JESHI la Magereza limesaini Mkataba (MoU) na Taasisi isiyo ya Kiserikali ya Technoserve
– Tanzania kushirikiana katika ufundishaji wa wafungwa mafunzo ya Ujasiriamali
wakiwa wanakaribia kumaliza vifungo vyao magerezani ili stadi hizo ziwasaidie
kumudu maisha mapya baada ya kutumikia adhabu zao.
Programu
hii itaendeshwa katika Mkoa wa Mbeya kwa kushirikiana na Mfuko wa “Master Card” kwa vijana wa kike na kiume wenye umri kati ya
miaka 18 hadi 30 hivyo wafungwa walioko katika Magereza yaliyomo Mkoani humo na
wengine wenye sifa toka Kanda ya Nyanda za Juu Kusini ili kupata mafunzo kupitia
progamu ya uimarishaji wa maendeleo ya vijana vijijini kupitia biashara “STRYDE”
inayoendeshwa na Taasisi hiyo.
Takwimu
za sasa zinaonesha kwamba kati ya asilimia 30 na 35 ya wafungwa wanaomaliza
vifungo vyao hurejea magerezani.Hivyo, mafunzo haya yatalenga kuwafanya wanapomaliza vifungo vyao waweze kupata maarifa
ya kuanzisha shughuli zao wenyewe za kujipatia kipato halali na kuacha vitendo
vya uhalifu katika jamii wanamoishi vinavyowafanya kurejea magerezani.
Aidha,
mafunzo haya ya Ujasiriamali yatajikita
katika kuwafundisha kilimo biashara, matumizi mazuri ya fedha binafsi, uwezo wa
kutumia ujuzi, ubunifu na tafakari ya kina katika kufanya maamuzi, mpango
biashara, mawazo ya biashara na uwezo wa kuandaa mpango biashara n.k.
Ushirikiano
huu ni mkakati endelevu wa Jeshi la Magereza katika kuboresha Programu za Urekebishaji
wa wafungwa magerezani ili wawe raia wema na wenye tija katika jamii na Taifa
kwa ujumla.
Program
za Ujasiriamali kwa wafungwa zinaendeshwa pia katika baadhi ya Magereza kwa
kushirikiana na wadau mbalimbali kama vile Dorcas International na New
Life in Christ katika Gereza la Karanga – ushonaji viatu, ufumaji na
uokaji mikate, Gereza Arusha – uokaji mikate, ufundi seremala na ufumaji.
Jeshi
la Magereza linawakaribisha wadau wa ndani na nje kushirikiana katika
urekebishaji wa tabia za wafungwa ili wawe na michango chanya katika jamii na
Taifa kwa ujumla.
IMETOLEWA NA KITENGO CHA HABARI NA MAWASILIANO
MAKAO MAKUU YA JESHI LA MAGEREZA
DAR ES SALAAM.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...