Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania Dkt Agnes Kijazi
katika picha ya pamoja na baadhi ya wadau wa hali ya hewa kutoka sekta mbali
mbali katika mkutano wa wadau wa utabiri wa mvua za msimu wa MASIKA kwa
mwezi Machi mpaka Mei 2014.
Kila mwaka mwezi Februari kabla ya kutoa utabiri wa msimu Mamlaka hukutana
na wadau wa sekta mbali mbali nchini ili kujadili utabiri wa msimu huo wa mvua
za MASIKA kwa kipindi cha miezi ya Machi hadi Mei na kuwapa wadau nafasi
ya kuchangia namna utabiri huo utakavyotumika katika sekta zao.
Akifungua mkutano huo Mkurugenzi Mkuu wa TMA Dkt. Agnes Kijazi alisema
mchango wa wadau katika matumizi ya utabiri ni wa muhimu kwani utabiri
unaotolewa hauwezi kuwa na manufaa endapo wadau kutoka sekta mbalimbali
hawatautumia katika kuboresha shughuli zao.Aliongeza kusema kutokana
na mabadiliko ya tabia nchi hali ya hewa imekuwa ikibadilika sana (climate
variability) hivyo akasisitiza kwamba ni muhimu sekta mbali mbali za kiuchumi na
kijamii zikatilia maanani taarifa za hali ya hewa katika mipango ya shughuli zao.
Mshiriki kutoka Wizara ya Kilimo na usalama wa chakula (MAFS-NFRA) Bw.
Joseph Peter Oganga alieleza umuhimu wa ushirikishwaji wa sekta mbalimbali
hususan kwenye upatikanaji wa chakula kwa kupanga namna ya kutumia utabiri
katika kupanga uzalishaji wa mazao husasn katika kipindi hiki ambacho dunia
nzima ikishuhudia mabadiliko ya tabia nchi .
Mshiriki kutoka Timu ya Wataalamu wa Kukabiliana na Maafa Mkoa wa Dar
es salaam – DARMAERT(Dar es salaam Multi-Agency Emergency Response
Team) Bw. Amini Mshana kwa upande wake alisema mikutano hii inasaidia sana
kujiandaa na maafa ili kupunguza athari zinazoletwa na maafa akitolewa mfano
mafuriko,mlipuko wa magonjwa n.k.
Kwa upande wa sekta ya habari, Mwakilishi kutoka Magic radio Bw Salum
Mkambala alisema wanahabari ndio kiunganishi cha jamii hivyo ni muhimu kujua
changamoto zinazoikabili TMA katika usambazaji wa taarifa za hali ya hewa na
kutafuta muafaka huku wakitumia fursa hii kuwaomba wadau wengine kutoa
taarifa zinazoeleweka kwa kila mwana jamii hususan zile zitokanazo na hali ya
hewa.
Taarifa za hali ya hewa ni muhimu katika sekta ya afya kwani magonjwa
yanayohusiana na hali ya hewa ni mengi kama vile malaria na kuharisha,
alisema mshiriki kutoka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii bw. Makono Andrew.
Wadau walioshiriki na kutoa michango yao katika mkutano huo ni kutoka
Wizara ya Afya (MNCP) Makono Andrew na Amina Kingo (Epidemiology),
Wizara ya Maji Mwasiti Rashid, Wizara ya Mifugo Lugendo Bunto,RedCross,
TBC Mwasu Sware, Salum Mkambala (Magic FM),DARMEART Amini Mshana,
Wizara ya Uchukuzi Shinja Shaffih,Ofisi ya Mkuu wa Mkoa DSM Boniface
Chija,Ofisi ya Mipango Josiah Mwabeza,Wizara ya Kilimo Joseph Ogonga,
Wizara ya Nishati na Madini Innocent Makomba,Climat Consult Philbert
Tibaijuka, Ofisi ya Waziri Mkuu (maafa) Edward Boniface,CWCAR-DSM Dkt
Mohamed Mhita.
Akifunga mkutano huo Dkt. Agnes Kijazi alisema utabiri wa msimu wa MASIKA
utatolewa rasmi tarehe 27 Februari 2014.
IMETOLEWA NA MONICA MUTONI;OFISI YA UHUSIANO MAMLAKA YA HALI YA HEWA
TANZANIA
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...