Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete atakuwa miongoni mwa wakuu wa nchi 16 na wageni wengine wengi maarufu, akiwamo Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Mheshimiwa Hillary Clinton, kushiriki mazishi ya aliyekuwa Rais wa Ghana, Mheshimiwa John Evans Atta Mills kesho , Ijumaa, Agosti 10, 2012, mjini Accra.

Rais Kikwete na ujumbe wake anatarajiwa kuwasili mjini Accra, mji mkuu wa Ghana, adhuhuri ya leo, Alhamisi, Agosti 9, 2012, kuhudhuria mazishi ya kiongozi huyo aliyefariki dunia mchana wa Jumanne, Julai 24, 2012 kwa ugonjwa wa kansa ya koo kwenye Hospitali ya kijeshi inayoitwa 37 Military Hospital mjini Accra.

Rais Mills ambaye amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 69 anatarajiwa kuzikwa kwenye makaburi yaliyoko eneo la bustani la Geese kwenye Mtaa wa Castle Drive karibu na Hekalu ya Osu mjini Accra baada ya kuwa mwili wake umeagwa kwenye shughuli maalum itakayofanyika kwenye bustani ya Independence Square kesho Ijumaa.

Rais Mills ambaye nafasi yake imechukuliwa na Rais John Dramani Makama atazikwa katika kaburi lililojengwa na kampuni ya ujenzi ya Serikali ya China ya HL Construction. Mwili utazikwa baada ya kupitishwa katika mitaa maarufu ya jiji la Accra ili kutoa nafasi ya mwisho kwa wananchi wa Ghana kuuona na kuuaga mwili huo kwa mara ya mwisho.

Jana, Jumatano, Agosti 8, 2012, mwili wa Mheshimiwa Mills ulihamishwa kutoka kwenye Hospitali ya 37 ya Jeshi la Ghana ambako umekuwa umehifadhiwa tokea kufariki dunia na kupelekwa kwenye nyumba ya familia iliyoko katika Barabara ya Spintex kwa ajili ya kufanyiwa taratibu za mila.

Baada ya shughuli hiyo, mwili wa Mheshimiwa Mills ulihamishiwa kwenye jumba la kulia la Ikulu ya Ghana ambako wananchi wamekuwa wanatoa salamu zao za mwisho kwa mwili wa kiongozi wao. Mwili wa Rais Mills utabakia katika sehemu hiyo mpaka utakapohamishiwa Independence Square kwa ajili ya shughuli ya mazishi.

Miongoni mwa watu waliotoa heshima zao za mwisho kwa mwili wa Rais leo ni pamoja na Rais John Kuffor ambaye Rais Mills alichukua madaraka kutoka kwake. Vikundi vya muziki na vikundi vya utamaduni viliendelea kutumbukiza Ikulu siku nzima jana na usiku kucha.

Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
9 Agosti, 2012

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 6 mpaka sasa

  1. Wazungu wanaita too much information - habari ya clinton, mchina gani kajenga kaburi, nk itatolewaje na Ikulu ya Tanzania?

    Haya tunasubiri picha za wakimuaga na kumpokea.

    ReplyDelete
  2. Hili ni Janga ala kitaifa, IKULU inatumia yahoo address kwa mawasiliano? kweli, mtaalamu wa IT Ikulu hakuna vision yoyote ya kusaidia kuuondoa msiba wa taifa? kutengeneza email ya domain ya ikulu kwa mtu anayejua IT ni kitu kisichozidi hata masaa mawili? lakini mtu mwisho wa siku anapokea mshahara na hata uchungu na vitu kama hivi hana

    ReplyDelete
  3. WaTanzania kazi kulalamika. Hamwezi soma habari kimya kimya? Duh!

    ReplyDelete
  4. Wachina nimewavulia kofia - yaani wameanza kupewa na tenda za kujenga makaburi ya vigogo wa Afrika!! Afrika imebakiziwa nini inachoweza kufanya kinachoendeleza utamaduni wake - of all places, Ghana? Shame on Mother Africa.

    ReplyDelete
  5. Niliiisha ona video ya mazishi ya watu wa Ghana ni kama sherehe na wala siyo maombolezo tena. Halafu wanapenda umaarufu sana. Unawezekana maisha yako kabla ya kufa ulikuwa unalalia kitanda cha kamba lakini siku ukifa utalazwa kwenye kitanda cha dhahabu. Shamra shamra na shangwe nyingi! Na wengine humo humo wanatafutia wachumba yaani utadhani harusi nilishangaa sana. Utamaduni wao umekuw akama wa watanzania na kufanya maharusi makubwa makubwwa kuliko uwezo wa wenye kuoa.

    ReplyDelete
  6. Ikulu inashangaza sana kutumia barua pepe ya 'Yahoo! Kwa nini wasingetumia moja tu hiyo ya 'press'?

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...