Na Mwandishi Maalum 
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon, amekiri , huwa katika wakati mgumu sana pale anapopashwa kumuandikia Balozi wa Nchi fulani, kumtaarifu kwamba mlinzi wako wa Amani amepoteza maisha wakati akitekeleza jukumu lake la ulinzi wa Amani. 
 Ban Ki Moon, ameyasema hayo wakati wa siku ya Kimataifa ya kuwakumbuka na kuwaenzi walizi wa Amani wa Umoja wa Mataifa ( Blue Helmet) na ambao wamepoteza maisha katika mwaka uliopita. Siku hiyo hufanyika Mei 29 ya kila mwaka. 
Kwa mwaka jana ( 2013) Jumla ya walinzi wa Amani wa Umoja wa Mataifa 106 wanaohudumu katika operesheni za Umoja wa Mataifa za kulinda Amani katika maeneo mbalimbali duniani walipoteza maisha . 
“Waheshimiwa Mabalozi mliopo hapa leo, naomba niwashukuru sana kwa niaba ya serikali zenu kwa kujitolea walinzi wa Amani ambao wanahudumu katika mazingira hatari sana. Lakini nikiri mbele yenu kuwa huwa ninakuwa mnyonge sana pale ninapopashwa kuwaandikia barua kwamba mlinzi wako wa Amani amepoteza maisha, naomba uitaarifu familia yake na Serikali yako” akasema Ban Ki Moon kwa huzuni. 
Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa, anasema “ Hata kama ni kuandika barua ya kutaarifu kupotea kwa maisha ya mlinzi mmoja, kwangu huwa ni majonzi makubwa, ninahuzunika kwa maisha yake kupotea lakini pia naifikiria sana familia yake iliyoondokewa na mpendwa wao” 
Hafla hiyo wa kuwakumbuka na kuwaenzi walinzi wa Amani ilitanguliwa na uwekaji wa shada la Maua katika eneo maalum lilotengwa kwaajili hiyo katika viunga ya Umoja wa Mataifa na kufuatiwa na utoaji wa medali ya Dag Hammrskjold Medal kwa kila aliyepoteza maisha. 
Naibu Muwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Balozi Ramadhan Muombwa Mwinyi ndiye aliyepokea medali za mashuja wa Tanzania ambazo baadaye zitakabidhiwa kwa familia za walinzi hao.
 Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika mwaka huo imepoteza mashuja wake 10, Saba wakipoteza maisha huko Darfur ( UNAMID) na watatu walipoteza maisha Mashariki ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ( MONUSCO).
 Mashuja hao ni Maj Khatibu Shabaan MSHINDO, Lt Rajabu Ahmed MLIMA,Pte Hugo Barnabas MUNGA, Pte Peter Muhiri WEREMA,Pte Rodney Gido NDUGURU, Cpl Oswald Paul CHAULA,Sgt Shaibu Shehe OTHMAN, Cpl Mohamed Juma ALI, Cpl Mohamed Chukulizo MPANDANA na Pte Photunatus Wilbard MSOFE.
 “Tunamlilia kila shuja aliyepoteza maisha kwa uhodari mkubwa, tunaomboleza pamoja na familia na rafiki zao. Lakini pia tunaowajibu wa kuhakikisha kwamba tunaimarisha mazingira ya utendaji kazi wao.” Akasisitiza Ban Ki Moon. 
Katibu Mkuu , akaeleza zaidi kwamba mwaka 2013 ulikuwa mwaka wa sita mfululizo ambapo walinzi wa Amani zadi ya 100 wamepoteza maisha. 
Baadhi yao waliuawa wakati misafara yao ilipovamiwa huko Darfur na Sudani ya Kusini, wengine wakapoteza maisha kwa kulipuliwa na mabomu ya kutega kama vile Mali, wengine wakapoteza maisha kwa kusombwa na mafuriko. 
“ Katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ( DRC) na kwingineko walinzi wetu wa Amani waliuawa wakati wakitoa ulinzi kwa raia, huku wengine kama vile Mashariki ya Kati na Haiti wakipoteza maisha kwa magonjwa ya mlipuko”anaeleza zaidi Katibu Mkuu. 
 Umoja wa Mataifa una zaidi ya walinzi wa Amani 116,000 kutoka nchi 120 wanaohudumu katika Operesheni 16 za kulinda Amani. Jumla ya walinzi wa Amani 3,200 wameshapoteza maisha tangu Umoja wa Mataifa ulipoanzisha Operesheni za kulinda Amani.
 . Bango lenye Majina ya Walinzi wa Amani 106 ambao wamepoteza maisha  mwaka 2013 wakati wakitekeleza dhamana ya  ulinzi wa Amani chini ya Mwamvuli wa Umoja wa Mataifa.  Kati ya walinzi hao 106 wamo watanzania 10.
 Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa,  Ban Ki Moon, akizungumza wakati wa hafla ya siku ya Kimataifa ya  kuwakumbuka na kuwaenzi walinzi wa Amani wa Umoja wa Mataifa, pamoja na  106 waliopoteza maisha mwaka jana, kumbukumbu hiyo hufanyika  Mei 29 kila mwaka.  Katika Salamu zake, Katibu Mkuu ameeleza kwamba hupata wakati mgumu sana kumtaarifu  Mwakilishi wa Kudumu wa nchi ambayo  Mlinzi wake wa Amani au Walinzi wake wa Amani wamepoteza maisha wakati wakitekeleza majukumu yao.

Naibu Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Balozi Ramadhan Muombwa Mwinyi akipokea  kutoka kwa Mkuu wa  Idara ya Operesheni za Ulinzi wa  Amani, Bw. Herve Ladsous   Medali ya  Dag Hammarskjold kwa niaba ya mashujaa 10 watanzania waliopoteza maisha mwaka jana huko Darfur na DRC.  Nyuma  ya Balozi ni Lt  Kanali Wilbert Ibunge, Mwambata Jeshi Uwakilishi wa Kudumu.

Balozi Mwinyi akisaini kitabu  na nyuma ni Lt Kanali Wilbert Ibunge
 Hii ndiyo Medali wanayopewa walinzi wa amani ambao wamepoteza maisha wakitekeleza jukumu lao la  kulinda amani, Medali hii hupewa Familia ya Marehemu si ya kuvaa bali ni ya kuweka nyumbani
Sehemu ya wageni waliohudhuria  hafla  hiyo ambayo awali ilitanguliwa na uwekaji wa Shada la Maua kwa  heshima ya mashujaa hao

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...