DIWANI wa kata ya Endiamtu mji mdogo wa Mirerani Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara,Lucas Zacharia akipiga mpira kuashiria uzinduzi wa michuano ya Umiseta wilayani humo ambapo alijitolea sh300,000 ya seti ya sare za michezo na mipira kwa timu ya wilaya hiyo.picha na woinde shizza,arusha.
Na Woinde Shizza,Arusha
WACHEZAJI 40 ambao ni wanafunzi wa shule za sekondari wa wilaya ya Simanjiro Mkoani hapa wamechaguliwa kuiwakilisha wilaya hiyo kwenye michezo ya shule za sekondari (Umisseta) itakayoanza kutimua vumbi hivi sasa.
Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa kuelekea wilayani Mbulu kwenye michuano hiyo,Ofisa Elimu wa sekondari (Taaluma) wa wilaya Simanjiro,Jilanga Mwantandu alisema wilaya hiyo itashiriki kwenye michezo ya mpira wa miguu,mpira wa pete na riadha.
Mwantandu alisema kuwa kwenye mchezo wa soka watakuwa na wachezaji 18,mpira wa pete wachezaji 12 na wanariadha 10 ambao wametoka kwenye timu tofauti za shule za sekondari za wilaya hiyo.
Diwani wa kata ya Endiamtu mji mdogo wa Mirerani,Lucas Chimbason Zacharia alijitolea sh300,000 kwa ajili ya timu hiyo kununua vifaa vya michezo fedha ambazo zilitolewa kwa niaba yake na mwakilishi wake,Japhary Matimbwa.
Akizungumza wakati wa kufunga michuano hiyo,Mkuu wa kituo cha polisi Mererani Mrakibu msaidizi,Ally Mohamed Mkalipa aliwaeleza wanafunzi hao kuwa michezo na masomo ni vitu ambavyo vina uhusiano mkubwa.
“Wakati nikisoma sekondari kama ninyi mimi nilikuwa nikicheza mpira wa kikapu hivyo tambueni kuwa michezo itawafanya mfanye vizuri darasani na wale mliochaguliwa kutuwakilishwa msituangushe mjitahidi,” alisema Mkalipa.
Pia Mkuu huyo wa kituo cha polisi Mirerani Mkalipa aliwapa motisha ya sh10,000 kila mmoja kipa bora wa michuano hiyo,Jalal Omar mfungaji bora Vincent Joseph na Kasimu Hamis mchezaji mwenye umri mdogo.
Akifunga mashindano hayo kwa niaba ya diwani wa kata ya Endiamtu Lucas Chimbason Zacharia mwakilishi wake Jafari Matimbwa alisema Diwani wa Kata ya Endiamtu Lucas amekubali kuwa mlezi wa timu ya Umiseta ya wilaya hiyo na hata kipindi cha mwaka ujao wa mashindano hayo atakuwa pamoja nao.
Matimbwa aliwataka wachezaji wa timu ya wilaya hiyo ambao hawakuchaguliwa kwenye timu hiyo wasijisikie wanyonge kwani wote wameonyesha kuwa wanauwezo ila nafasi zilizotolewa ndiyo chache.
Aliwataka watakaowakilisha wilaya hiyo kwenye umisseta mkoa wa Manyara kuonyesha nidhamu na pia wale ambao hawakuchaguliwa waongeze juhudi ambapo pia zaidi ya kumpa sh10,000 mchezaji mdogo zaidi ya wote kwenye michuano hiyo Kasimu Hamis wa shule ya sekondari Mirerani Benjamin Mkapa alimuahidi kumnunulia vifaa vya michezo ili kuendeleza kipaji chake.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...