Na Bashir Yakub.
Hakimiliki katika masuala ya ardhi huhusisha umiliki wa ardhi zenye hati. Umiliki huu hutoa wajibu na haki fulani kwa mmiliki katika ardhi husika. Si rahisi kudai una hakimiliki katika ardhi kama hauna hati.
Aidha tumezoea kuona hati zilizo na jina la mtu mmoja mmoja. Hii ni hata kwa wanandoa ambao hudai mali husika zinatokana na jasho lao wote. Lakini je unajua kuwa inawezekana hati miliki ikawa na majina ya wanandoa wote badala ya kuwa na jina la mmoja tu hasa baba ambao ndio wengi hupenda majina yao yaonekane hapo ?. Jambo hili linawezekana na linaruhusiwa.
1.HAKIMILIKI YA PAMOJA KUONDOA MGOGORO.
Kutokuelewana ambako mara kadhaa hutokea baada ya kifo cha mmoja wa wanandoa kwaweza kuondolewa na umiliki wa ardhi wa pamoja. Ikiwa una wasiwasi juu ya mustakabali wa mali hasa ardhi huko mbeleni ni vema basi ukachukua hatua hii ya kusajili kwa umiliki wa pamoja.
Kama kiwanja/ nyumba ina hati yenye majina mawili la baba na mama halafu mmoja wao akafariki itakuwa ni vigumu ndugu au mwingine yeyote mwenye nia mbaya kudai umiliki wa kiwanja/nyumba hiyo.
Lakini hali itakuwa tofauti iwapo hati ina jina la mmoja na huyohuyo mmoja ndiye aliyefariki. Pale pote ambapo ndugu walidhulumu mali za marehemu hasa ardhi ni pale ambapo kuna jina la mmoja.
Mara nyingi fitina huingia pale penye mwanya wa kufanya hivyo. Si rahisi fitina kuingia pasi na mwanya. Kuweka majina ya wanandoa wote kwenye hati za ardhi ni hatua ya kuziba mwanya wa fitina. Itawezekanaje ndugu au mwingine mwenye nia ovu kudai umiliki wa ardhi ya marehemu huku akijua kuwa hati inalo jina la mke pia. Si rahisi hata kidogo.
Lakini pia umiliki wa pamoja huondoa mgogoro pale panapo talaka. Swali la je mwanandoa fulani amechangia chochote katika kupatikana kwa mali huwa halipo ikiwa majina yote mawili ya wanandoa yameonekana kwenye hati.
asante kwa kutuelimisha Mungu akubariki, mara nyingi watanzania tunaishi kwa mazoea, elimu hii itawafungua wengi macho!!!
ReplyDelete