Na Anna Nkinda – Maelezo
Mke wa Rais Mama Salma Kikwete amepongezwa kwa jitihada zake za kuinua sekta ya michezo nchini   jambo ambalo limewafanya  vijana wengi kujipata ajira katika fani hiyo.
Pongezi hizo zimetolewa jana na Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu cha Mkoa wa Lindi  (LIREFA) Francis Ndulane wakati wachezaji wa timu ya Kariakoo ya mkoa huo walipozitembelea ofisi za Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA)  zilizopo Ikulu jijini Dar es Salaam.
Ndulane alisema kuwa mchango unaotolewa na  Mama Kikwete umewapa hari na kuwatia  moyo vijana wengi na hivyo kuweza kuendeleza sekta ya michezo mkoani humo.
Alisema kuwa hapa nchini vijana wengi wana vipaji mbalimbali, lakini hawana watu wa kuwaendeleza, hivyo alimshukuru kwa jitihada zake za kuwaendeleza katika sekta hiyo na hivi sasa  wanaamini  kuwa wataweza kujiajiri na kuweza kuzisaidia familia zao.
Kwa upande wake Mama Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya WAMA aliwapongeza wachezaji hao kwa juhudi kubwa wanayoifanya katika soka hadi kufikia hatua ya kushiriki ligi ya taifa ya mabingwa wa mkoa ngazi ya taifa na kufikia hatua ya nane bora.
Naye Mwenyekiti wa timu hiyo Abdalah Livemba aliwashukuru Mama Kikwete na Waziri wa Mambo ya Nje Bernard Membe kwa moyo walionao wa kuisaidia timu hiyo hadi kufikia  hapo ilipo.
Alimuomba kuwatafutia mdhamini ili aweze kuwasaidia  kubeba mzigo mkubwa wa kuitunza timu hiyo ambao unaelekea kuwalemea.
Mama Kikwete aliikabidhi timu hiyo zawadi za  viatu pea 29, jezi seti mbili ambazo ni 32, mipira mitatu, pampu moja  na  soksi  pea 16.
Timu ya Kariakoo inashiriki mashindano ya ligi ya mabingwa mkoa ngazi ya Taifa ambayo yalianza tarehe 12/6/2013 kwa kuzishirikisha  timu 28 kutoka nchi nzima wao wamebaki kati ya timu nane na leo wanapambana na Friends Rangers ya mkoa wa Dar es Salaam mchezo utakaofanyika katika uwanja wa Azam Complex uliopo Chamazi jijini Dar es Salaam.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 1 mpaka sasa

  1. Michezo ni muhimu kwa jumuiya na nchi yoyote inayopata changamoto kutoka kwa mataifa mengine mbali mbali.Tunasimama pamoja katika hili kuwapongeza wote wanaoshiriki katika michezo na viongozi wanautupa "tafu" katika hili. Mchango wako unatupa na utaendelea kutupa changamoto vijana tunaotaka kulitangaza taifa hili ulimwenguni.
    Kwa hili tunasema shukrani Mama Kikwete.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...