Habari Ankal pamoja na timu nzima ya Globu ya Jamii,

Naomba mniwekee mada yangu hii kwenye libeneke la mtandao wa Globu ya Jamii ili kilio chetu kisikike.

Mimi ni mwananchi wakawaida ninayebangaiza maisha hapa mjini kama na wenzangu wengine. Miaka ya nyuma hakukuwa na shida ya usafiri kama ilivyosasa. Naomba kuuliza Sumatra kwanini waliamua kufuta TLB za Hiace na wakati wakijua zilikuwa ni msaada mkubwa kwa wananchi? 

Pili sasa hivi na coaster hazilipi TLB kisa eti wanataka magari makubwa zaidi ya coaster? Hivi hiki nipindi cha kufanya hivyo na maisha yalivyo magumu au Sumatra kushirikiana na Serikali wanataka kupunguza wananchi mjini?

Kwakweli hatuwaeliwi hata kidogo. Kama mwananchi kwa sasa anatumia nauli zaidi ya 5000 kwa siku hiyo ni haki? na wanapokataa kusajili hizo coaster eti nazo ziende pembezoni mwa mji mnafikiri mnachotengeneza kwa wananchi ni nini, kama sio kufikia wakati tukachoka na tukachukua sheria mkononi. 

Fikiria kutoka mwenge kwenda Bunju au Tegeta nauli 1000 au 1800 saa za jioni magari yanakuwa hamna hapo hatujaweka nauli ya kutoka mjini au sehemu nyingine. Hivi Sumatra mnapenda maisha yetu au kila mkiamka mnafanya maamuzi yenu mnavyotaka ilimradi wananchi wanapata shida. 

Madiwani, Wabunge tuliowachagua mko wapi? Hii shida haikubaliki hata kidogo maisha yamekuwa magumu. Kuna watu wameenda kuomba TLB za mwenge Bunju,Makumbusho Bagamoyo magari yao yamenyimwa eti ni madogo mpaka yawe na uwezo wa kubeba abiria kuanzia 30. 

Kwanini wamiliki wa magari kama coaster au Hiace hawathaminiwi? Tunaomba kujulishwa zaidi.

Mdau 
mwenye machungu na hadha ya usafiri nchini

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 13 mpaka sasa

  1. Mdau MuhimuApril 12, 2012

    Tukubaliane na ukweli kuwa Hiace hazina tija kwa usafiri wa mjini kama ambavyo tungekuwa na magari makubwa.

    1. Hiace zilikuwa zikisababisha foleni na kero hasa katikati ya Jiji kutokana na wingi wake na tija kuwa cha kiwango cha chini mno.

    2.Hiace ina uwezo wa kuchukua abiria hadi 15 wakati basi kubwa moja mfano double coaster ina uwezo wa kubeba abiria zaidi ya mara 2 ya kipanya hivyo ni bora kuwa na mabasi machache yenye uwezo wa abiria wengi kuliko kuwa na 'vipanya' vingi katikati ya jiji vyenye uwezo mdogo wa kubeba abiria.

    3. Suala la Coaster kutokuwa na leseni (TLA) kutokana kigezo cha umri wa gari( sheria inakataza kusajili gari la abiria ambalo lina umri zaidi ya miaka 10 tangu kutengenezwa kwake) hilo ni la kisheria zaidi na wala sidhani kama linaweza kuwa kigezo cha kuondoa sheria hii ya kusajili magari ya zamani bali pale linapokamatwa likifanya 'kazi' bila leseni halali ya SUMATRA basi sheria huchukua mkondo wake.

    4. SUMATRA wala serikali haina lengo la kumuondoa yoyote mjini na haitakaa ifanye hivyo bali itaendelea kusimamia sheria zilizopo ambazo msingi wake ni kuwalinda wananchi na SIO kuwafukuza.

    5. Umma unatakiwa uelewe kuwa katika mkakati wa kuanza kwa usafiri wa mabasi yaendayo KASI hata haya mabasi tunayoyaita 'makubwa' kwa sasa yataonekana madogo na yatatakiwa kuondoka katikati ya JIJI ili kupisha usafiri wa mabasi makubwa zaidi ambayo yatukuwa na uwezo wa kubeba abiria zaidi ya 75.

    Mdau uliyeandika taarifa hii elewa kuwa kwa sasa wahusika wadau wa usafiri DSM wanaangalia wapi pa kupeleka magari haya tunayoyaita makubwa kwa sasa na MADA za VIPANYA ilishafungwa siku nyingi.

