Na Latifah Boma
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo amelitaka Shirika la Umeme nchini (Tanesco) liongeze juhudi katika kuhamasisha wananchi kuunganishwa na huduma ya umeme.
Aliyasema hayo katika mkutano baina yake na wawakilishi kutoka kampuni inayosambaza umeme vijijini ya Derm Electronics na watendaji kutoka Tanesco na Wakala wa Nishati Vijijini (REA), uliofanyika katikati ya wiki hii, jijini Dar es Salaam.
Kampuni hiyo, inayosambaza umeme mkoani Dodoma na Mara, ilieleza kuwa moja ya changamoto kubwa inayoipata katika utekelezaji wa kazi zake ni muamko mdogo kutoka kwa wananchi kutaka kujiunga na huduma ya umeme.
Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Derm Electronics, Ridhuani Mringo alisema kuwa suala hilo limewafanya wakumbwe na changamoto ya kutimiza malengo yao ya kusambaza umeme kwa idadi iliyopangwa katika makubaliano na Serikali.
Alisema wameweza kuunganishia umeme kwa wananchi takribani 2,000 kati ya 11,000 waliotarajiwa mkoani Dodoma na wananchi takribani 3,000 kati ya 14,000 mkoani Mara.
Aidha, Profesa Muhongo aliipongeza kampuni hiyo kwa kufanya kazi nzuri kwani wameweza kumaliza asilimia 96 ya kazi yao, wakiwa wameweza kupitisha umeme katika vijiji 125 mkoani Dodoma na vijiji 161 mkoani Mara.
Profesa Muhongo pia aliwaagiza watendaji kutoka Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kufanya ukaguzi, baada ya wiki moja katika maeneo ya kazi ya wakandarasi hao wanaosambaza umeme vijijini ili kuhakikisha kuwa kazi hizo zinafanyika kwa ufanisi.
Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Derm Electronics, Ridhuani Mringo (mwenye miwani) akimueleza jambo Profesa Muhongo katika mkutano kati ya Wizara na kampuni ya Derm Electronics uliofanyika katikati ya wiki hii, jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (katikati) akimsikiliza mmoja ya watendaji kutoka Shirika la Umeme nchini (TANESCO) waliohudhuria mkutano kati ya Wizara na kampuni ya Derm Electronics uliofanyika katikati ya wiki hii, jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya wawakilishi kutoka kampuni ya Derm Electronics na watendaji kutoka Shirika la Umeme nchini (Tanesco) na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) wakifuatilia mkutano kati ya Wizara na kampuni ya Derm Electronics uliofanyika katikati ya wiki hii, jijini Dar es Salaam. Wa Tatu kulia ni Mkurugenzi Mkuu wa REA, Dkt. Lutengano Mwakahesya na wa Pili kulia ni Mkurugenzi wa Ufundi kutoka REA, Mhandisi Bengie Msofe.


BUNDA MANYAMANYAMA WAMESIMAMISHA NGUZO TU HAKUNA KINACHOENDELEA, JAMANI TUSAIDIENI ILI TUWEZE KUUNGANISHA UMEME MAJUMBANI MWETU
ReplyDelete