Na Zainab Nyamka, Globu ya Jamii.
SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Nchini (TFF) limekanusha kuhusika na taarifa za upotoshaji zinazoendelea kuenea juu uratibu na ushiriki wa timu ya Yanga katika mashindano ya Kombe la Shirikisho msimu wa 2015/16. TFF imekanusha taarifa hizo za wao kutuhukiwa kuihujumu Yanga zinazotolewa na Mkuu wa Kitengo cha habari na mawasiliano wa klabu hiyo Jerry Muro kupitia vyombo mbalimbali vya habari.

Akitolea ufafanuzi suala hilo Afisa habari wa TFF, Alfred Lucas amesema kuwa shirikisho hilo limekuwa likitoa kwa Yanga na Azam katika uwakilishi wao wa nchi kwenye mashindanmo ya kimataifa. Aprili 21 Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) lilitoa waraka kwa timu zilizokuwa zikiwania kuingia hatua ya Makundi (Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho) kupeleka majina ya maofisa watakaohudhuria warsha ya namna ya kuratibu mechi hizo kuelekea fainali wakiambatanisha na vivuli (photocopies) vya hati zao za kusafiria.

Viongozi waliohitajika ni meneja wa timu, Daktari na ofisa habari wa timu na taarifa hiyo iliwafikia kabla ya Yanga kucheza na Esperanca ya Angola huku TFF ikiwaataarifu timu hiyo kutuma nyaraka hizo kati ya Aprili 26 na Aprili 28 na kuwa lengo la warsha ile ilikuwa  kujadili maswala ya uratibu, ufundi, udhamini na kanuni za mashindano huku CAF ilijitolea kugharamia usafiri, malazi na gharama zote kwa watu watatu kutoka Yanga. 

"Taarifa hizi na hata ukumbusho zilipelekwa kwa baruapepe, simu na hata kuonana ana kwa ana kwa Katibu Mkuu wa Yanga, Ofisa Habari na Viongozi wengine wa klabu", amesema Alfred. Maofisa wa TFF kwa nyakati tofauti waliwataka viongozi hao wa Yanga na kuwakumbusha kutuma majina CAF na vivuli vya hati hati ya kusafiria, lakini kwa sababu wanazoweza kuzielezea wenyewe kwa nini hawakupeleka majina.

Amesema, Mei 22 ikiwa ni siku mbili kabla ya warsha kuanza Kaimu Katibu Mkuu wa Yanga Baraka Deusdedit alituma majina CAF yakiwa hayana vivuli vya hati ya kusafiria na siku moja kabla ya washiriki kuanza kuwasili Cairo, Baraka alituma nyaraka kama zilivyotakiwa na wakatumiwa tiketi tatu na CAF lakini hawakusafiri wakidai klabu haijatoa ruhusa.

"Licha ya juhudi zote hizi tulizozifanya lakini Yanga wanaona sisi hatufai na kuwahujumu jambo ambalo ni opotoshwaji mkubwa kwani wanapaswa kuwaambia ukweli mashabiki na wanachama wao", amesema Alfred.  Lawama hizo zinazotolewa na  Muro ni yale yaliyotolewa kwa timu zote kwenye semina ya Cairo, Misri hivyo hawana sababu ya kulalamika na kuichafua TFF. Aidha amesema kuwa, TFF haitasita kuchukua hatua za kinidhamu kwa wasemaji wa klabu wanaochafua jina la TFF kwa kuficha madhaifu yao ya kiutawala.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...