KINONDONI, DODOMA ZAINGIA ROBO FAINALI COPA
Timu za Kinondoni na Dodoma zimeingia robo fainali ya michuano ya Copa Coca Cola 2012 baada ya kushinda mechi zao za 16 bora zilizochezwa leo jijini Dar es Salaam.

Kinondoni imeitoa Rukwa baada ya kuichapa mabao 3-1 katika mchezo uliofanyika Uwanja wa Karume. Mabao ya washindi yalifungwa na Yahya Mohamed dakika ya 13, Issa Allydakika ya 44 na Mabrouk Liyayala dakika ya 80. Ladislaus Fwamba aliifungia Rukwa dakika ya 46.

Kwa ushindi huo, Kinondoni itacheza robo fainali ya tatu Julai 10 mwaka huu Uwanja wa Karume dhidi ya mshindi wa mechi ya 16 bora kati ya Kilimanjaro na Mwanza itakayochezwa leo saa 10 jioni.

Nayo Dodoma imenyakua tiketi ya kucheza robo fainali baada ya leo kuifunga Arusha bao 1-0 katika mechi iliyochezwa Uwanja wa Tanganyika Packers. Bao la washindi lilifungwa dakika tano kabla ya filimbi ya mwisho na Ayoub Khalfan.

Katika robo fainali, Dodoma itacheza na mshindi wa mechi ya 16 bora kati ya Tabora na Tanga itakayochezwa leo jioni Uwanja wa Tanganyika Packers.

Robo fainali zote zitachezwa Uwanja wa Karume ambapo ya kwanza itafanyika keshokutwa asubuhi (Julai 10 mwaka huu) kati ya Temeke na Mjini Magharibi wakati jioni itakuwa Mara na Morogoro.

RAMBIRAMBI MSIBA WA SHABANI SEMLANGWA
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha mjumbe wake wa Kamati ya Nidhamu na Usuluhishi, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Shabani Semlangwa kilichotokea Julai 5 mwaka huu kutokana na maradhi.

ACP Semlangwa ambaye alizikwa juzi (Julai 6 mwaka huu) katika Kijiji cha Gumba, Wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani alitoa mchango mkubwa akiwa mjumbe wa Kamati hiyo inayoongozwa na Kamishna wa Polisi (CP) mstaafu Alfred Tibaigana.

Msiba huo ni pigo kwa familia ya ACP Semlangwa, TFF na familia ya mpira wa miguu kwa ujumla nchini kutokana na mchango na mawazo aliyotoa kwa shirikisho akiwa mjumbe wa kamati hiyo.

TFF inatoa pole kwa familia ya marehemu ACP Semlangwa, jamaa na marafiki na kuwataka kuwa na uvumilivu katika kipindi hiki cha msiba huo mzito. Pia TFF itatoa ubani wa sh. 200,000 kwa familia ya marehemu kama rambirambi zake.

Mungu aiweke roho ya marehemu ACP Shabani Semlangwa mahali pema peponi. Amina

Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...