    Mdau muhimu - DSM

    ReplyDelete
  2. Mzee wa BunjuApril 12, 2012

    Hakya Mungu huyu jamaa sio kwamba anatuonea HURUMA ya usafiri JIJINI bali USONGO na SUMATRA' kwa kumkatalia kusajili 'KIMEO' chake.

    Pole sana hata mie nilienda pale Mwalimu house wakanikatalia katakata hata hivyo baada ya kuelekezwa vizuri na vijana wa pale niliona wao kama SUMATRA hawana ubaya katika hili bali ni serikali iliamua na wao ni watekelezaji.

    Tunatakiwa tulie na serikali hasa wizara iruhusu tusajili magari hayo.

    ReplyDelete
  3. NADHANI WEWE SI MWANANCHI WA KAWAIDA KAMA UNAVYODAI BALI NI MMOJA WA WAMILIKI WA HIACE NA HIZO COASTER !!!

    ReplyDelete
  4. Pole sana Mdau, kwa hiyo unataka niamini kuwa unataka hata mikweche isajiliwe ituuwe kwa kuwa tu umeagiza kigari kibovu?

    Magari ya kubeba abiria duniani yana umri wake na sio kiholela kama unavyotaka wewe.

    Sidhani kama kusajili hayo magari unayosema yakisajiliwa yataondoa nauli kubwa za daladala kwani kinachotakiwa hapa ni usimamizi wa sheruia tu.

    Usitafute kisingizio eti kuna urasimu ili magari ambayo hayastahili yatubebe na hatimae hatuue!

    ReplyDelete
  5. hizo coaster na Hiace hazina mpango wwte. ungesema lini serikali itaboresha usafiri kama ilivyokuwa uda!? kwani hizo hiace,coaster,bajaj,bodaboda ni uchafu tu kwanza barabara zetu hazitoshelezi ghasia zote hizo. hapo ni nabasi ya uhakika kama uda na tax tu.kuepusha ajali zisizokuwa na lazima tuige maendeleo tusiige uchafu wa mumbai na lagos.

    ReplyDelete
  6. Hekima ManApril 12, 2012

    hahahaaaaaaaaaaaaaaaa!!!!!
    jamaa kanichekesha sana, kumbe ni 'gia' ya kusajili msala wake.
    Cha kufanya nenda polisi then mahakamani wakupe HATI ya mahakama ili ulsajili gari lako kimkato!

    ReplyDelete
  7. Mdau tatizo ubwa ni kuwa Mfano ktk Shirika linaloendesha Michezo ya Bahati na Kuchagua Washindi kwa kawaida pana Vigezo lazima vizingatiwe ili matokeo yasiwe na Dosari:

    Mfano Hairuhusiwi wao kushiriki miongoni mwa Wahusika Wafanyakazi wa Kampuni husika na Familia zao ktk Kampuni nayofanya michezo hiyo.

    Tatizo linakuja pale kuwa Ma Bosi hao hao wa SUMATRA ndio wamiliki wa Mabasi makubwa wao na Wajomba zao na ndugu zao wa Kiiukoo hivyo sera zote hizo lengo lake ni kuwahakikishia Ulaji wao wenyewe na miradi yao nje ya kazi na ndugu zao wa karibu.

    HIVYO HUU NI UTARATIBU WA KUJIMEGEA MAPANDE YA KIMAISHA, AU MTU ANACHEZA MPIRA UWANJANI ANAPIGA MPIRA WA KONA HALAFU YEYE MPIGAJI WA KONA ANAWAHI KUFUNGA GOLI NA ANAFANIKIWA BAO LINAZAMA WAVUNI HUKU REFA NA MAKAMISAA WAKISHUHUDIA MUUJIZA WA MWAKA KIASI CHA WAO KUBAKI WAKITUMA REKODI YA TUKIO HILO LA KIOJA HUKO MAKAO MAKUU YA SHIRIKISHO LA FIFA ISWISI !

    ReplyDelete
  8. Big up SUMATRA! Majiji yanatakiwa yawe hivyo. Ondoa coaster zote na vipanya vyote. Mwisho wa siku mabasi makubwa ndo yabaki mjini. Kwa kufanya hivyo mtapunguza magari mjini na foleni itapungua sana. Maana kama mabasi makubwa yatakuwa yakutosha, hata mimi sitakuwa na haja ya kwenda kazini kwa gari binafsi. Huyu anayelalamika huenda ana kipanya chake anataka kukisajili lakini kakataliwa. Nchi haiwezi kwenda kwa kuangaliana usoni bwana.

