Salaam Aleikum,

wanablog ya jamii. Natumai wote mu wazima wa Kheri kutokana na hifadhi ya mtume Mohamed, Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam. Ama baada ya salaam, ndg. Zanguni, waislaam na wakristo wapenda amani, napenda kuungana nanyi katika mjadala mfupi kuhusiana na swala la lugha katika nchi yetu ya Tanzania (Tanganyika na Zanzibar)

Kupitia hii blogu yetu ya jamii, kumekuwepo na manun'guniko kadhaa kuhusiana na lugha stahiki ya taifa. Wengine wanapendekeza tutumie Kiswahili, wengine wanasema tutumie lugha ya Kiingereza kwani ndio lugha ya kimataifa. Kijana wetu mahiri Mashaka John amekuwa akiandika makala mazuri sana kuielemisha jamii kutumia lugha ya kigeni (kiingereza). 

Nikiwa mmoja wa washabiki wakubwa wa bw. Mashaka, nimekuwa nikivutiwa na uchambuzi wake wa kina kuhusiana na maswala ya kiuchumi na kijamii. Zaidi ni ufundi na ustadi wake wa lugha hii ya kigeni

Majuzi, kuna video moja Ankal alituwekea kuhusiana na Uchumi wa Marekani ambako bwana Mashaka kupitia BBC, aliongea kwa lugha ya Kiswahili. Niseme Mashaka aliongea kwa ufasaha mkubwa ingawa alikuwa na lafudhi ambayo moja kwa moja siyo ya kitanzania. 

Ni lafudhi iliyosiki au kuegemea lugha ya kiingereza zaidi. Bahati mbaya wasomaji wa blogu yetu walimshambulia sana wakikosoa lafudhi na siyo muktadha,na ufasaha wake katika kujadili mada husika kutumia lugha ya kiswahili.

Aibu kubwa ni vijana wetu wanaosoma English medium ambao mara nyingi hawaeleweki lugha wanayotuitumia kama ni kiingereza au Kiswahili hasa Kizazi cha bongo fleva kinachotia aibu hasa kuwaangalia kwenye luninga. Wanajieleza kwa lugha tofauti kwa wakati mmoja, na kila lugha wanaboronga. 

Kiswahili chao hakieleweki, viingereza vyao na lafudhi ya kulazimisha ndio kabisa na hii inachanganya sana. Najiuliza ni utandawazi, au elimu duni, kwa maana hata hapa Zanzibar hili tatizo linakuwa kwa kasi sana.

Tanzania kuna makabila mengi, na kila kabila ina lafudhi yake mahususi. Hususan ndugu zetu wamasai wana lafudhi yao, Wahaya, Wachaga na wasukuma wana lafudhi zao. Wapo viongozi wa kitaifa ambao wamebezwa na kusimangwa kwa kutokujua lugha ya kiingereza. 

Waziri Fulani hapa majuzi ametukanwa sana kwa kutumia kiingereza kibovu. Sasa nashindwa kuelewa ni lugha ipi inayokubalika katika taifa letu. Mikataba mibovu tunayoingia ni kutokana na wengi wetu kutokuelewa lugha ya kigeni vizuri.

Kwa watu wasiopendelea upande wowote na walio tayari kusikia hoja,nawaombeni waungwana mlijadili hii hoja kwa weledi.Hizi lugha mbili ni muhimu katika kuetekeleza majukumu yetu ya maendeleo ya taifa. Je ni hipi iliyomuhimu kuliko enzake?
Hamza Al-Mhari Nasseeb
Ngome Kuu, Zanzibar

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 17 mpaka sasa

  1. Msidanganywe na huyo mashaka. He is another American project to counter China. Atuelezee kasoma wapi kwa hela ya nani? Ikiwa ni mtanzania kwa nini awe na lafudhi ya kigeni?

    ReplyDelete
  2. Mashaka john kasomea two islands of Zimbabwe and unguja

    ReplyDelete
  3. Kwa wanaosafiri katika nchi za watu lazima ujue lugha japo moja, na kiingereza ni wengi wanakijua. Zaidi ya hapo kiswahili kinatosha.

    ReplyDelete
  4. Hivi wengi wetu bado tunamtazamo wa kuongea lugha kwa ufasaha ndo kusoma na ni kuwa na akili sana!Huku ni kujidanganya na ni kasumba ya kiwenda wazimu tu.

