Na Eleuteri
Mangi-MAELEZO.
Wanadamu wameumbwa kwa hulka
na silika ya kuwa na uwezo wa kuwasiliana miongoni mwao, jamii wanamoishi,
taifa na hata ulimwenguni ili waweze kutimiza nia na azma yao ya kuwasiliana.Ili mawasiliano hayo yakamilike
ni lazima yabebe ujumbe unaokusudiwa kufikishwa katika jamii.
Ujumbe huo ili uweze
kumfikia mlengwa, ni lazima iwepo njia ya kuufikisha ujumbe huo kwa mlengwa
ambao huwasilishwa kwa maandishi (magazeti), sauti (redio) na picha (TV) pamoja
na mitandao ya kijamii kupitia huduma ya inteneti.Vyombo hivyo vya habari
vinahusisha wataalamu ambao kazi yao ni kuhakikisha jamii inapata ujumbe kwa wakati
ili kuweza kujenga, kuboresha na kuimarisha maisha yao kiuchumi, kijamii, kisiasa
na kiutamaduni.
Vyombo vya habari hakika
vimekuwa ndio macho na masikio ya wananchi ili kufikisha ujumbe unaohusu mambo
mbalimbali yanayofanyika ndani na nje ya nchi.
Tunapoelekea siku ya maadhimisho
ya uhuru wa vyombo vya habari duniani ambayo huadhimishwa kila mwaka Mei 2 na 3,
maadhimisho hayo mwaka huu yataadhimishwa nchini Finland, ambapo wanahabari
wote duniani wataungana kuwakumbuka wenzao waliofariki dunia walipokuwa wakitekeleza
majukumu yao na kupanga mipango mipya ya namna watakavyoboresha kazi zao ziwe za
ufanisi zaidi.
Tanzania ikiwa miongoni
mwa mataifa ya dunia hii, nayo haipo nyuma katika suala la uwepo wa vyombo vya
habari.
Ni dhahiri vyombo vya
habari nchini vimekuwa kiungo muhimu katika kisaidia Serikali kutoa taarifa
mbalimbali na ajira hatua ambayo imesaidia kupunguza tatizo la ajira nchini.Ukilinganisha na nchi
nyingine za Afrika Mashariki, Tanzania inayoongoza kwa kuwa na vyombo vingi vya
habari, hali ambayo ni msingi wa kuajiri watu wengi zaidi katika tasnia hiyo.
Waziri wa Habari,
Utamaduni, Sanaa na Michezo Nape Nnauye ambaye ndiye mwenye dhamana ya habari
nchini anasema Serikali inaunga mkono juhudi zinazofanywa na vyombo vya habari
nchini.“Tulipofika ni pazuri
ukilinganisha na tulipotoka, mengi yamefanyika hasa ukiangalia idadi ya vyombo
vya habari nchini na uhuru wa waandishi wa habari wanavyoanadika na wanavyofikisha
ujumbe kwa wasomaji, wasikilizaji na watazamaji” alisema Waziri Nape.
Aidha, Waziri Nape
amesema kuwa bado Serikali inakusudia kuboresha mazingira ya waandishi wa
habari ili waweze kufanya kazi zao kwa hali ya uhuru hasa wanapotimiza majukumu
yao ya kiundishi wa habari.Kwa mujibu wa takwimu
za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ambacho ni chombo kilichoanzishwa
kisheria kusimamia sekta za mawasiliano na utangazaji nchini hadi sasa kuna jumla
ya vituo kadhaa vya radio na televisheni vilivyosajiliwa.
Idadi ya vituo vya redio
vilivyosajiliwa nchini hadi sasa ni 123 ambavyo ni sawa na asilimia 43.4 katika
ukanda wa Afrika Mashariki huku miongoni mwa vituo hivyo vinamilikiwa na
makampuni binafsi, taasisi na mashirirka ya dini, jamii na Serikali ambayo inayomiliki
kituo kimoja cha TBC Taifa inayoendeshwa chini ya Shirika la Taifa la
Utangazaji (TBC), nchini Kenya vipo vituo vya redio 118 sawa na asilimia 41.7,
Uganda 37 sawa na asilimia 13.1, Rwanda vituo vitatu sawa na asilimia 1.1 wakati
Burundi ina vituo vya redio viwili ambavyo ni sawa na asilimia 0.7.





Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...