Waziri Mkuu,Mh. Mizengo Pinda.

WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda amesema masharti ya madaktari ya kutaka Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk . Hadji Mponda na Naibu wake, Dk. Lucy Nkya waondolewe nyadhifa zao ndipo majadiliano mengine yaendelee, hayakubaliki.

Pia amewasihi madaktari hao kutoendelea na mgomo leo na badala yake waiachie Serikali iendelee kushughulikia madai yao, likiwamo suala la kubadili uongozi wa wizara hiyo na iwapo wataendelea na mgomo, watambue kuwa maisha ya Watanzania yako mikononi mwao.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Pinda alieleza kushangazwa na kitendo cha madaktari hao kung’ang’ania hoja ya kufukuzwa kwa Dk Mponda na Dk Nkya, wakati waliwasilisha mbele ya Serikali madai mengi na yanayoendelea kushughulikiwa na kutoa mapendekezo ya nini kifanyike.


Alisema alipokutana na madaktari hao aliunda Kamati iliyojumuisha sekta mbalimbali wakiwamo wajumbe wawili wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), wauguzi na wafamasia, kwa ajili ya kushughulikia madai ya madaktari hao na kamati hiyo ilishakamilisha kazi yake.

Hata hivyo, alisema katika mkutano wao wa mwisho na Serikali ulioongozwa kwa upande wa Serikali na Katibu Mkuu wa Wizara ya Menejimenti ya Utumishi wa Umma, George Yambesi, madaktari hao wakiongozwa na Mwenyekiti wa MAT, Dk Namala Mkopi, waligoma kuendelea na mazungumzo wakitaka viongozi hao wasimamishwe.

“Niliambiwa kuwa wakati kikao hicho kinaanza, madaktari waliweka masharti ya kutaka viongozi hawa wasimamishwe ndipo majadiliano mengine yaendelee, nikajiuliza kwa nini wang’ang’anie masharti haya wakati tayari Serikali ilishasema yanashughulikiwa?” Alihoji. Alisema anachofahamu ni kwamba viongozi hao wawili nafasi zao ni za kisiasa na mwenye mamlaka ya kuwateua ni Rais.

“Hivyo kitendo cha Mkuu wa Nchi kupewa saa 72 awe amewasimamisha kazi, kwanza mimi sikubaliani nacho na ninajua hata Rais mwenyewe hatakubaliana nacho,” alisema.

Alisema inafahamika wazi kuwa madai waliyotoa madaktari hao kwake yanafanyiwa kazi na mengi kama vile nyongeza ya posho, posho za mazingira hatarishi, mishahara, posho za usafiri na bima, yanazungumzika na kwamba utaratibu wa kuyafanyia kazi ulikuwa unaendelea.

Alitoa mfano kuwa madaktari hao walitaka posho ya sasa kwa kima cha juu kwa madaktari ya Sh 25,000 kwa siku iongezwe na kufikia Sh 50,000 huku wengine wakitaka ifikie Sh 80,000, jambo ambalo linaweza kushughulikiwa ingawa kwa kupitia kwanza bajeti na hali ya uchumi wa nchi.

“Ndiyo maana nashangaa wenzetu hawa kulileta suala hili leo, wakati tulishatoka nao mbali hadi kufikia kusimamisha kwanza Katibu Mkuu (Blandina Nyoni) na Mganga Mkuu (Deo Mtasiwa), ili kupisha uchunguzi huku madai mengine yakishughulikiwa, kwa masharti haya mapya labda kama wenzetu wana jambo lingine,” alisema.

Aliwaomba madaktari hao waiachie Serikali kazi ya kushughulikia madai yao na kuendelea na kazi leo, lakini wakiendelea na mgomo huo kwa kisingizio cha kuwasimamisha Dk Mponda na Dk Nkya haitaleta picha nzuri kwa Watanzania, kwa kuwa wao ndio waathirika wakuu.

“Kwanza jamani huyu Dk Mponda ndiyo kwanza ana mwaka mmoja na miezi kadhaa tangu awe Waziri wa Afya na mengi ya madai ya madaktari hawa yanaonekana wazi ni matatizo ya muda mrefu, hali ambayo kweli Serikali imeona na kuamua kuijenga sekta hiyo ya afya ili iwe na meno,” alisema.

Alisema amesikia na kupokea ujumbe mwingi kuwa madaktari hao wamepanga kugoma leo huku wakidai kuwa wataikomesha Serikali.

“Naomba watambue kuwa wanachofanya si kuikomesha Serikali, bali kuwakomesha wagonjwa, kwani wao ndio waathirika wakuu, naomba watumie busara na hekima na kurejea kazini, ili kuwalinda Watanzania wasio na hatia.” Alisema ni jambo linalosikitisha kuona madaktari hao ambao wanatambua umuhimu wao kwa Taifa hasa suala la afya, kutumia fursa hiyo ya maisha ya Watanzania kuibana Serikali, kwa kuwa wanafahamu wanaweza kufanya lolote wanalotaka.

