Kamati ya Ushauri ya Ugawaji wa Vitalu vya Utalii ikiwa
katika picha ya pamoja na Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi Khamis
Suedi Kagasheki (mwenye kaunda suti) na
Kaimu Katibu Mkuu, Bw. Ibrahim Mussa (wa kwanza kulia).
Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Balozi Khamis Suedi
Kagasheki amezindua rasmi Kamati ya Ushauri ya Ugawaji wa Vitalu vya
Utalii nchini.
Kamati hiyo inaundwa na wajumbe 10 kutoka sekta
mbalimbali na inajukumu la kumshauri waziri katika masuala yote yalioainishwa kwenye sheria na kanuni za Wanyamapori juu ya
ugawaji vitalu.
Akizungumza katika uzinduzi huo uliofanyika katika Ukumbi
wa Selous uliopo Wizara ya Maliasili na Utalii Makao Makuu, Dar es Salaam, Mhe.
Kagasheki alisema anaimani kamati hiyo itamsaidia kwa kumpa ushauri utakaokuwa
umefanyiwa utafiti wakina kutokana na kamati hiyo kuundwa na watu wenye uweledi
na uzoefu mbalimbali katika masuala ya usimamizi wa raslimali na maliasili.
Aidha, Mhe. Kagasheki aliwataka wajumbe wa kamati hiyo
kutekeleza majukumu waliopewa kwa kushirikiana kikamilifu na kwa kuzingatia maslahi
ya taifa.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Ushauri wa Ugawaji
wa Vitalu, Prof. Leticia Rutashobya alimshukuru Mhe. Waziri kwa kumpa jukumu la
kuongoza kamati hiyo na kuahidi kuhakikisha inatekeleza majukumu yake kwa
uadilifu.
Kamati ya Ushauri wa Ugawaji wa Vitalu inaundwa na Prof.
Leticia Rutashobya (mwenyekiti) na wajumbe wake Mhe. Zakhia Hamdan Meghji, Bw.
Alli Mufuruki, Bw. Mohamed Abdukadir, Bw. Raymond Mbilinyi, Dkt. Simon Mduma,
Bw. Allan Kijazi, Dkt. Fred Manongi, Prof. Alexander N. Songorwa na Bi. Agnes
Ndumati; na itahudumu hadi tarehe 15 Julai, 2016.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...