kwenda huko hivyo hii inaonesha ni namna gani tulivyo wagonjwa hivyo kila mmoja kwa nafasi yake ajipange kuhamasisha ili wananchi wetu waingie katika utaratibu wa Bima ya Afya," alisema Telele.
Hoja hiyo iliungwa mkono na Mkuu wa Wilaya ya Monduli, Jowika Kasunga ambaye alisema kuwa endapo kutakuwa hakuna uwajibikaji wa ukweli na wenye nia ya dhati ya kufanikisha suala hili, lengo hilo zuri la wananchi kuwaweka kwenye utaratibu mzuri halitafikiwa.
"Jamani ifike mahali kila mmoja awajibike kwa nafasi yake, haiwezekani fedha nyingi za Mfuko huu ziwe zinakwenda kwenye vituo vya madhehebu ya dini na binafsi huku hospitali zetu zikiambulia fedha kidogo...hapa jibu lake ni kuwa wenzetu wanatoa huduma nzuri ambao wananchi wanaamua kuifuata hivyo ni lazima tulione hili na tulifanyie kazi kuanzia sasa kwani fedha hizi zingeweza kusaidia katika kuboresha huduma za matibabu," alisema Mkuu huyo wa Wilaya.
Katika michango mingine wadau hao waliutaka Mfuko huo kuhakikisha wanashirikiana na viongozi wa ngazi zote na kutoa taarifa za utekelezaji katika maeneo husika ili kutoa changamoto kwa maeneo ambayo hayafanyi vizuri.
"Mfuko huu umekuwa msaada mkubwa kwa wanachama wanaotibiwa nao hasa katika kipindi hiki ambacho gharama za matibabu zimekuwa zikipanda kila kukicha hivyo ni lazima viongozi tuhakikishe tunajadili na kulifuatilia kwa ukaribu sana ili kuwa na uhakika wa afya bora za wananchi wetu," walisema wadau hao.
Hata hivyo, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Hamis Mdee, alisema kuwa Mfuko umejipanga kuhakikisha unashirikiana na viongozi wa ngazi zote wakiwemo wa kiserikali, kisiasa na viongozi wa madhehebu ya dini ili kuhakikisha dhana ya Bima inaeleweka vyema na kufanikisha lengo la kuwahudumia watanzania asilimia 30 ifikapo 2015.
Michuzi hawa jamaa mfuko wa Afya hawana kitengo cha PR? inatakiwa wakulipe sana.kila siku wako michuzi.bajeti yao ya PR wakupatie sio kukupa ofa mbuzi tu.
ReplyDeletemdau BABA J.
uk.