Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema kuwa jamii inahitaji kuelimishwa zaidi juu ya umuhimu wa uzazi wa mpango kwa maendeleo ya nchi sambamba na kutunza afya ya jamii hasa kwa akina mama na watoto.
Kauli hiyo imetolewa na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad katika hafla ya uzinduzi wa Ripoti ya Idadi ya Watu Duniani ya mwaka 2012 iliyofanyika katika viwanja vya skuli ya Mkwajuni Mkoa wa Kaskazini Unguja, ambako alimuwakilisha Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohd Shein.
Amesema jamii bado haijatoa umuhimu unaostahiki katika matumizi ya njia za uzazi wa mpango, hali inayopelekea kuwepo kwa ongezeko kubwa la watu ambalo huathiri harakati za maendeleo na afya ya jamii.
“Taarifa zinaonesha kwamba Zanzibar hivi sasa inakadiriwa kuwa na idadi ya watu 1.3 milioni, wanaoongezeka kwa kasi ya asilimia 3.1 kwa mwaka ambapo idadi ya watu katika kila kilomita moja ya mraba imefikia watu 496 mwaka 2011”, ilieleza sehemu ya hotuba hiyo ya Dkt. Shein iliyosomwa na Makamu wa Kwanza wa Rais.
Amefahamisha kuwa bado vifo vya mama wajawazito viko juu duniani lakini vimepungua kwa upande wa Tanzania na Zanzibar hasa kwa kina mama wenye umri mdogo na wanaokabiliwa na tatizo la umaskini.
“Kwa Tanzania katika mwaka 2004/05 idadi ya vifo ilikuwa 578 kwa kila akina mama waja wazito 100,000 na kupungua kidogo hadi kufikia vifo 454 mwaka 2010. Hata hivyo kwa Zanzibar vifo vya akina mama vimepungua kutoka vifo 473 mwaka 2006 hadi vifo 281 mwaka 2011, kwa kila kina mama 100,000 kwa takwimu za hospitali”, alifafanua.
Amesema mafanikio hayo yametokana na juhudi za serikali katika kuimarisha huduma za afya kwa jamii ikiwa ni pamoja na kutoa chanjo za pepopunda na shurua, sambamba na kuimarisha huduma za afya ya uzazi katika hospitali mbali mbali.
Ametoa wito maalum kwa Wazazi kuwaozesha watoto zao kuanzia umri wa miaka 20 na kuendelea ili wamalize masomo yao kwani elimu ni ufunguo wa Maisha.
Kwa upande wao wawakilishi wa Umoja wa Mataifa wameipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuona umuhimu wa huduma ya uzazi na kuamua kutoa huduma hiyo bila ya malipo.
Mwakilishi Mkaazi wa Shirika la Idadi ya watu (UNFPA) Tanzania bibi Mariam Khan amesema bado suala la uzazi wa mpango linakabiliwa na changamoto nyingi ikiwa ni pamoja na wanajamii kuona ugumu juu ya matumizi ya njia za uzazi wa mpango
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akiwasili katika hafla ya uzinduzi wa Ripoti ya Idadi ya Watu Duniani ya mwaka 2012 iliyofanyika katika viwanja vya skuli ya Mkwajuni Mkoa wa Kaskazini Unguja,
Meza kuu
Waziri wa Afya Juma Duni Haji akiungana na kikundi cha Sanaa Zanzibar kutoa burudani ya ngoma ya Msewe wakati wa uzinduzi wa Ripoti ya Idadi ya Watu Duniani kwa mwaka 2012, huko Mkwajuni Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akizindua Ripoti ya Idadi ya Watu Duniani kwa mwaka 2012, huko Mkwajuni Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akionnyesha Ripoti ya Idadi ya Watu Duniani kwa mwaka 2012, baada ya kuizindua rasmi huko Mkwajuni Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...