Kwenda kwa:        DR ABDALLAH KIGODA, Waziri wa Viwanda na Biashara

Kuhusu:             BIASHARA YA MIITO YA SIMU (RINGBACK TONES)

Kumekuwa na malalamiko makubwa sana kuhusu biashara ya mauzo ya nyimbo kama miito kwenye simu. Malalamiko haya yalianzia kwa wasanii wenyewe na baadaye mimi binafsi niliwasilisha hoja zao Bungeni mwaka 2012. Hata hivyo, hadi sasa malalamiko haya bado hayajapatiwa ufumbuzi na hivyo wasanii kuendelea kunyonywa. Tatizo kubwa katika biashara hii ni USIRIna UNYONYAJI kwa wasanii wa Tanzania. Suala la USIRI lipo Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia. Suala la Unyonyaji lipo Wizara ya Viwanda na Biashara.

USIRI
Biashara hii ya “Ring Back Tones” (RBT) hufanywa na Kampuni za simu (Network providers) kwa kununua maudhui kutoka wachuuzi (Content Providers) ambao nao huingia mikataba na Wasanii (Content Creators). Hakuna sheria yoyote au Kanuni hapa nchini inayoongoza biashara hii na hivyo “Network providers” na “Content Providers” kuwa watu pekee wenye taarifa zote za biashara hii. Kampuni za simu hujumuisha mapato ya biashara hii na mapato yake mengine (Not Ringfenced), hawatoi taarifa za manunuzi ya nyimbo (au ‘content’ nyingine yeyote) kwa wadau na hasa wasanii. Wachuuzi (Content Providers) nao hawatoi taarifa za mauzo kwa wasanii na wanatumia uelewa mdogo wa wasanii kuwasainisha mikataba inayowanyonya. Matokeo yake ni kwamba msanii hupata kiasi cha asilimia mbili tu (2.5%) ya mapato ghafi ya kazi yake. Hivi sasa biashara hii inathamani (turnover) ya takribani shilingi 44 bilioni kwa mwaka.

Suluhisho: Serikali kupitia Wizara ya Mawasiliano iandike kanuni (regulations) zitakazolazimisha makampuni ya simu kuweka wazi mapato yatokanayo na biashara ya RBT (Miito ya simu) kila baada ya miezi 4 (disclosure rules). Kanuni hizi zielekeze makampuni kutoa taarifa za mauzo kwa kila kazi (nyimbo/vichekesho etc.)

UNYONYAJI
Kutokana na usiri ulioelezwa hapo juu, wasanii wamekuwa wakinyonywa kimapato. Kwa mfano Msanii hulipwa mapato yatokanayo na ununuzi wa awali wa kazi yake (wimbo) katika mwezi (downloads).

Lakini mapato yatokanayo na “subscriptions” ambapo mlaji hukatwa shilingi 30 kila siku msanii hapati chochote. Hivyo katika mapato ya sh. 1,300 kila mwezi kwa kila mteja kwa kila wimbo, msanii hupata mgawo wake kutoka shilingi 400 tu za ‘downloads’ na ndio maana wasanii wote nchini hupata 2.5% ya shilingi 44 bilioni zinazokusanywa na Kampuni za Simu.

Nchini Marekani biashara ya miito ya simu (RBT) imetafsiriwa kama maonyesho (Public Performances) na hivyo “copyright Association” ya Marekani imeweka kiwango cha chini cha mrahaba (royalty) ambacho msanii hulipwa. Marekani msanii hulipwa asilimia 10 ya patoghafi linalozalishwa na kazi yake kama muito wa simu.

SULUHISHO
Serikali kupitia Wizara ya Viwanda na Biashara iandike kanuni kwamba mauzo ya kazi za wasanii kama miito ya simu inachukuliwa kama ‘performance’ na kwamba Kampuni za simu zitalipa sio chini ya asilimia 12 (12%) ya mapato ghafi, ambapo asimilia 10% itakwenda kwa msanii na asilimia 2% COSOTA kwa ajili ya usimamizi na Ulinzi wa kazi za Wasanii.

HITIMISHO
Kanuni za Uwazi (disclosure rules) katika biashara hii ya ‘Ring Back Tones’ na mgawo wa haki wa mapato (fair and just revenue share) ndio suluhisho endelevu na litakaloleta tija kwa wasanii wa Tanzania na hata Serikali kukusanya mapato stahili. Kanuni (Regulations) zinazopendekezwa zianze kutumika kuanzia tarehe 1/7/2013

Kabwe Z. Zitto, Mb
Kigoma Kaskazini
Dodoma, 13 Mei 2013.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 5 mpaka sasa

  1. AnonymousMay 15, 2013

    Msaada Tutani. Wasomi Wachumi Watanzania Wazalendo hebu jitokezeni na kuelezea ukweli. Tumemsikia mtoa mada hii muda mrefu sasa. Ukweli no upi?? Kama ni kweli na si kujitafutia umaarufu, marekebisho yafanyike mapema ili haki itendeke.

    ReplyDelete
  2. mama TusajigweMay 15, 2013

    Nampenda sans huyu Zitto, huwa mara nyingi hueleza ukweli. Hutetea mambo mbalimbali, hayuko kwenye uchama wala usiasa! kwenye ukweli na uwongo hutenganisha.
    Endelea kutetea vijana hasa wasanii! Big up!
    Mama T.

    ReplyDelete
  3. AnonymousMay 15, 2013

    PENDEKEZO siyo PENDEZO

    ReplyDelete
  4. AnonymousMay 15, 2013

    Ahsante mbunge kijana kwa kuliona hilo. Hebu pia wakumbuke na wana Kigoma wa jimboni kwako waliokupa kura

    ReplyDelete
  5. AnonymousMay 15, 2013

    12 % is TOO LOW !Msambazaji kama I-tunes (inayoongoza duniani kwa digital music sales) ambayo ndio haswa ilibidi usambazaji huu ufananishwe nao huchukua asilimia 30% tu na huwapa Content Creators 70%. Wao i-tunes kama vile kampuni za simu Tanzania hunufaika na VOLUME ya watu hivyo 30% ya TZS 44bn ndio iwe ya kwao kwani mtandao wa simu walishaweka na teknolojia ya ringtones ni cheap kuiweka na imeshawalipa. Hii 12% ya kwenda kwa wasanii ya Mh. Zitto haizingatii pia ma-meneja na makampuni yanayowasimamia wasanii kwani kampuni za simu hazitaki/haziwezi kuingia mikataba lukuki na msanii mmoja mmoja. Nampongeza Mh. Zitto kwa "kukinukisha". Tuombee wahusika wanasikiliza na watachekechua na kutekeleza

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...