1. Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) ina jukumu la kulinda na kudumisha afya ya jamii kwa kuhakiki ubora, usalama na ufanisi wa vyakula, dawa, vipodozi na vifaa tiba.

  1. Hivi karibuni, TFDA imepokea taarifa ya kuwepo kwa hofu juu ya usalama wa dawa aina ya Diclofenac kupitia mitandao ya simu na vyombo vya habari. Kufuatia taarifa hiyo, TFDA inapenda kutoa ufafanuzi kama ifuatavyo:

a.      Diclofenac ni dawa iliyoko kwenye kundi la dawa zinazojulikana kitaalam kama “Non – Steroidal Anti-inflammatory Drugs” (NSAIDs). Dawa hizi hutumika kutuliza maumivu na kuondoa uvimbe unaosababishwa na magonjwa mbalimbali. Magonjwa hayo ni pamoja na magonjwa ya viungo, mifupa, uvimbe wa fizi na maumivu ya kichwa.  

b.      Mamlaka imesajili dawa ya Diclofenac kutoka makampuni mbalimbali ndani na nje ya nchi baada ya kutathmini ubora, usalama na ufanisi wake. Hata hivyo Diclofenac, kama ilivyo kwa dawa nyingine, ina madhara yanayofahamika. Kwa baadhi ya wagonjwa Diclofenac inaweza kusababisha vidonda vya tumbo, kuumwa kichwa, kuharisha, kutapika na kuwashwa mwili.
   
c.        Pamoja na madhara yaliyoainishwa hapo juu, hivi karibuni imetolewa taarifa na Mamlaka ya udhibiti wa dawa ya nchi za Umoja wa Ulaya (European Medicines Agency) kwamba watu wenye matatizo  ya moyo na shinikizo la damu, kisukari, waliowahi kupata kiharusi, wenye lehemu (cholesterol) nyingi kwenye damu, mshituko wa moyo na wanaovuta sigara wanaweza kupata matatizo kwenye moyo na mfumo wa damu ikiwa watatumia Diclofenac kwa kiwango kikubwa na kwa muda mrefu.

  1. Kufuatia taarifa hiyo, TFDA inaendelea kufuatilia madhara yatokanayo na dawa hii kwa kushirikiana na taasisi nyingine za kitaalam ndani na nje ya nchi ikiwa ni pamoja na Shirika la Afya Duniani (WHO). Aidha, tunawakumbusha watoa huduma za afya kutoa taarifa za madhara yatokanayo na matumizi ya dawa kwa kujaza fomu maalum zinazopatikana katika vituo vyote vya afya nchini.
  2. Mamlaka inasha+uri watoa huduma za afya nchini na wagonjwa kuchukua tahadhari za madhara haya hasa kwa watu wenye magonjwa ya moyo, shinikizo la damu, kisukari, wenye lehemu nyingi kwenye damu na wanaovuta sigara ikiwa ni pamoja na kutumia dawa mbadala.

  1. Vilevile wananchi wanashauriwa kuepuka matumizi holela ya dawa bila kupata ushauri wa kitaalam ili kuepuka madhara yanayoweza kujitokeza.

Imetolewa na:

Mkurugenzi Mkuu
Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) – Makao Makuu
S. L. P 77150
Dar-es-Salaam
Tanzania
Simu: +255 22 2450751
+255 22 2450512
Barua pepe: info@tfda.or.tz



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 1 mpaka sasa

  1. AnonymousJuly 18, 2013

    Jamani hawa hawa TFDA waliandika Diclofenac haina madhara yoyote kwa binadamu, leo nashangaa wanaandika Diclofenac ina madhara fulani kwa baadhi ya binadamu. TFDA jitahidini kuwa MAKINI na kutoa habari za UHAKIKA, fanyeni utafiti kwanza kabla hamjawaambia wanachi chochote kile.

    Sasa kuhusu UBUYU tusubirie mseme hauna madhara, wakati mlishaandika na kutuelezea kuwa UBUYU una madhara na hauifai kwa binadamu.

    TUSUBIRIE MTUAMBIE KUWA UBUYU HAUNA MADHARA YOYOTE! JE HUWA MNATAFITI KABLA AU?

    TFDA JUU JUU JUU ZAIDI.

    ILA MNAWEZA KUSHIRIKIANA NA MUHAS MANA WANA KITENGO CHA WAFAMASIA NA KUFUNDIASHA NA PIA TAASISI ZINGINE ZA KITAFITI KABLA YA KUWAAMBIA WANACHI AU KABLA YA KUPUBLICISE.

    NASUBIRIA SANA KUHUSU MAELEZO YA UBUYU KWA UAFASAHA ZAIDI NA HAYO MADHARA MLIYOSEMA MKIYA-JUSTIFY.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...