Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Tulia Ackson akimuonesha Rais Dkt. John Pombe Magufuli sehemu ya Madawati yaliyotengenezwa na fedha zilizopatikana kutokana na kubana matumizi kutoka Ofisi ya Bunge katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwa amekaa kwenye moja ya Dawati katika hafla hiyo fupi ya ugawaji wa Madawati hayo.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza na Mwanafunzi wa darasa la tano katika shule ya Msingi Bunge George Samwel wakati akiangalia mfano wa darasa ya jinsi madawati hayo yatakavyo katika katika shule mbalimbali nchini.
Sehemu ya Wanafunzi wakiwa wamekalia kwenye madawati yatakayogawiwa leo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli , katika hafla ya ugawaji Madawati hayo, inayofanyika hivi sasa kwenye viwanja vya Karimjee, Jijini Dar es salaam.
 Sehemu ya Madawati hayo yatakayowawiwa leo.


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amezindua mpango wa ugawaji wa madawati yanayotengenezwa kutokana na fedha zilizotolewa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania baada ya kubana matumizi katika bajeti yake.
Uzinduzi huo umefanyika leo tarehe 13 Julai, 2016 katika viwanja vya Karimjee Jijini Dar es salaam ambapo Rais Magufuli amekabidhi madawati 537 kwa mbunge wa jimbo la Ilala Mheshimiwa Mussa Azan Zungu kwa niaba ya wabunge wa majimbo yote ya Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar ambayo yatagawiwa idadi hiyohiyo ya madawati kwa kila jimbo.
Madawati hayo 537 ni sehemu ya madawati 61,385 ambayo yametengenezwa katika awamu ya kwanza na yatafuatiwa na madawati mengine 60,000 yatakayogawiwa katika awamu ya pili na yote kwa ujumla yatagharimu shilingi bilioni 4 ambazo zilitolewa na Bunge tarehe 11 Aprili, 2016 baada ya kubana matumizi katika bajeti yake, ikiwa ni kuitikia wito wa Mhe. Rais John Pombe Magufuli.
Mikoa itakayonufaika katika awamu ya kwanza ya ugawaji wa madawati hayo ni Dar es salaam, Pwani, Morogoro, Lindi, Mtwara, Ruvuma, Iringa, Njombe, Mbeya, Songwe, Rukwa, Katavi, Unguja, Pemba na Tanga.
Akizungumza katika hafla hiyo, Rais Magufuli amewashukuru na kuwapongeza wabunge kwa kutoa mchango huo na pia amewapongeza wadau wengine ambao wameitikia wito wake wa kuchangia madawati kwa lengo la kuondoa tatizo la wanafunzi kukaa chini.
Rais Magufuli amesema baada ya kuanza kutekeleza ahadi ya kuondoa ada kwa shule za msingi na sekondari, idadi ya wanafunzi waliojiandikisha kuanza darasa la kwanza imeongezeka kutoka wanafunzi 1,282,100 hadi kufikia wanafunzi 1,896,584 sawa na ongezeko la asilimia 84.5 hali iliyosababisha upungufu wa madawati 1,400,000 lakini tatizo hilo limetatuliwa kwa kiasi kikubwa ambapo mpaka sasa zaidi ya madawati 1,000,000 yametengenezwa.
Aidha, Dkt. Magufuli amelitaka Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na Jeshi la Magereza kuongeza kasi katika utengenezaji wa madawati ili yakamilike haraka na kuanza kutumika.
Hafla hiyo imehudhuriwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa, Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Tulia Ackson, Wabunge wa kamati ndogo ya tume ya huduma za bunge, Viongozi wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) na Jeshi la Magereza pamoja na wanafunzi wa shule ya msingi Bunge.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es salaam

13 Julai, 2016

Orodha ya Mgawanyo wa Madawati hayo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 4 mpaka sasa

  1. AnonymousJuly 13, 2016

    M/Mungu akujaalieMheshimiwa Rais pamoja na watendaji waongofu katika hili la madawati. Tulikuwa tunaona na wengine tumepitia katika kukaa juu ya vipande vya mawe na kukaa chni kabisa katika Mashule yetu. Tulikuwa tukijiuliza hivi tumemkosea nini Mwenyezi Mungu? Kumbe ilikuwa ni makusudi ya baadhi ya waliopewa dhamana ya kutuongoza. MwenyeziMungu akuongoze katikamkutuletea neema na maendeleo katika nchi yetu adhimu.Mimi binafsi nakutakia maisha mema na marefu na uendelee kufanya kazi zako kwa bidii ukiwa na wafanaykazi wengine mahiri.Asante Serikali, Asante Mungu

    ReplyDelete
  2. AnonymousJuly 13, 2016

    Huu ndo uzuri wa kuwa na raisi mwalimu na msomi kwani anajali elimu. Pia anaamini elimu ni applicable ndo maana hukagua vyetu vya maafisa wake. wale waliokuwa wamezoea msemo wa "kufeli masomo siyo kufeli masiha" watapumzika kwa miaka 10 hivi kwanza. Maanake ilishazoeleka kilaza wako unamkuta kwenye interview pannel ya interviewers pale uombapo kazi. Hiyo ilivunja moyo wa watoto kusoma wakiamini masomo hayana kitu bali zali.

    ReplyDelete
  3. AnonymousJuly 14, 2016

    Hili ni jambo zuri ninawapongea lakini ningependekeza Fikeni vijiji kabisa jamani kulea wazazi hawajiweji hata kuchangia! sasa Bunge si hata mzazi moja tu au wawili wanaweza kuchangia hayo madawati! Nendeni kula ambako hakufikiki~

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...