    ReplyDelete
  9. Ulivyoanza umeonekana kama mtumiaji wa vyombo vya usafiri lakini ulivyoendelea umegeuka na kuwa mmiliki wa usafiri uliotengwa na sumatra/serikali.

    ReplyDelete
  10. Mimi nadhani wewe ni mmojawapo wa wamiliki wa Hiace au Coaster walikaotaliwa TLB. Sidhani kwamba lengo ni kupunguza watu mijini bali utitiri wa vipanya na kuimarisha usafiri mijini. Hata hivyo kwani kuna ubaya gani kuishi vijijini?. Inasikitisha kwamba UDA iliachwa iangamie, vinginevyo wakazi wa miji mikubwa hasa Dar watanufaika zaidi na kuwepo kwa mabasi makubwa kama ilivyokuwa enzi ya UDA. Hongera serikali kwa kupiga stop vipanya na Coaster

    ReplyDelete
  11. Uchafu wa mazingira ni pamoja na kuwa na vipanya(Hiace), vingi na vina beba watu kidogo kidogo, idadi kubwa ya vipanya vinaendeshwa hovyo, wanakugonga ukienda polisi hufanikiwi kulipwa. Vingi vibovu moshi mtupu mjini husababisha muda wa mtanzania kuishi kuwa mfupi, kuvidhibiti na kuvisimamia ni ngumu.Jibu ni mabasi makubwa na yaende kwa muda na ziimarishwe njia za kupita na baiskeli ili wengine tuache magari nyumbani tutumie baiskeli kufika makazini na kudumisha afya zetu. Degelavita.

    ReplyDelete
  12. Jamani hapa mjini Dar es Salaam, foleni sisizo kuwa na sababu maalumu zimezidi bora tu hiace pikipiki na hizi costa zizuiliwe yaje magari ya mwendo kasi ili tuwahi kwenda kazini na jioni tuwahi nyumbani. Nyie wamiliki mnabishana bure wakati utafika jiji litakuwa safi hizo pikipiki/daladala zenu zitakuwa za kibaha na mlandizi chamazi tuangoma nk. Siku ikifika mwendo kasi kwa kwenda mbele.

    ReplyDelete
  13. mdau mtoa mada itabidi utupende watanzania kwa umbumbumbu wetu wengi tumekushambulia lakini ndio sisi tunaolalamika asubuhi usafiri unapokuwa wa shida au tunapolipishwa nauli zaidi kwenye NOAH ambazo ni ndogo kuliko HIACE, ndio sisi wenyewe tunaopanda mikweche ambayo ni mikweche kuliko lako ambalo hata hatujaliona lakini tumeliita mkweche/kimeo pale ambapo usafiri unapokuwa mgumu. tumekushambulia kwasababu tumekwisha fika maofisini kwetu kwa hiyo tumesahau usumbufu tulioupata asubuhi. naomba utupende tu kwani haya yote yanatokana na uwezo wetu wa kufikiri kuhusu haya yafuatayo; nini kinaathiri uzima wa gari, umri wa gari au matunzo inayopata gari? jibu tutalipata tukitembelea maonyesho ya magari. nani anatakiwa kununua mabasi hayo makubwa, wafanyabiashara wa daladala tu au hata serikali? kama sheria hii ni kwa wote mbona UDA hawana mabasi makubwa na ni ya serikali? kama ni kwa wafanyabiashara wa daladala tu, serikali inawasaidia vipi ili wawe na uwezo wa kununua mabasi hayo makubwa? je tunapokataa kuisajili gari yako, ni ajira ngapi tumepoteza? hatutaki mabasi yaliozidi miaka 10, je tuna viwanda vingapi vya magari kwamba tunaweza tengeneza yetu? je hatuna watu wenye elimu na uwezo wa kukaguwa mabasi kabla hayajasajiliwa ili kubaini kuwa basi hili halifai hata kama lina umri mdogo au linafaa ingawa lina umri mkubwa? mdau mtu mmoja mwenye akili timamu kwenye kundi la vichaa, vichaa watamuona yeye ndio kichaa na wao vichaa ndio wazima.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...