Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Balozi Salim Ahmed Salim, akizungumza kuhusiana na utoaji wa maoni ya Mabadiliko ya Katiba ya Tanzania katika mkutano huo uliofanyika viwanja vya Mtende.
Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Tanzania Dk Mvungi, akitowa maelezo kwa Wananchi wa Kijiji cha Mtende waliofika kutoa maoni yao katika viwanja vya Skuli ya Mtende.
Mwananchi wa Kijiji cha Mzuri Makunduchi Duli Ali Duli, akichangia maoni yake kwa Tume iliofika kukusanya maoni ya Wananchi kuhusu Mabadiliko ya Katiba ya Tanzania, amesema kuwe na Serikali mbili ya Zanzibar na Tanganyika, na kuondoa kasoro zilioko katika Muungano huu.
Mwananchi wa Kijiji cha Mtende Makunduchi Aziza Mcha, akikabidhi barua yake yenye maoni yake kwa Mwenyekiti wa Mkutano wa kutowa maoni ya mabadiliko ya Katiba ya Tanzania Mohammed Yussuf Mshamba, wakati tume hiyo ilipofika katika Wilaya ya Kusini Unguja kukusanya maoni ya Wananchi kuhusu Katiba, mkutano huo umefanyika katika viwanja vya Skuli ya Mtende.

Kazi ya kukusanya maoni ya wananchi kuhusu Katiba Mpya inayofanywa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba kupitia mikutano iliyoanza siku ya Jumatatu, Julai 2, 2012, katika mikoa minane imeanza vizuri.

Mikutano hiyo inayofanyika mara mbili kwa siku, inafanyika katika mikoa ya Dodoma, Kagera, Kusini Pemba, Kusini Unguja, Manyara, Pwani, Shinyanga na Tanga. Mikutano hii inatarajiwa kumalizika siku ya Jumatatu, Julai 30, 2012.

Taarifa ambazo Makao Makuu Tume imezikusanya kutoka kwa Wajumbe na Waratibu wanaosimamia mikutano hiyo huko mikoani hadi jana (Jumatatu, Julai 2, 2012) jioni zinaonyesha kuwa mikutano yote 14 iliyopangwa kufanyika siku ya kwanza, yaani jana, Jumatatu, Julai 2, 2012 ilifanyika kama ilivyopangwa na wananchi walijitokeza kwa wingi na kutoa maoni yao kwa amani na utulivu.

Katika mikutano hiyo, wananchi waliwasilisha maoni yao kwa kuongea na kwa maandishi kwa Wajumbe wa Tume walioendesha mikutano hiyo.

Pamoja na kuwapongeza wananchi kwa ushiriki wao, Tume inapenda kusisitiza tena kuwa wananchi wajitokeze katika mikutano inayoendelea na kutoa maoni kwa amani, utulivu na katika hali ya kusikilizana.

Kwa upande wa Dodoma, Tume inaendelea kukusanya maoni katika Wilaya ya Bahi; Katika mkoa wa Kagera Tume inaendelea kukusanya maoni katika wilaya ya Biharamulo; katika mkoa wa Manyara Tume inaendelea kukusanya maoni katika wilaya ya Mbulu wakati katika mkoa wa Pwani Tume inaendelea kukusanya maoni katika wilaya ya Mafia.

Mkoani Shinyanga Tume inaendelea kukusanya maoni katika wilaya ya Kahama; mkoa wa Tanga Tume inaendelea kukusanya maoni katika Wilaya ya Lushoto wakati kwa upande wa Zanzibar, Tume inaendelea kukusanya maoni katika mkoa wa Kusini Unguja katika wilaya ya Kusini.

Pamoja na kuwasilisha maoni kupitia mikutano inayoitishwa na Tume, wananchi pia wanaweza kuwasilisha maoni yao kwa Tume kupitia tovuti ya Tume (www.katiba.go.tz) au barua pepe maoni@katiba.go.tz au kwa njia ya posta kupitia anuani zifuatazo:

i. Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Makao Makuu, Mtaa wa Ohio, S.L.P 1681, DAR ES SALAAM, Simu: +255 22 2133425, Nukushi: +255 22 2133442; Au ii. Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Ofisi Ndogo, Jengo la Ofisi ya Mfuko wa Barabara, Mtaa wa Kikwajuni Gofu, S.L.P. 2775, Zanzibar, Simu: +255 224 2230768, Nukushi: +255 224 2230769

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 1 mpaka sasa

  1. AnonymousJuly 03, 2012

    michuzi

    asante kwa taarifa hii

    wape big up hii tume kwa jinsi walivyoanza kazi, sijawahi kuona watu waliojipanga kama hawa kwa jinsi walivyoanza yao ... website nzuri yenye taarifa zote muhimu, hiki ndio watanzania tunategema kutoka idara mbali mbali za serikali lakini hatukipati

    wameweka uwezekano wa kukusanya maoni kwa watu na njia mbali mbali

    tunategema watatoa kazi nzuri

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...