Leo tarehe 29 Machi 2013, mnamo saa mbili na nusu asubuhi jengo linalojengwa kwenye kiwanja namba 2032/73 Mtaa wa Indira Gandhi lilianguka kutokana na sababu ambazo bado hazijathibitishwa kitaalam na mamlaka husika. Shirika la Nyumba la Taifa linasikitika sana kutokana na kuanguka kwa jengo hilo pamoja na maafa yaliyotokana na tukio hilo la kusikitisha. Pia Shirika linatoa pole kwa wale wote waliofikwa na msiba uliotokana na ajali hii.

Mradi huu wa ubia kati ya NHC na M/s Ladha Construction Limited ya Jijini Dar Es Salaam ulianza kutekelezwa tarehe 4 Februari 2008 ambapo Shirika la Nyumba litakuwa na hisa asilimia 25 na mbia ana asilimia 75 mara baada ya mradi kukamilika. Kwa mujibu wa sera ya ubia iliyoanza kutumika mwaka 1993 na kuhuishwa mwaka 1995 na 2005, Shirika la Nyumba la Taifa lilikuwa likitoa ardhi ambayo ilikuwa ikihesabika kama asilimia 25 ya mtaji wake kwenye jengo husika na mbia alikuwa akipata asilimia 75.

Kwa mujibu wa mkataba huo mbia mwendelezaji M/s Ladha Contruction Limited kama walivyo wabia wengine, anapaswa kabla ya kuanza ujenzi kupata vibali kutoka kwenye mamlaka husika na kuwa na wataalam wa ujenzi na washauri waliokubalika na kuthibitishwa na mamlaka husika. Aidha, mbia huyu akishapata wataalam hao ndiye anayehusika kuingia nao mikataba ya kazi ya kujenga na kusimamia ubora wa jengo husika kwa mujibu wa sheria. Katika mradi huu mbia mwendelezaji aliajiri wataalamu wote waliosajiliwa na Mamlaka husika ambazo ni CRB, ERB, AQRB na Mansipaa husika na mamlaka nyinginezo. Kwa kuwa ujenzi ulikuwa bado haujakamilika, Shirika lilikuwa bado halijapata asilimia 25 ya umiliki wake.

Pia tunapenda kuufahamisha Umma kuwa, Shirika la Nyumba la Taifa, lilisimamisha utoaji wa miradi mipya ya ubia mwaka 2010 ili kuweza kutathimini mafanikio na changamoto za utekelezaji wa miradi ya ubia na hivyo kuwezesha kutengeneza sera mpya. Kama sehemu ya zoezi hilo, shirika pia lilifuta jumla ya mikataba 64 ambayo ilikuwa imesainiwa lakini haijaanza ujenzi.

Katika sera mpya ambayo utekelezaji wake utaanza hivi karibuni Shirika litahusika moja kwa moja katika kuteuwa mjenzi mtaalam (contractor), msimamizi mtaalam wa mradi husika (consultant) na kusimamia kikamilifu shughuli zote za ujenzi.

Tunapenda kuufahamisha umma kuwa taarifa zaidi zitatolewa baada ya vyombo husika kuwasiliana na mjenzi wa mradi huu. Aidha, taarifa zinaweza kupatikana moja kwa moja kutoka M/s Ladha Construction Limited ambaye ndiye mbia mwendelezaji aliyekuwa anasimamia ujenzi huu.

IMETOLEWA NA KITENGO CHA MAWASILIANO NA HUDUMA KWA JAMII
 
S.L.P. 2977 Simu: 2851590 DAR ES SALAAM
Telegrams : "NYUMBA" TANZANIA
Fax 2851442

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 11 mpaka sasa

  1. Pole haitoshi na hapo ndipo nawashangaa washusika, tunahitaji tufahamishwe ninamna gani waliofikwa na janga hilo wanavyofidiwa

    ReplyDelete
  2. so mnawekeza asilimia 25 ,bila kujua ubora? ungekuwa ni mradi wa mtu binafsi unaweka hela yako /kiwanja 25% na baadae zaidi ya hapo, usingesimamia ujenzi?

    ReplyDelete
  3. Watanzania tunatabia ya kudanganyana au kupotoshana hata sisi wasomi huwa tunawadanganya au kupotosha ukweli pale tunapojua wanajamii si wajuaji hivyo. NHC kama sehemu za wamiliki wa jengo kama walivyokiri wenyewe wanahusika moja kwa moja na janga hili na wanatakiwa wawajibishwe pia kwa mchango wao kama sehemu ya wamiliki. Kufidia harasa Mimi nalia na NHC. Wao wanavyosema eti sisi ni asilimia 25 tu, basi ni kukiri kuwa mchango Wao katika Maafa haya ni kwa asilimia 25 tu? Bwana Mchechu NHC ni partner in this crime, like it or not, and you have a case to answer
    As well, Joe Bura dar

    ReplyDelete
  4. Wanasheria mpo hapo? Eti "kwa kuwa ujenzi ulikuwa haujakamilika NHC haikuwa imepata hisa zake za asilimia 25" ni upotoshaji kwa waliokimbia umande. Sisi wasomi tumafahamu jukumu lenu NhC kisheria na sio blah blah hizi, Kama polisi na upelelezi wameingia mkenge kwa tamko Kama hili basi sitashangaa maana ujuzi unaweza sumbua. Wapate ushauri dhubuti wa kisheria. Joe bura dar

    ReplyDelete

  5. NHC WATUAMBIE MKATABA ULIKUWA KUJENGA GHOROFA 10 IWEJE WAMUACHIE MWEKEZAJI AJENGE GHOROFA 16? INA MAANA HIZO GHORFA 6 ZA ZIADA WANAGAWANA MCHECHU NA MHNDI

    ReplyDelete
  6. Hakuna jipya kwenye huu waraka.

    ReplyDelete
  7. Tunagundua mmeona mapungufu ya utaratibu wa awali, hivyo kurekebisha.
    Bado hata hivyo mnawajibika na yatokanayo na utaratibu mbovu wa awali, kwamaoni yangu

    ReplyDelete
  8. hapo kubalini mmechemsha jamani ila I guess you have to have some PR spin pf sort. Cha maana sasa hivi mgeungana wale wamiliki wakubwa wa majengo jijini and start something like a MOAT, meaning you guys, PPF, PSPF, NSSF, TBA etc muanzishe umoja wenu ili pamoja na mambo mengine muweze kuboresha preventive measures na huduma za uokoaji na kuwasaidia Kikosi cha Zimamoto kuwa na proper rescue team considering some of you have buildings which are more than 30 floors.

    ReplyDelete
  9. Wabia wawili watasimamiaje kitu kwa pamoja? Mkataba ndio wakuangaliwa unasema nani kati yao atateua wataalam na nani atasimamia hadi mwisho wa mradi, kama ni wote watasimamia itaonyeshwa pia, ndio maana kuna mkataba ili kuepuka michanganyo.

    ReplyDelete
  10. Load of bollocks!

    ReplyDelete
  11. nyie nhc msituzingue, mbona majengo mengine hamtuambii mnapata asilimia ngapi au mkataba ukoje?
    ebu cheueni hiyo asilimia 25 kwa wahathirika wa ajali hii.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...