Naja kwenu waungwana, nawapa yangu salamu,
Nawasalimu watwana, walimu na Maimamu,
Shukurani kwa Maulana, kwangu hakuna ugumu,
Ipi tofauti yao, kibogoyo na mapengo.
Najiona zumbu kuku, kubaini tofauti,
Namuuliza Bukuku, yupo kimya amenyuti,
Ahadi kutoa buku, kwalo jibu madhubuti,
Kibogoyo na mapengo, ipi yao tofauti.
Swali kwa Bini Zuberi, kapekue vitabuni,
Kafungue na Zaburi, kupata jibu makini,
Wala sione hatari, uliza wanazuoni.
Kibogoyo na mapengo, ipi yao tofauti.
Nawe Tedi wa Mapunda, mapengo unayajua,
Naijo yamempenda, Nesrori nae anajua,
Mlo mkuu ni matunda, na uji si tunajua,
Kibogoyo na mapengo, ipi yao tofauti.
Steji ameivuka, ankali wangu Tevini,
Mdomoni yashatoka, kayatupa shimoni,
Meno yalisha mtoka, asubiri uzeeni,
Kibogoyo na mapengo, ipi yao tofauti.
Ya mtoto yakisha toka, huota ya ukubwani,
Hata akila bazoka, hayanguki sakafuni,
Pengo hili kuzibika, kawaida maishani,
Kibogoyo na mapengo, ipi yao tofauti.
Pengo hili pengo gani,halizibiki ukubwani,
Kibogoyo mtu gani, hapa kwetu mtaani,
Meno hana asilani, babu yake Selemani,
Kibogoyo na mapengo, ipi yao tofauti.
Yamesha watoka meno, kibogoyo na mapengo,
Hakuna alo na meno, kuota hayana mpango,
Vibunye hawana meno, wazee wapinda mgongo,
Kibogoyo na mapengo, ipi yao tofauti.
Kadi tama tamatia, kalamu naweka chini,
Jibu siache patia, na kunitoa shakani,
Wengi tunayapitia, kukosa meno kinywani,
Kibogoyo na mapengo, ipi yao tofauti.
Mroki Mroki ‘Father Kidevu’




Kwanza mshukuru "Mola", sozawa so mshirika,
ReplyDeleteVyote anovitawala, bayana vilofichika,
Kutowa hana khiyana, humpa anomtaka,
Kibogoyo meno hana, mapengo ziba hakika!
Achia ya utotoni, muda kifika hung'oka,
Yakaota ya thamani, mazuri ya uhakika,
Kipanguka ukubwani, kinywa shoo imetoka,
Kibogoyo meno hana, mapengo ziba hakika!
Tofauti kubwa sana, pasina tochi kutaka,
Yaonekana bayana, kiuliza takucheka,
Pengo hutambulikana, penye jino likitoka,
Kibogoyo meno hana, mapengo ziba hakika!
Yang'okapo ukubwani, ndipo huanza mashaka,
Ya mbele au ya ndani, mapengo hatamu shika,
Kiwa nazo mfukoni, la dhahabu taka weka,
Kibogoyo meno hana, mapengo ziba hakika!
Mapengo ziba waweza, kinywacho hasitirika,
Ngungutuwa ukaweza, mihogo na kadhalika,
Kenuwa hawa wa kwanza, japo silo la kucheka
Kibogoyo meno hana, mapengo ziba hakika!
Mapengo hubaki jino, si yote sema hang'oka,
Si kibogoyo mfano, denda anochuruzika,
Mpe ugali wa ngano, tafuna taungulika,
Kibogoyo meno hana, mapengo ziba hakika!
Kibogoyo hana meno, ndafu sije mualika,
Mpapase kwa mkono, ukitaka uhakika,
Hana japo la mfano, seuze la kubandika,
Kibogoyo meno hana, mapengo ziba hakika!
Hubakia fizi tupu, jishauri taka cheka,
Nyama mwiko kwenye supu, mishikaki huondoka,
Kwake madhila matupu, busu atahangaika,
Kibogoyo meno hana, mapengo ziba hakika!
Tamati nnasimama, nisije nikapituka
Tofauti itazama, kwa wengi mekubalika,
Ikubali si lazima, ila wazi nimeweka,
Kibogoyo meno hana, mapengo hwenda zibika!
nani watwana wewe?
ReplyDelete