*Asema kama niliweza TFF siwezi kushindwa TOC
*Aahidi ushirikiano wa karibu na Serikali, wadau wa michezo
*Ashangaa kukosekana kwa medali za Olimpiki tangu 1980
*Aahidi uwazi kwenye mapato na matumizi ya TOC

Na Mwandishi Wetu
SIKU chache baada ya kupitishwa kugombea nafasi ya Katibu Mkuu wa Kamati ya Olimpiki ya Tanzania (TOC), Katibu Mkuu wa zamani wa Shirikisho la Soka nchini (TFF) Frederick Mwakalebela  amezindua kampeni zake kwa kishindo na kuahidi kurejesha heshima ya nchi kwenye michezo kimataifa.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Mwakalebela alisema ni aibu kwa nchi yenye idadi ya watu zaidi ya milioni 40 na vipaji kibao kama Tanzania kukosa medali kwenye michezo mikubwa kama ya Olimpiki kwa zaidi ya miaka 30 sasa.
“Olimpiki ni mashindano makubwa yanayojumuisha michezo mbalimbali, lakini tangu mwaka 1980, pamoja na kupeleka wanamichezo kwenye mashindano hayo, hatujawahi kupata medali hata moja,” alisema.
 Akiwa makini kutopeleka lawama kwa uongozi wa TOC uliopita, Mwakalenela alisema kilichosababisha kupatikana kwa medali mwaka 1980 huko Moscow, Urusi (USSR) ni mfumo mzuri wa maandalizi ya timu ambapo timu hiyo ilifanya maandalizi ya mwaka mzima kwa kufanya ziara mikoani na nje ya nchi.
“Kwanini siku hizi inashindikana kufanya hivyo? Ni ukosefu wa ubunifu, na ndio maana ninagombea ili kuleta mawazo mapya michezoni. Nikiingia ofisini kazi yangu ya kwanza itakuwa ni kuiweka TOC karibu na wadau wakubwa wa michezo ambao ni Serikali, vyombo vya habari, makampuni ya biashara, majeshi, shule, vyuo na taasisi mbalimbli binafsi.
“Ndani ya miezi mitatu tu wadau hao watakuwa ‘marafiki’ wa TOC na maandalizi ya michezo ya Olimpiki ya mwaka 2016 huko Rio de Janeiro, Brazil yataanza mara moja. Tukikosa medali mwaka huo, basi ni lazima tutapata mwaka 2020,” alisema kwa kujiamini.
Akijibu maswali mbalimbali ya waandishi, Mwakalebela aliyefanya kazi kwa ufanisi mkubwa akiwa TFF, alisema TOC mpya itakaa na Rais Jakaya Kikwete na kumwomba kabla hajamaliza muda wake wa uongozi serikalini awaachie wanamichezo wa Tanzania kumbukumbu ya Kijiji cha Olimpiki.
Alisema kuwapo kwa kijiji hicho kutawapa nafasi vijana wenye vipaji nchini kuonyesha uwezo wao na kutokana na wao, ndipo timu bora ya taifa itakayokuwa ikiiwakilisha nchi kwenye michezo mbalimbali itakuwa ikipatikana.
“Tutashirikiana na wizara husika, balozi za kimataifa, Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NGOs) yanayotoa nafasi za mafunzo (scholarship awards) na organaizesheni za michezo za kimataifa kuwatafutia wanamichezo wetu nafasi za masomo na mafunzo nje ya nchi.
“Hili liwahi kufanyika na watu kama kina Filbert Bayi, Suleiman Nyambui na Mwinga Mwanjala walifaidika sana na mpango huu na kisha kuliletea taifa letu sifa kubwa michezoni,” alisema Mwakalebela ambaye kwenye kinyang’anyiro hicho atapambana na Bayi anayetetea nafasi ya Katibu Mkuu wa TOC.
Kikubwa zaidi, Mwakalebela alisema mapato na matumizi ya TOC yatawekwa wazi ili kile kidogo kinachopatikana, kikijumlishwa na kingine kutoka serikalini na kwa wadau, kifanye kazi iliyokusudiwa ya kuendeleza michezo nchini.
TOC ndio msimamizi na mlezi wa vyama na mashirikisho ya michezo nchini na ndio waandalizi wa timu za taifa zinazoshiriki michezo ya Olimpiki, Jumuiya ya Madola na Michezo ya Afrika (All African Games).

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 3 mpaka sasa

  1. Haya bwana. Nimewahi kuskia bwana huyu akiwa huko TFF na ilitokea nini cjui hayuko huko tena.
    Ok labda tumpe nafasi huku TOC kwa kauli zake hizi nzuri zinazoyapendeza masikio yetu.... Hata mkosaji aweza pewa nafasi ya pili. Nashauri haya aliyoyasema hapa yachapwe na kuwekwa kwenye mbao za matangazo huko afisi za Olimpki na iwe dira na angalizo nyakati za utendaji wake. Na siye Wadau bila kupepesa mimacho tuje tumwuulize Pale atakapo kiuka aliyoyaimba leo. Else Tumpongeze endapo atatufikisha kunako nozi zake na zilizo za wengi pia.Isijekuwa mvinyo mupya chupa ileiile! God Bless Us All

    ReplyDelete
  2. Huyu nadhani anaweza nimeuona uso wake unaeleza kuhusu moyo wake, mpeni atafanya kweli.

    ReplyDelete
  3. kule TFF hakukosea chochote ila aliacha mwenyewe ili kwenda kugombea ubunge huko Iringa ambako alikumbwa na kashfa ya rushwa!!! anafaa tumpe nafasi atuletee mageuzi TOC

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...