TAKRIBAN kilometa 10 kutoka Kijiji cha Dakawa kuna kitongoji cha Magogo kilichoko msituni kabisa ambako pia kuna mashamba ya mpunga.


Msitu huu ambao bado ungali na miti mingi ya asili ambayo imenusurika kucharangwa na wachoma mkaa na wanaotafuta ardhi yenye rutuba kwa ajili ya kilimo, ndiko akinamama wapatao 30 wameamua kutundika mizinga kwa ajili ya ufugaji wa nyuki katika shamba lenye ukubwa wa ekari nne.

Licha ya kujikwatua vilivyo, lakini wanapoingia katika msitu huu akinamama hawa hawana mchezo kabisa, baadhi yao wanavaa mavazi maalum ya kujikinga na nyuki na kuanza kukagua mizinga yao kama tayari nyuki wamekwishaingia.
Ofisa Nyuki wa Wilaya ya Mvomero, Oscar Kunambi (aliyechuchumaa kushoto) akisaidiana na mwanakikundi cha Dakawa Green Voices, Neema Obeid, kuweka vizuri mzinga.



“Kujipamba ni jambo la kawaida, lakini tunapokuja huku tuko kikazi zaidi,” anasema Neema Obeid huku akipenya kwenye vichaka kuiendea mizinga ambayo iko juu ya miti mikubwa.

Akina mama hao wa kikundi cha Dakawa Green Voices Women Group wameamua kuingia kwenye ujasiriamali wa ufugaji wa nyuki kwa malengo makubwa mawili – kupata fedha kutokana na mazao ya nyuki pamoja na kupambana na mabadiliko ya tabinchi.

“Misitu inateketea, watu wanaendelea kuchoma mkaa na wengine wanafyeka miti ili wapate mashamba, lakini kwa kuanzisha ufugaji huu wa nyuki, kamwe hatutakubali kuona yeyote akikata hata fimbo, achilia mbali miti mikubwa,” anasema Bi. Mariam Bigambo, mshiriki kiongozi wa mradi huo.
Mwanahabari Judica Losai (wa pili kushoto) akimuuliza maswali Ofisa Nyuki wa Wilaya ya Mvomero, Oscar Kunambi, wakati wakiwa kwenye eneo la ufugaji wa nyuki. 


Mariam Bigambo ni miongoni mwa akinamama 10 waliopatiwa mafunzo nchini Hispania mapema mwaka huu na wanatekeleza kwa vitendo mradi wa Green Voices, ambao unafadhiliwa na taasisi inayojihusisha na maendeleo ya wanawake wa Afrika, ijulikanayo kama Women for Africa Foundation inayoongozwa na Makamu wa Rais mstaafu wa Hispania, María Teresa Fernández de la Vega. Hapa nchini, mradi huo unasimamiwa na asasi ya Environment Media Agenda (EMA) chini ya uratibu wa Bi. Secelela Balisidya.

BOFYA HAPA KUSOMA ZAIDI

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...