Mkuu wa wilaya ya Babati Crispin Meela
Na Woinde Shizza,Manyara

Mkuu wa Wilaya ya Babati Mkoani Manyara, Crispin Meela ameifunga shule ya msingi Matufa kwa muda usiojulikana baada ya kutitia kwa matundu ya vyoo vya wanafunzi na walimu kutokana na mafuriko yaliyosababishwa na mvua zinazonyesha.

Akizungumza baada ya kuitembelea shule hiyo, Meela alisema kutokana na matundu  24 ya vyoo vya shule hiyo kuharibika inabidi shule hiyo ifungwe kwani hakuna vyoo vingine vya kutumiwa kwa wanafunzi na walimu. Hata hivyo, kaya 64 zilizokuwa zinaishi kwenye shule hiyo ya Matufa kwa kukosa makazi baada ya nyumba zao kusombwa na mafuriko yaliyosababishwa na mvua zilizonyesha siku mbili hivi sasa wamepatiwa hifadhi kwa kuwekwa kambini.

Alisema kutokana na maafa hayo hana budi kuifunga shule hiyo kwa muda usiojulikana na anatarajia watahakikisha tatizo hilo linapatiwa ufumbuzi kwa muda mfupi kupitia ushirikiano wa viongozi wa wilaya na mkoa huo. “Namuagiza mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Babati vijijini Dominick Kweka, kuhakikisha shule hiyo inajengewa vyoo mara baada ya wiki moja kupita ili wanafunzi waweze kuendelea na masomo yao,” alisema Meela.

Kwa upande wake, mbunge wa jimbo la Babati vijijini Vrajlal Jitu Soni aliwapa pole wakazi wa vijiji vya Magugu na Matufa vilivyopo kwenye tarafa ya Mbugwe ambao wameathirika kutokana na mafuriko hayo. Jitu Soni alisema hivi sasa wanafanya tathmini ya mafuriko hayo ili kamati ya maafa kupitia ofisi ya Waziri Mkuu waweze kuwapatia msaada wananchi hao ambao nyumba na mazao yao yamechukuliwa na mafuriko hayo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...