Na Mwandishi wetu, Sikonge

WAZEE wanaonufaika na fedha zinazotolewa na serikali katika mpango wake wa kunusuru kaya maskini kupitia mradi wa TASAF III wilayani Sikonge Mkoani Tabora wameanza kufunguka juu ya manufaa wanayopata kupitia mpango huo.

Wakizungumza na mwandishi wa gazeti hili juzi wakati wa zoezi la kugawiwa fedha hizo ikiwa ni mgao wa 6 tangu kuanza kwa mradi huo, wazee hao walisema wazi kuwa mpango huo umeanza kuboresha maisha yao sambamba na afya zao.

Walisema fedha hizo zimewawezesha kuwa na uhakika wa maisha sambamba na kupata milo 3 ya chakula na sasa wana afya njema sana.

Mzee Nikulao Hussein (75) mkazi wa kijiji cha Chabutwa Mashariki katika kata ya Chabutwa wilayani Sikonge alisema mwanzoni alipewa sh 30,000 akazitumia kwa chakula tu lakini mgao uliofuata alinunua kuku 2 baadae 3.
Mratibu wa TASAF wilayani Sikonge Mkoani Tabora Claud Nkanwa (wa pili kutoka kulia) akisimamia zoezi la uhawilishaji fedha kwa kaya maskini katika kijiji cha Mitwigu wilayani humo.

Aliongeza kuwa fedha hizo japo ni kidogo lakini zinawasaidia sana kimaisha kwani zamani alikuwa anaishi maisha ya taabu sana ikiwemo kuomba omba lakini sasa haombi tena kwa watu.

‘Sasa siombi tena chakula kwa watu, naomba serikali iache mradi huu uendelee, wasiuondoe,' aliongeza.

Mzee Magubika Andrea (80) mkazi wa kijiji cha Mitwigu anaeleza kuwa tangu aanze kupata hela za TASAF III maisha yake yamebadilika sana kwani ana uhakika wa kupata chakula kila siku na tayari amefuga kuku 10 na amepanga kununua bati moja moja ili kuezeka nyumba yake, anataka kuondoa nyasi.
Wananchi wa kijiji Mitwigu wilayani Sikonge Mkoani Tabora wakiwa kwenye foleni ya uwezeshwaji fedha za TASAF juzi.

Mzee Mrisho Athuman (74) wa kijiji cha Kikungu alieleza bayana kuwa alikuwa anaumwa sana na chakula kilikuwa hamna, lakini baada ya kupata hela hizo akanunua dawa na chakula, sasa ameshapona na afya yake imerudi vizuri hana wasiwasi tena ameanza kunawili.

‘Kama sio hizi hela za serikali ningekufa mapema, nilikuwa naumwa sana, ndani chakula hamna, watoto hawaendi shule hata nguo walikuwa hawana, baada ya kupewa hela sasa watoto wanasoma, na mimi nimepona kabisa na nina kuku 6’, aliongeza.

Bi.Anet Joel Sangira (74) mkazi wa kitongoji cha Magharibi kata ya Chabutwa anasema hali yake ilikuwa duni sana lakini baada ya kuwezeshwa 40,000 za awali watoto wake 3 na wajukuu 2 waliokuwa wameacha shule sasa wanaenda wote na mmoja amekuwa wa kwanza darasani kati ya watoto 60.
Wazee wa kijiji cha Chabutwa wilayani Sikonge Mkoani Tabora wakisubiri mgao wa fedha za TASAF(Picha na Allan Ntana).

‘Nyumba yangu ilikuwa ya nyasi sasa nimebadilisha nimeweka bati upande mmoja nitamalizia upande mwingine kidogo kidogo nikipata hela nyingine’, alisema Salome.

Mratibu wa Mradi wa TASAF wilayani Sikonge Claud Nkanwa anaeleza kuwa mradi huu umewasaidia sana wananchi wengi kwani wengi wao walikuwa wanakula mlo mmoja tu kwa siku kutokana na kuishi maisha ya umaskini.

Anaelezea changamoto kubwa anayokumbana nayo kuwa ni baadhi ya wananchi kuomba kuongezewa hela kwa msingi kwamba hela wanayopewa ni kidogo na kwamba wanashindwa kuigawa kwa chakula na kuanzisha miradi.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 1 mpaka sasa

  1. AnonymousJune 16, 2016

    Kuondoa umasikini ni wajibu wa kila mtanzania.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...