Kocha Jackson Mayanja wa Kagera Sugar amepigwa faini ya sh.
500,000 na kufungiwa mechi tatu kwa kutoa lugha ya kashfa kwa maneno na vitendo
kwa waamuzi wa mechi yao na Mtibwa Sugar kuwa walipewa rushwa.
Adhabu dhidi ya Kocha Mayanja kwenye mechi hiyo namba 136
iliyochezwa Aprili 1, 2015 kwenye Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga imetolewa
kwa kuzingatia kanuni ya 40(1) ya Ligi Kuu.
Klabu ya Mtibwa Sugar imepigwa faini ya sh. 500,000 baada ya
timu yake kukataa kuingia vyumbani wakati wa mapumziko katika mechi namba 142
dhidi ya Stand United iliyochezwa Aprili 5, 2015 katika Uwanja wa Kambarage
mjini Shinyanga. Adhabu hiyo imetolewa kwa mujibu wa kanuni ya 14(13) ya
Ligi Kuu.
Nayo Simba imepigwa faini ya sh. 300,000 kwa mujibu wa
kanuni ya 14(9) ya Ligi Kuu baada ya timu yao kugoma kuingia kwenye vyumba vya
kuvalia nguo (changing room) kwenye Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga wakati
wa mechi dhidi ya Kagera Sugar. Hatua hiyo ilisababisha wachezaji wakaguliwe
kwenye gari lao.
Pia Simba imepigwa faini ya sh. 500,000 kwa kuzingatia kanuni ya
14(13) ya Ligi Kuu baada ya vilevile kugoma kuingia vyumbani wakati wa
mapumziko kwenye mechi hiyo hiyo namba 146 iliyochezwa Aprili 6, 2015.
Kipa Tony Kavishe wa Polisi Morogoro amepigwa faini ya sh. 500,000
na kufungiwa mechi tatu kwa kosa la kumpiga ngumi mwamuzi msaidizi namba mbili,
Hassan Zani kwa kuzingatia kanuni ya 37(5) ya Ligi Kuu. Alifanya kosa hilo
kwenye mechi namba 147 dhidi ya Mgambo Shooting iliyochezwa Aprili 5, 2015
katika Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...