Mwalimu wa Taaluma wa Shule ya Sekondari Maneromango iliyopo Kata ya Maneromango, Wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani, Jonas Buheruko akifanya mahojiano na Ripota wa Globu ya Jamii (hayupo pichani) jana ofisini kwake.
Baadhi ya wanafunzi wa kidato cha nne wa Shule ya Sekondari Maneromango iliyopo Kata ya Maneromango, Wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani wakifanya mitihani yao ya majaribio ya robo muhula jana.

Na Joachim Mushi - Kisarawe

WANAFUNZI 159 wa Shule ya Sekondari Maneromango wametoroka kufanya mitihani ya majaribio ya robo muhula iliyoanza juzi katika shule hiyo.

Wanafunzi hao ambao ni vidato mbalimbali kuanzia cha kwanza hadi cha nne,ni kati ya wanafunzi 383 wa Shule ya Sekondari Maneromango waliotakiwa kuanzia kufanya mitihani yao Machi 27, 2012 shuleni hapo.

Akizungumza katika mahojiano na Ripota wetu katika shule hiyo iliyopo Kata ya Maneromango, Wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani,Mwalimu wa taaluma wa shule hiyo, Jonas Buheruko alisema ofisi yake imebaini utoro huo baada ya kukusanya taarifa kutoka vidato vyote.

Akifafanua alisema hali hiyo ya utoro na hasa wanafunzi kukimbia mitihani hujitokeza mara kwa mara jambo ambalo limekuwa miongoni mwa vikwazo vya shule hiyo kufanya vizuri kitaaluma.

Alisema taarifa zilizokusanywa siku ya kwanza kuanza kwa mitihani hiyo,Machi 27 mwaka huu, zimebaini kidato cha nne ndiyo wanaoongoza kwa utoro wa mitihani kwani kati ya wanafunzi 106 waliotakiwa kuanza kufanya mitihani hiyo ya majaribio ni 45 pekee walifanya huku 65 wakiingia mitini.

"Taarifa zangu nilizokusanya baada ya kuanza tu kwa mitihani zinaonesha kidato cha kwanza wametoroka wanafunzi 10 kati ya 81, kidato cha pili wametoroka 31 kati ya 103, kidato cha tatu wametoroka 53 kati ya 93 waliotakiwa kuanza kufanya mitihani hiyo," alisema Mwalimu Buheruko.

Hata hivyo alisema kitendo cha utoro wa mithani shuleni hapo sasa kinaendelea kuwa sugu licha ya walimu kufanya jitihada za kuwafuatilia wanafunzi na kutoa adhabu mbalimbali kulingana na taratibu za shule.

Aidha aliongeza mwaka 2011 wanafunzi 34 wa kidato cha nne kati ya 85 walikimbia kufanya mtihani wa majaribio wa Wilaya shule hapo jambo ambalo linawakatisha tamaa walimu katika utoaji wa elimu shuleni hapo.

"Wamekuwa wakikimbia mitihani mara nyingi...tunawapa adhabu lakini wapo radhi kufuraia adhabu unayowapa kuliko kuja kufanya mitihani...wakati mwingine tunapozidiwa tumekuwa tukipeleka majina ya watoro kwa Mwenyekiti wa Kijiji na Ofisa Mtendaji wa Kata lakini bado hatujaweza kudhibiti utoro huu," aliongeza mwalimu Buheruko.

Akizungumzia hali hiyo, Mratibu wa Elimu Kata ya Maneromango, Nicolaus Lemma amesema wamekuwa wakiwaita mara kadhaa wazazi wa wanafunzi na kuwashtaki pale inapobainika wanachangia utoro wa watoto wao, ila tatizo hilo si kwa sekondari pekee bali hata shule za msingi eneo hilo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 6 mpaka sasa

  1. Uongozi wa shule hiyo una matatizo. Haiwezekani kwa shule yenye uongozi makini kuwa na kiwango kikubwa cha utoro kiasi hicho. Au pengine ndio moja ya zile shule ambazo zina uhaba mkubwa wa waalimu?

    ReplyDelete
  2. Nakubaliana na Mdau na tishio la Azabu sio tatizo la kufanya kusiwe na Utoro sehemu zisizo na Elimu kama hizo zinatakiwa kuwekwe upendo ili wawe wanapenda Shule na umakini wa wanafunzi na wanafunzi gani wanapata tabu kwenye Elimu wasaidie kwa namna gani na mbinu zipi Elimu muhimu tusikate tamaa nao, mie nakubaliana na mdau Walimu ni wachache na siku hizi Walimu wanachagua wapi wasomeshe.

    ReplyDelete
  3. No wonder hiyo shule katika national mwaka jana ilikuwa haina division 1,2 and 3 bali ilikuwa na division 4 sita na division 0 106

    ReplyDelete
  4. Tusilaumu walimu jamani..kama wazazi hawafuatilii maendeleo ya watoto wao,hayo ndio matokeo..mbona mikoa mingine utoro sio kama hao??kama mzazi hajui maana ya elimu unategea nini?pole kwa walimu kwani jitihada zao zote kwa malipo duni wayapatayo,bado tena mnapewa lawama kwa utoro wa wanafunzi..wameripoti mpaka kwa watendaji wa kiserikali wa eneo lao ili wapate msaada lakini hakuna...kijiji/kata wawaambie umuhimu wa elimu wakazi wa eneo lao..

    ReplyDelete
  5. Wengi wa watoto hawa ni kabila gani? inaweza kuchangia.

    ReplyDelete
  6. Heko Maneromango kwa kufikika:

    Ni wakati sasa hizi huduma za MICHUZI BLOGSPOT WIFI ziwafikie watu wengi kadiri iwezekanavyo zaidi ya hapo Maneromango!

    Libeneke oyeeeeeeeee!!!!!!!!!!

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...