![]() |
Mchora vibonzo Nathan Mpangala akifundisha uchoraji baadhi ya wanafunzi wa Shule ya Msingi Koboko, Moshi mwaka 2011. Ili tufanikiwe katika sanaa, uibuaji na ukuzaji vipaji kuanzia umri mdogo havikwepeki. |
Hivi karibuni, Rais wa Jamhuri wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, ameteua Baraza la Mawaziri ikiwemo Wizara ya Habari, Michezo, Utamaduni na Wasanii (Sanaa) inayoongozwa na Mh. Nape Nnahuye.
Binafsi kutajwa moja kwa moja kwa wasanii (wa sanaa za ufundi, muziki, filamu na jukwaani) katika wizara naona ni hatua moja mbele. Sasa, natarajia wizara itajishughulikia maswala ya wasanii kwa mtazamo tofauti na miaka iliyopita ambapo wasanii tulijumuishwa kwenye kapu la utamaduni hali iliyosababisha kutokuwepo kwa njia rasmi za uibuaji na uendelezaji vipaji, kutokuwepo na ulinzi wa ubunifu, sanaa kutochukuliwa kama ajira rasmi nk.
Nachukua nafasi hii kutoa wito kwa wachora vibonzo wote nchini, kama wafanyavyo wasanii wa sanaa za aina nyingine nasi tujitokeze, tupaze sauti, tusemee maono na matarajio yetu ili tuisaidie serikali ya awamu ya tano katika mipango yake inayohusiana habari na wasanii.
Kwa kipindi kirefu sasa, wachora vibonzo nchini tumekuwa tukielimisha, kufundisha, kuburudisha na hata kuitangaza nchi kimataifa. Pia tumesaidia mauzo ya magazeti na kuvutia watazamaji kwenye luninga.
Pamoja na mafanikio hayo, kumekuwa na changamoto mbalimbali ambazo zikikwamisha fani hii. Vikwazo hivo ni pamoja na kutokuwepo kwa njia rasmi ya uibuaji na ukuzaji vipaji mashuleni, wachora vibonzo wengi wao kutokuwa na mikataba ya kazi, kuwepo kwa mazingira ya kazi ambayo si rafiki, malipo duni na wakati mwingine hayana uhakika, kutokuwepo kwa mafunzo ya mara kwa mara, wachoraji vibonzo tumepuuzia vikundi/vyama vyetu vya kutetea stahiki zetu za jumla nk.
Hali hii imefanya uchoraji vibonzo kutoshamiri ukilinganisha mataifa yaliyoendelea. Hatuna uhakika na kesho. Imeathiri ubunifu, mafunzo, vipato na haki miliki. Wachora vibonzo wanaochipukia wamekuwa wakikatishwa tamaa.
Sasa ni wakati mwafaka wachora vibonzo tujitokeze, tuzisemee haki zetu ambazo tunaamini ni stahiki yetu. Tukifanya hivyo tutakuwa tunajiwekea mazingira mazuri ya kazi na pia tutakuwa tumekitendea haki kizazi kijacho. Uhakika wa uibuaji, ukuzaji na ulinzi wa ubunifu na haki zingine za wachoraji vibonzo wa kesho inategemea misingi imara tutakayoiweka leo.
Baadhi ya matarajio yetu toka kwa serikali ya awamu ya tano;
1. Somo la sanaa lirudishwe mashuleni kama ilivyokuwa miaka ya nyuma.
2. Wakati huu Serikali inapopanga mikakati yake kuhusu wasanii ikumbuke kuwa kuna wachora vibonzo.
3. Kwa kuwa tunafanya kazi katika vyombo vya habari, serikali inapokuwa ikishughulikia masuala ya habari isisahau kwamba wachora vibonzo nao ni sehemu na wana uzito sawa kama ilivyo kwa wanahabari wengine.
4. Kwa kuwa hakuna njia rasmi za ukuzaji sanaa ya uchoraji vibonzo nchini, natoa wito kwa vyombo vya habari kugharama mafunzo ya wachora vibonzo mara moja moja.
5. Wachora vibonzo, huu si wakati tena wa kunung’unika. Tuungane, tupaze sauti ya pamoja kuhusu stahiki zetu ili tuisaidie serikali ya awamu ya tano kujua maono na matarajio yetu. Tukiendelea kukumbatia ubinafsi, hakuna mtu atakayesimama kwa niaba yetu. Na ikitokea serikali kutusahau basi kabla hatujainyooshea kidole itabidi kwanza tujilaumu wenyewe. Sauti ya pamoja inahitajika katika hili tena sasa hivi.
6. Tuimarishe vikundi/vyama vyetu ili tuvitumie kutetea stahiki zetu na kizazi kitakachokuja. Katika hili hakuna njia ya mkato.
7. Kwa kuwa wengi wetu tunajitegemea, ni wakati mwafaka sasa wa kuwepo kwa mikataba baina ya wachora vibonzo na vyombo tunavyofanyia kazi. Pamoja na mambo mengine mikataba hiyo izingatie haki miliki na malipo ya kuridhisha.
Kwa kumalizia navishukuru vyombo vya habari kwa kutumia vibonzo kwa wingi. Pia, nazipongeza taasisi mbalimbali za serikali na binafsi kwa kutumia vibonzo kwenye machapisho yao.
Mwisho lakini si kwa umuhimu, nazipongeza taasisi mbalimbali ambazo zimetambua na kuamua kutoa tuzo kwa wachoraji vibonzo. Hatua hii inatia moyo na tunaiunga mkono kwani inachochea ubunifu zaidi.
Asante.
Imetolewa na:
Nathan Mpangala,
(Mchora vibonzo),
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...