Na Mwandishi wetu, Sikonge
WAZEE wanaonufaika na fedha zinazotolewa na serikali katika mpango
wake wa kunusuru kaya maskini kupitia mradi wa TASAF III wilayani
Sikonge Mkoani Tabora wameanza kufunguka juu ya manufaa wanayopata
kupitia mpango huo.
Wakizungumza na mwandishi wa gazeti hili juzi wakati wa zoezi la kugawiwa fedha hizo ikiwa ni mgao wa 6 tangu kuanza kwa mradi huo, wazee hao walisema wazi kuwa mpango huo umeanza kuboresha maisha yao sambamba na afya zao.
Walisema fedha hizo zimewawezesha kuwa na
uhakika wa maisha sambamba na kupata milo 3 ya chakula na sasa wana afya njema sana.
Mzee Nikulao Hussein (75) mkazi wa kijiji cha Chabutwa Mashariki
katika kata ya Chabutwa wilayani Sikonge alisema mwanzoni
alipewa sh 30,000 akazitumia kwa chakula tu lakini mgao uliofuata
alinunua kuku 2 baadae 3.
Mratibu wa TASAF wilayani Sikonge Mkoani Tabora Claud Nkanwa (wa pili kutoka kulia) akisimamia zoezi la uhawilishaji fedha kwa kaya maskini katika kijiji cha Mitwigu wilayani humo.
Aliongeza kuwa fedha hizo japo ni kidogo
lakini zinawasaidia sana kimaisha kwani zamani alikuwa anaishi maisha ya
taabu sana ikiwemo kuomba omba lakini sasa haombi tena kwa watu.
‘Sasa siombi tena chakula kwa watu, naomba serikali
iache mradi huu uendelee, wasiuondoe,' aliongeza.
Mzee Magubika Andrea (80) mkazi wa kijiji cha Mitwigu anaeleza kuwa
tangu aanze kupata hela za TASAF III maisha yake yamebadilika sana
kwani ana uhakika wa kupata chakula kila siku na tayari amefuga kuku
10 na amepanga kununua bati moja moja ili kuezeka nyumba yake, anataka
kuondoa nyasi.
Wananchi wa kijiji Mitwigu wilayani Sikonge Mkoani Tabora wakiwa kwenye foleni ya uwezeshwaji fedha za TASAF juzi.
Mzee Mrisho Athuman (74) wa kijiji cha Kikungu alieleza bayana kuwa
alikuwa anaumwa sana na chakula kilikuwa hamna, lakini baada ya kupata
hela hizo akanunua dawa na chakula, sasa ameshapona na afya yake
imerudi vizuri hana wasiwasi tena ameanza kunawili.
‘Kama sio hizi hela za serikali ningekufa mapema, nilikuwa
naumwa sana, ndani chakula hamna, watoto hawaendi shule hata nguo
walikuwa hawana, baada ya kupewa hela sasa watoto wanasoma, na mimi
nimepona kabisa na nina kuku 6’, aliongeza.
Bi.Anet Joel Sangira (74) mkazi wa kitongoji cha Magharibi kata ya
Chabutwa anasema hali yake ilikuwa duni sana lakini baada ya
kuwezeshwa 40,000 za awali watoto wake 3 na wajukuu 2 waliokuwa
wameacha shule sasa wanaenda wote na mmoja amekuwa wa kwanza darasani
kati ya watoto 60.
Wazee wa kijiji cha Chabutwa wilayani Sikonge Mkoani Tabora wakisubiri mgao wa fedha za TASAF(Picha na Allan Ntana).
‘Nyumba yangu ilikuwa ya nyasi sasa nimebadilisha nimeweka bati upande
mmoja nitamalizia upande mwingine kidogo kidogo nikipata hela
nyingine’, alisema Salome.
Mratibu wa Mradi wa TASAF wilayani Sikonge Claud Nkanwa anaeleza kuwa
mradi huu umewasaidia sana wananchi wengi kwani wengi wao walikuwa
wanakula mlo mmoja tu kwa siku kutokana na kuishi maisha ya umaskini.
Anaelezea changamoto kubwa anayokumbana nayo kuwa ni baadhi ya
wananchi kuomba kuongezewa hela kwa msingi kwamba hela wanayopewa ni kidogo na kwamba wanashindwa kuigawa kwa chakula na kuanzisha miradi.


Kuondoa umasikini ni wajibu wa kila mtanzania.
ReplyDelete