    Hivi huwezi kuleta maendeleo katiak eneo lako la utawala bila kuongea lugha kwa ufasaha.Mumepotea sana kama mnaamini kuwa usomi ndo huo.

    Mkipewa nafasi onyesheni vipawa vyenu kwa kuwapa watu maendeleo,si kwa kutafuta udakitari na kupamba lugha.Waweza kuleta maendeleo kwa kuona tu na kuiga bila hata ya kuiga uzuri wa lugha.

    ReplyDelete
  5. Kiswahili lazima kitumike katika blog hii kwa kuwa blog hii ni ya kimatumbi,lakini pia kama kutakua na article ya kingereza aka kimombo kinajipenyeza basi si vibaya kuipachika hewani habari hiyo ya kingereza.
    wadau ffu

    ReplyDelete
  6. bandugu. kuwa maarufu ni kitu kibaya sana. yaani hata ukikooa tabu. sasa mashaka kafanya nini? kuongea na lafudhi nayo ni tabu? mashaka huko juu kama mnara wa voda

    ReplyDelete
  7. tatizo la lugha ni sisi wazazi. tunawaruhusu watoto kuiga upumbavu kwenye TV.... Msikilize Wema sepetu akiongea, Kiswahili alishahau kwa sababu yeye ni maarufu. mtoto kazaliwa hapa kakulia hapa.
    nampongeza mashaka kwa sababu anaishi marekani, kasomea na kukulia marekani lakini bado anaongea kiswahili fasaha. hakuna neno hata moja alilotumia la kiingereza.

    ReplyDelete
  8. As long as Mashaka is Linked to Wall-street, nobody will ever listen to him in this country. If he love Tanzania he need to come and Join Zitto and the rest in M4C au amsaidie Mzee Wassira CCM na hicho kiingereza chake au lafudhi yake

    ReplyDelete
  9. Nadhani swala la lugha linaitaji mjadala mzito ndani na nje ya bunge.

    ReplyDelete
  10. yohanna mashaka ni mwarubaini ya Zitto Kabwe

    ReplyDelete
  11. mdau kauliza tutumie lugha gani zaidi, ninyi hapo juu mnajibu vitu tofauti, huo ndio usomi gani wakutoelewa hata swali?? swali lake kalitoa mwishoni kabisa "NI HIPI ILIYOMUHIMU KULIKO ENZAKE?" sasa kama utungo wa msitari huu upo sawa au la mimi si mtaalam, lakini nimeelewa swali, hivyo mchango wangu ni huu,
    kwa shughuli zetu za kimaendeleo tutumie lugha inayoeleweka vizuri kwa wahusika wote kwa wakati huo kwa ajili ya mafanikio ya jambo linalohusika kwa wakati huo bila kujali matamshi, mimi naamini ufasaha wa lugha kwenye mawasiliano ni ujumbe kumfikia SAWIA unampelekea bila kujali umetamka vipi, bali katika mafunzo ya lugha umuhimu wa matamshi fasaha ni mkubwa.

    ReplyDelete
  12. Binafsi naona cha muhimu ni uelewa sahihi wenye kuleta maendeleo kwa mtu, jamii na taifa. bila kujali lugha utakayotumia. WACHINA wamejiendeleza kwa lugha yao, huo ni mfano tosha sana.

    ReplyDelete
  13. Ni ukweli usiopingika kuwa ukijua lugha zaidi ya moja zote kwa ufasaha una faida zaidi ya yule asiyejua. Lakini pia ni muhimu kujua wakati na mahali sahihi pa kutumia lugha husika. na kama utaamua nkutumia lugha moja si vema/busara kuchnganya. Kama ni kiswahili, basi tumia kiswahili mpaka mwisho na kama ni kiiengereza basi hakikisha unakijua ipasavyo kuweza kuongea bila kuchanganya. Mwalimu wangu wa kiiengereza nikiwa sekondari alitueleza kuwa kuchanganya lugha wakati wa kuongea ni USHAMBA

    ReplyDelete
  14. Kwanza kwa kukujibu swali lako bwana mtoa mada, Tunatakiwa tutumie kiswahili kwa sababu sisi siyo waingereza na wala hatuishi uingereza.

    Bahati mbaya tuliyoipata hapa kwetu ni kwamba; watu wajinga wanadhania kuzungumza kiingereza ni kipimo cha weledi.

