Tume ya Mabadiliko ya Katiba inatarajia kuanza kufanya mikutano na wananchi wa mikoa minane kuanzia siku ya Jumatatu, Julai 2, 2012 hadi Jumatatu, Julai 30, 2012 kwa lengo la kukusanya maoni yao kuhusu Katiba MpyaMikoa hiyo ni Dodoma, Kagera, Kusini Pemba, Kusini Unguja, Manyara, Pwani, Shinyanga na Tanga. Katika mkoa wa Dodoma, Tume itaanza na Wilaya ya Bahi; Katika mkoa wa Kagera Tume itaanza na wilaya ya Biharamulo; Katika mkoa wa Manyara Tume itaanza na wilaya ya Mbulu na katika mkoa wa Pwani Tume itaanza na wilaya ya Mafia.
Kwa mkoa wa Shinyanga Tume itaanza na wilaya ya Kahama na kwa mkoa wa Tanga, Tume itaanza na Wilaya ya Lushoto. Kwa Zanzibar, Tume itaanza kukusanya maoni katika mkoa wa Kusini Unguja katika wilaya ya Kusini.
Taratibu zote za kuanza kazi zimekamilika zikiwemo kuandaa ratiba na kuisambaza katika mikoa na wilaya husika. Wajumbe wa Tume na watumishi wa Sekretarieti wamejigawa katika makundi saba. Kila kundi litafanya mikutano katika mkoa mmoja isipokuwa kundi moja litakalofanya mikutano katika mikoa miwili ya Kusini Unguja na Kusini pemba.
Tume inawaomba wananchi kuhudhuria mikutano itakayoitishwa na Tume na kushiriki kikamilifu katika kutoa maoni yao kwa uwazi, uhuru na utulivu.
Pamoja na kuwasilisha maoni kupitia mikutano itakayoitishwa na Tume, wananchi pia wanaweza kuwasilisha maoni yao kupitia tovuti ya Tume (www.katiba.go.tz) au kwa njia ya posta kupitia anuani za zifuatazo:
Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Makao Makuu,
Mtaa wa Ohio,
S.L.P 1681,
DAR ES SALAAM,
Nukushi: +255 22 2133442;
Au Jengo la Ofisi ya Mfuko wa Barabara,
Mtaa wa Kikwajuni Gofu,
S.L.P. 2775, Zanzibar,
Simu: +255 224 2230768,
Nukushi: +255 224 2230769



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...