Panya hawakamatani, na pia hawatajani,
Ati nani kala nini, kala wapi na kwanini,
Panya daima makini, watajane kiwe nini,
Wanapokula ghalani, panya hula na yamini!
Panya si wakutamani, ni mnyama makini,
Apuliza mdomoni, hana haya jamani,
Huharibu suruali na gauni, panya haogopi kabatini,
Wanapokula ghalani, panya hula na yamini!
Wanagombana na paka, panya wana mbongo,
kwa uroho pasi mipaka, shimo waishilo bongo,
ufisadi wamejipaka, ni rangi zao za ubongo,
Wanapokula ghalani, panya hula na yamini!
Yao ni moja dhamiri, kushiba kwa kila kadiri,
Shibe yao ni stahili, yao pekee kwa kila staili,
Wanakula bila kikomo,hatakama ukiwabaini,
Wanapokula ghalani, panya hula na yamini!
Hao siyo panya buku, mbona wacheza kiduku,
walionapo sanduku, limesheheni tu buku,
wanang'ata zo buku, kutoa chote huku,
Wanapokula ghalani, panya hula na yamini!
Panya hawa ni stadi, hasa kwenye ufisadi,
Watuachia samadi, baada ya kula kwa ustadi,
Si deni zao ahadi, ni njia tu ya kufisadi,
Wanapokula ghalani, panya hula na yamini!
Panya huyu ni hatari, hasa kwenye mifuko,
Ya mafao ya jamii, amehamia huko jamani,
Kasababisha tafrani, sekta binafsi huko walakini,
Wanapokula ghalani, panya hula na yamini!
Mapanya haya yana laana, hayafanyi ya maana,
Hayaachi kufaana, japo kidogo tu maana,
2015 tuyatose kuona, wengine hatuna maana,
Wanapokula ghalani, panya hula na yamini!


Hii inanikumbusha yule jamaa anayekata tawi huku amelikalia hajui kama atadondoka na yeye atadhurika. Ndio viongozi wetu hao wanakula tu, hawajui na wao wanajitia mashakani kwani umasikini ukizidi sijui wataishi wapi.
ReplyDeleteUnakata tawi huku umelikalia hujui ukila sana unawatia watu umasikini, sasa umasikini ukizidi si tutahatarisha amani jamani. Au mtakimbilia Uswiss
ReplyDeletehawa viongozi ni wazee wenu ambao kwa miaka wamekalia madarakani na kwenye mashirika ya umaa ya taifa na ya kitaifa wakipeana upendeleo katika ajira, elimu, upendeleo kila mahala. Kila wizara, mashirika ya kimataifa ya kitaifana wako wao kwa wao. Leo hawaoni aibu kukaa katika majukwaa na kusema nchi inaliwa. Ndio Nyerere aliowapa madaraka, mika yote hiyo na watoto wao ndio waliopo katika mabenki ikiwa vilevile benki kuu. Walizowea kula na wakawasomesha watoto wao, wamejaa vyuo vikuu vyote, wanaongoza huko vyuoni, ingawa baadhi yao walisoma kwa cheti kimoja ukooo mzima. Leo wanaendeleza mtindo ule ule wa kula na kujenga mahekalu mbezi beach, segerea, kawe beach, kurasini. Ulizia nani wamejenga huko. Yale ya Kariakoo yanaonekana, lakini mahekalu yamejificha huko pempezoni mwa Dar es Salaam. Wengine hata wakipata misiba huwa hawafanyii nyumbani kwao kuogopa wasijulikani mali walizokuwa nazo. Tuseme nini akina kawambwa, Ardhi yote imeporwa. Sisi na Wahindi wa Wamarekani hawako tafauti.
ReplyDeleteBismillahi nianze, mshukuru RAHMANI,
ReplyDeleteNusuru nisiteleze, ichunge yangu 'lisani'
Machache niyaongeze, khusu huwa 'hayawani'
Mitego uisambaze, hawanasi abadani!
Huwaoni wakanasa, ndipo zidi 'aksheni'
Kwa paka ndio kabisa, humpita mapajani,
Huzidi yao mikasa, wakitinga sandukuni,
Mitego uisambaze, hawanasi abadani!
Khasa palipo nafaka, tele hawakosekani,
Maskani wataweka, wabanane vilindoni,
Magunia hutoboka, wakamaliza vya ndani,
Mitego uisambaze, hawanasi abadani!
Hukuchezea foliti, darini na mivunguni,
Kisahau lako shati, seuze nguo ya ndani,
Hawapotezi wakati, weshararuwa zamani!
Mitego uisambaze, hawanasi abadani!
Ulikomee kabati, na mitego milangoni,
Tairuka samasoti, tele wajazane ndani,
Wayavamie makoti, na 'diraa' la mwandani,
Mitego uisambaze, hawanasi abadani!
Tafuna na kupuliza, khisi uchungu huoni,
Kumbe wanakuumiza, na jeraha haliponi,
Na gonjwa lao sambaza, limaarufu JIJINI,
Mitego uisambaze, hawanasi abadani!
Kubwa lao panya buku, linatisha kama nini,
Liwinde kule na huku, jepesi ngia shimoni,
Hukuvizia usiku, kwenye shuka limo ndani,
Mitego uisambaze, hawanasi abadani!
Panya wasio na woga, hasa buku namba wani,
Wanokomba hadi mboga, wasoogopa jikoni,
Sumu siku kiimwaga, ndo hufunga Ramadhani,
Mitego uisambaze, hawanasi abadani!
Mote wataka faidi, vya ndani na jalalani,
Kila kitu wafisidi, ubakie idharani,
Wana za peke kusudi, YARABI amewalani,
Mitego uisambaze, hawanasi abadani!
Kiamboni wamechosha, mejaa kwa madazani,
Wajuzi tufahamisha, ipi yao 'solusheni',
Haraka kuwakomesha, ipatikane amani,
Mitego uisambaze, hawanasi abadani!
Hili shairi si moja kati ya mashairi yaliyokamilika, umemtumia panya kwa wasifu wake kuelezea ufisadi. Ndio idea imekaa njema lakini hujaweza kuoanisha ipasavyo ilete mantiki ya kishairi. Creativity and more brainstorming is needed. By the way good idea.
ReplyDeletekikweli ya umiza sana kuyaona mapanya hayaaa yakiendelea mwaka 2015, yetu sisi wananchi kuyatokomeza daima, mshairi umenena yaniingia moyoni, mungu akubariki kuwasilisha ujumbe kwa jamii wala usikome , endeleza mpambano kuelimisha jamiiiii, tufunguke mwaka 2015
ReplyDeleteTanzania Motomoto. Nina omba kuliza panya hata kama ana ishi kwenye nyumba ya fahari hana raha. Utamkuta amejaa na wasiwasi kazi yake kubwa ni kunusa nusa adui kila pahali.
ReplyDeleteMnh...mshairi umetunga kweli kweli...
ReplyDelete