Sheikh Hamis Mattaka (kushoto) akitoa tamko mbele ya waandishi wa habari kwa niaba ya Mwenyekiti wa jopo la Masheikh wanazuoni wa kiislam Tanzania kuhusu mchakato wa kukusanya maoni ya Katiba, Sensa ya watu na Makazi na Hali ya Zanzbar leo jijini Dar es Salaam. Kulia ni Sheikh Iddi Simba.

Na. Aron Msigwa – MAELEZO,Dar es Salaam.

Taasisi ya masheikh na wanazuoni wa Kiislamu Tanzania imeunga mkono kauli iliyotolewa hivi karibuni na Sheikh mkuu wa Tanzania, Mufti Issa Shaaban Simba ya kuwataka waislamu na watanzania kote nchini kushiriki kikamilifu katika Sensa ya watu na Makazi itakayofanyika Agosti 26 mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam kwa niaba ya mwenyekiti wa jopo la masheikh na wanazuoni wa Kiislamu Tanzania Sheikh Hamis Mattaka amesema hatua hiyo inafuatia kuwepo kwa baadhi ya makundi yanayowahamasisha waumini wa dini ya kiislamu na wananchi kutoshirika zoezi la Sensa ya watu na makazi.

Amesema wao kama jopo la wanazuoni hawaoni tatizo la zoezi hilo kutokana na umuhimu wake kwa taifa na kuongeza kuwa Sensa ya watu na makazi ipo kwa mujibu wa sheria za nchi na imepitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Jopo hilo limeiomba serikali kuweka sheria itakayozuia utoaji wa takwimu zinazohusu dini za watanzania zinazotolewa na vyanzo mbalimbali ndani na nje ya nchi kwa kuwa kipengele hicho si sehemu ya sensa nchini.

“Tunajua kuwa serikali ilikua na nia njema kukiondoa kipengele cha dini katika Sensa hapana budi nia njema hiyo ya serikali ilindwe kwa kuweka sheria itakayozuia kutoa takwimu zinazohusu dini za watanzania” amesema Sheikh Mattaka.

Amefafanua kuwa Sensa ya awali ya mwaka 1957 kipengele cha dini kilihusishwa na baadaye kuondolewa katika Sensa zilizofuata kwenye madodoso ya kukusanyia takwimu za kaya.

“Sisi kama jopo kila siku tunasema ili twende salama kama wananchi wa nchi hii ni wajibu wetu kuheshimu na kufuata sheria kwa maana ya kutii sheria bila shuruti, kwa hiyo tunasema Sensa ya watu na makazi ni jambo la kisheria si jambo la mitaani, hatuwezi kulumbana na kujadili jambo ambalo liko wazi kisheria na limepitishwa na wabunge tuliowachagua sisi wenyewe”.

Amefafanua kuwa zoezi la Sensa ya watu na makazi litaiwezesha serikali kupanga mipango ya maendeleo kwa kuwa na takwimu sahihi za watu na makazi, hali ya kipato cha kaya, vizazi na vifo na pia kuiwezesha serikali kwapatia huduma bora wananchi wake.

Katika hatua nyingine jopo la masheikh na wanazuoni wa Kiislamu Tanzania imewataka wananchi kushiriki kikamilifu katika mchakato wa ukusanyaji wa maoni ya katiba.

Aidha jopo hilo limewataka watanzania wote kwa ujumla kuitumia fursa hiyo muhimu kutoa maoni ambayo yataiwezesha nchi kupata katiba itakayokidhi matakwa ya wananchi.

“ Sisi kama jopo la wanazuoni wa kiislamu tunawataka waislamu na watanzania wote kwa ujumla kuitumia fursa hii muhimu kwa kutoa maoni yao ili hatimaye nchi yetu ipate katiba itakayokidhi matakwa ya wananchi kwa miaka mingi ijayo” amesema Sheikh Mattaka.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 7 mpaka sasa

  1. AnonymousJune 30, 2012

    Namimi ni mkristu lakini nawaunga mkono hawa wananzuoni wanaonekana wanapoint za msingi.... kwasababu haya maswala ya huyu dini hii yule dini ile, hayana msingi wowote ule zaidi ya kutugawanya na kuvunja utaifa wetu kwa hasara yetu na kwa faida ya watu wachache ambao aidha ciyo watanzania au ni watanzania wasio wazalendo au watu wasioitakia mema tanzania .Mungu ibariki tanzania Mungu ibariki Afrika

    ReplyDelete
  2. AnonymousJune 30, 2012

    mdau hapo juu huna point na funga mdomo wako, tukitaka sisi waislam tujulikane tuko wangapi nyinyi mnasema udini , wakati wa maslahi nyinyi mnakimbilia kusema wakristo wako wengi zaidi kuliko waislam ...
    iko siku tutapata haki yetu waislam.

    ReplyDelete
  3. AnonymousJune 30, 2012

    Takukuru wafanye kazi yao! inaonekana kuna watza wenzetu wamechukua rushwa ili wahamasishe washindano ya kuzaa baina ya wakristu na waislamu.

    ReplyDelete
  4. AnonymousJune 30, 2012

    ipo haja ya kujua ıdadı kamılı ya wa dını za watanzanıa kwa asılımıa zaosıonı tatızo maana marekanı na ulaya wanajua ıdadı hıı na wameanıka ktk vyombo upelelezı IWEJE SISI WENYEWE TUSIJUE???MMECHEMSHA JOPO LA MASHEKHE

    ReplyDelete
  5. AnonymousJuly 01, 2012

    Mimi ni muislamu, nadhani hakuna ubaya kuuliza dini ya mtu katika sensa, ni muhimu kuwa na takwimu za idadi ya waislamu, wakristo, wahindu, wapagani n.k, vitu ambavyo si muhimu kuulizwa katika sensa ni kabila na rangi ya mtu.

    ReplyDelete
  6. AnonymousJuly 01, 2012

    Hapa utaona tofauti ya mwislamu msomi na mwislamu umwinyi anayekalia majungu na kutafuta fitina ya kuwagawa wananchi. Big Up jopo la Waislamu wasomi. Tuwaelemishe na wengine wafikiri kama UA Emirate. Huko ndo dunia inavyokwenda.

    ReplyDelete
  7. AnonymousJuly 01, 2012

    Mi naona katika siku Za hivi karibuni, suala la dini limeshika hatamu. Jamani tunayemwamini ni Mungu mmoja (Waislamu na Wakristu). Uzuri wote tunafahamu kuwa Tz ni non-religious country. Kwahyo Kama unataka ukristo nenda Vatican kaishi na Kama unataka uislamu nenda Arabic countries. Hapa hakuna udini, ukabila wala utaifa ndio maana unaona mataifa yote yanayotutembelea yanafurahi kutembelea kwetu. Mungu Ibariki Tz, Mungu Tubariki sote wananchi tupendane Kama siku zote tunavyopendana na kuheahimiana. Asanteni wakuu wetu Mufti Issa Shaaban Simba

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...