Alisema kimsingi, zipo sheria za nchi ambazo zinaweka bayana masharti kwa sekta zinazogusa watu, ikiwamo ya afya wafanyakazi wake kutogoma, kwa kuwa waathirika zaidi wa migomo hiyo ni wananchi ambao hawana hatia. Aliwataka madaktari kutambua kuwa sheria katika eneo hilo iko makini na kuwasihi iwapo wanataka kugoma basi wagome kwa misingi ya kisheria.

“Ila jamani ninawaomba sana madaktari wasigome na kuacha watu wakifa kwa kisingizio cha watu wawili, watambue kuwa huwezi kumpa Rais masharti, hili halikubaliki si hapa tu hata nchi zingine.” Kuhusu Serikali imejipangaje iwapo madaktari hao watagoma leo, Pinda alisema haijajiandaa na lolote kwa kuwa inaamini wataalamu hao watatumia hekima na kuiachia Serikali ishughulikie madai yao na wao kuendelea na kazi.

“Lakini jamani tujipange kwa lipi, kwa kuwa Mponda hajaondoka? Basi kama ni hivyo kuna tatizo kubwa kuliko inavyodhaniwa.” Aidha Pinda alisema mpaka sasa hajafahamu athari za mgomo wa madaktari uliopita na kutaka swali hilo, waulizwe wahusika wenyewe wa sekta ya afya, kwa kuwa wao ndio wanaofahamu jinsi Watanzania walivyoumia.

Chanzo :Habari Leo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 21 mpaka sasa

  1. Sawa

    David V

    ReplyDelete
  2. KINACHONISHANGAZA ZAIDI HAPA NI KIMOJA TU KWANI MPONDA NA lUCY KYA WAO WANAJISIKIAJE KAMA MA DACTALI WATAENDELEA KUGOMA KWA AJILI YA WATU WAWILI NA KUWEKA HATARINI MAISHA YA WATANZANIA??????

    KWANINI WAO WASIJIUDHURU??? KWANI MAISHA YA WATANZANIA HAYANA DHAMANI TENA??? AU WAO NI BORA KULIKO UHAI WA WATANZANIA????

    KUSEMA KWELI HII NI AIBU KUWA MWAFRIKA NA KUWA MTANZANIA KWA UJUMLA

    ReplyDelete
  3. Madaktari wanaheshimika sana sehemu yoyote duniani, nashangaa hapa bongo wanasiasa wanaheshimika zaidi. Kwa hatua iliyofikiwa nadhani Mh. Raisi inabidi aingilie mwenyewe!!!

    ReplyDelete
  4. madaktari mnaidharaulisha fani yenu,na wananchi hawawelei...hizo posho mnazoomba mtakua tofauti gani na wabunge?

    ReplyDelete
  5. Hawa madaktari kweli wakati mwingine hamnazo , wametaka mganga mkuu na katibu wa wizara ya afya wasimamishwe kazi, PM amefanya hivyo, hivi wanafikiri ni wao tu wapo katika hii nchi? ni wao tu ambao ni wafanyakazi katika hii nchi? baadhi ya madai yao serikali imeanza kuyafanyia kazi, nchi yetu bado haijafikia ni maskini uchumi wetu sio mzuri huwezi kulinganisha na nchi za Europe. inasikitisha mno kwanini rais hawafukuzi kazi wote waogoma, maana wanataka kuchochea upotevu wa amani ktk nchi yetu

    ReplyDelete
  6. sione haja kwa nini waziri huyo wa afya na naibu wake wasijiuzulu,wanangojea nini kama wanawatakia mafanikio mema wananchi,huo ni uroho wa madaraka

    ReplyDelete
  7. Sidhani kama madaktari wanasababisha vifo, ni hao wanaokataa kujiuzulu ndo wanasababisha vifo.

    ReplyDelete
  8. Pinda madaktari ni baadhi ya watz wachache waliobahatika kwenda shule na wana ufahamu. Kwa hiyo siasa serikali mnazocheza msidhani hawafaham, wanajua na wako clear kwenye point. We zunguka we lakini madai yao toka mwanzo, dai la kwanza ilikuwa Mponda ajiuzulu, sasa wewe ukaenda kupiga siasa badala ya kazi..haya sasa, kanyaga twende.

    ReplyDelete
  9. Wakati wa Mwalimu cheo kilikuwa na dhamana. Siku hizi cheo si dhamana bali ni kulindana. Kama madaktari hawawataki mawaziri wao, waachie ngazi ili kuokoa maisha ya wagonjwa. Kwa kifupi hakuna tofauti ya Syria na Tanzania hapa. Kiburi cha Rais wa Syria kitafanya watu wafe bila sababu. Lakini siku moja ataondoka tu. Hatatawala maisha. Kiburi cha hawa viongozi kitafanya wagonjwa wapoteze maisha yao, hata wao hawatatawala milele, wataondoka tu. Watu wa haki za binadamu mko wapi? International Criminal Court na Ocampo tumaomba mfuatilie suala hili ili wahusika wawajibishwe.

    ReplyDelete
  10. Kwa mtindo huu, hivi wananchi wakianza kuwapiga mawe viongozi mtawaona wabaya kweli!!!