    Kuhusu John Mashaka na usaili wake kwenye BBC TV; Bashaka alizungumza kiswahili kwa lafudhi isiyokuwa ya kiswahili wala kizungu. Hii ni ishara kwamba mashaka anayo lugha yake ya kwanza ambayo siyo kiswahili na wala siyo kiingereza.

    ReplyDelete
  15. Maoni yangu naona ni vizuri kutumia Kiswahili kwa sababu tumekubaliana hiyo ndiyo lugha ya Taifa. Mtu anaruhusiwa kujifunza lugha yoyote na nahimiza tujifunze lugha zaidi ya moja kwani ni faida kwa taifa, kwani tunapata wageni toka pembe zote za ulimwengu (utalii n.k) au nasie tunakwenda huko. Lakini naona si uzalendo pale Viongozi mbali mbali wanapotoa hotuba yote kwa Kingereza ili kuonyesha wamesoma. Mataifa makubwa kama China, Japan, Wafaransa, marekani, n.k viongozi wao wamesoma tena wengine Magharibi lakini ukiwaona wanafanya mahojiano kwenye TV. wanatumia lugha yao na Mkalimani kwa pembeni, ingawa wanajua kiingereza, bali wanaonyesha uzalendo wao.
    Na jamaa akina Mashaka na wengine wengi na lafudhi zao ndiyo tunaita kasumba. Kwani mie niko Ughaibuni kwa miaka karibu 30 na nimesoma vile vile, na kila mwaka lazima nirudi bongo na kama unifahamu huwezi hukajua nimetoka sehmu nyingine. Vile vile naongea na wabongo katika chama chetu sioni wakiwa na lafudhi tofouti kama za Mashaka, na kuna wazee wamekaa miaka 40 au 50 bila kuja Bongo. kwa hiyo naona ni tabia ya mtu pekee.

    ReplyDelete
  16. kakakuona_sijaonaNovember 15, 2012

    Ndugu zangu wa TZ,nafikiri lafudhi ya mtu kwa kawaida inatokana na sehemu au mazingira aliyokulia mtu,nitajaribu kutoa mfano mfupi na wa kueleweka.
    Chukua mfano wa wazazi walio Dar ambao wametoka nje ya Dar ila watoto wao wamezaliwa na kukulia na kusomea Dar,hawa watoto moja kwa moja wakiongea kiswahili lafudhi yao itakuwa ni ya ki-Dar tofauti kabisa na wazazi wao.Hivyo hivyo kwa mtoto atakayekulia Bukoba,Tanga,Mwanza,Arusha n.k. ambaye wazazi wake hawatokei sehemu hizo,na hiyo inaenda mpaka ukivuka mipaka ya nchi kwa watoto wanaoongea kiswahili lakini wamekulia nchi zisizoongea kiswahili basi nao lafudhi zao hazitakuwa za kiswahili cha bongo au za wazazi wao ambao wamekulia Tz.Kwa hiyo basi kama Mashaka hakukulia Tz basi si kitu cha kushangaza kama lafudhi yake si ya kiTZ,ila kama kakulia Tz basi hapo itapaswa kujiuliza ni vipi?na pia inatupasa kuwasifia wale ambao hawajakulia Tz lakini bado wana uwezo wa kuongea kiswahili safi hata kama lafudhi si ya kibongo.Ndiyo maana unakuta mchaga,mnyakyusa au mndengereko anaweza kuongea kiswahili fasaha/si fasaha kikiwa na lafudhi ya alikokulia.
    Nafikiri nimefafanua na kueleweka vizuri.

    ReplyDelete
  17. Mi naona lugha sahihi ya kutumia hapa bloguni ni kiswahili kwani wengi wanaokuja kusoma hapa ni waswahili na hata wale wanaojuwa kiingereza ni wachache sana wanaweza kujieleza kwa kutumia hiyo lugha ya kigeni. Wasanii wa bongo fleva si watu wa kuwaiga, tuseme ni kazazi kilichopotea na hawajuwi nini wanachokifanya zaidi ya kuiga tamaduni za kijinga toka nje. Hapa ni kiswahili tu ndicho kinachofaa maana walengwa wote ni waswahili hao wanaosema hawajuwi kiswahili wanadanganya tu.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...