    ReplyDelete
  11. Watanzania watakufa kwa ajili ya watu wawili tu kugomea vyeo, hivi wanajua kuwa sio vyeo vya kurithi hivyo. Ondokeni jamani wizara imewashinda. Mnaowaongoza hawawataki

    ReplyDelete
  12. Ebu wabunge ni zaidi ya madaktari!!! who said so, madaktari ni zaidi hata ya mama mzazi ndo maana nchi zote zinawaheshimu. Achieni ngazi walengwa tena mkae mbali na doctors wa Tz mkiugua

    ReplyDelete
  13. Safi my mate doctors, wakisha jiuzulu tugome wote tena ili jk aondoke na pinda wake

    ReplyDelete
  14. muda umefika sasa kama waziri mkuu alisema yeye ni mpagania haki za watanzania basi wakati ndio huu. Kwanini watu wawili wasababishe vifo , shida na maumivu kwa wengi. Kama nyie ni mawaziri mnaopenda kazi zenu na heshima zenu basi mjiuzulu maana mnaotaka kuwaongoza hawataki. Time for waziri mkuu usaidie walio wengi na unajua watu wanasema wengi wape.

    ReplyDelete
  15. Siasa bwana! Najua baada ya sharti hili la madaktari litafuata sharti lingine ngumu na sijui itakuwaje.

    ReplyDelete
  16. Udini unawasumbuwa hao madaktari..chunguzeni mtagunduwa...na wapo madaktari wanaofuata mkumbo...! nchi hii..kitanuka siku si nyingi,,..!

    ReplyDelete
  17. Ndio maana JKT ilikuwa muhimu kwa watu kabla hawajaanza kazi. angalia wasomi wasiofanana na matendo yao. Ni bora kutokuwa na madaktari kuliko kuwa na aina hii ya madaktari. fukuza wote, futa vyeti na wasiajiriwe tena na warudishe hela waliosomea.

    ReplyDelete
  18. Katika awamu ya kwanza ya mgomo wa Madaktari niliwaelewa na ujumbe ulifika panapohusika vyema. Mazungumzo yakaanza ila hatua hii ya pili naona Madaktari wamepotea sana. Naheshimu kazi yao lakini this time around wamefurunda. Ikiwa Serikali itaridhia madai ya Waziri na Naibu kutimuliwa ina maana siku za mbeleni itabidi wawe cinsulted na Rais ni Waziri yupi wanayemtaka. THIS IS NOT THE WAY TOTAKE THE GOVT AT RANSOME!!!!Ernest

    ReplyDelete
  19. Mponda, Nkya achieni ngazi jamani ili kuokoa maisha ya wayanzania wasio na hatia.
    Kama mnaowaongoza hawawataki sasa mnamuongoza nani? tumieni akili.

    ReplyDelete
  20. Hapa tatizo ni kwamba hayo madai ya wanaojiita madaktari ni ya kipuuzi na yako nje ya misingi ya taaluma ya kweli ya kidaktari. Sasa baada ya hao wanaotakiwa kujiuzulu wakifanya hivyo halafu itokee kwamba na wauguzi wadai ni lazima daktari fulani aachishwe kazi vinginevyo nao watagoma ndio iwe hivyo? Maendeleo kamwe hayawezi kupatikana kwa namna hii. Watu waende katika majadiliano yenye kufuata misingi ya haki ya kitaaluma na kabisa siasa zisiruhusiwe kuchukuwa nafasi.

    ReplyDelete
  21. Hawa Madaktari naona nao wanakuwa wabinafisi tu,
    Watutuko kwenye secta na ajira za makampuni tunavumilia mambo mengis sana, unaingia ofisn sa2 uantoka jioni unafika kwako sa mbili na hela mbuzi mkononi,
    Hawa wanachoataka ni kwa vile Hao vingoz wanawabana kufanya kazi katika hospital binafsi wakati wa kazi,wanawaacha wangonjwa wanakimbilia kwenye hospital binafs ili wapata hela,
    Hilo ndo jambo kubwa wanalotaka hao jamaa waondoke ili waweze endelea fanya kazi hospital nying ndani ya mda wa kazi, na inasemakam wapo wengine wakipigiwa simu wawapo hosptla like Muhimbili hutoka na kuaga kuwa wana emergencey na kwenda kufanya kazi hospital Binafis for emergency call ambayo wanalipwa zaid,
    Inafika mda tunawasiwasi na msingi wa madai yao ni nini, Wawe na msimamo kama wasomi,huwezi kumpa Raisi amri ya kufanya utakavyo ili awafukuze kazi Fulani na Fulani ili wewe ufanye kazi.
    Kuweni wasomi wa kweli na toeni hoja za msing,matatizo yenu yanashughulkiwa ,nyinyi nini tatizo sasa kusubiria matokeo ama kufuatilia,
    Isitoshe mna wawakilishi kwenye kamati ya kushughulikia matatizo yenu,
    Kwani hao nao hawawapi feedback,
    Tunajua mapungufu ya Serikali yetu ila kwa hili shinikizo lenu hapana,hamjafikiria vizuri zaidi mnajenga chuki na wanachi kwa sasa

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...