Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa ameutaka uongozi wa  Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA) kutoa adhabu kali kwa wamiliki wa vyombo vya usafirishaji na madereva wazembe wanaosababisha ajali za barabarani.

Ameyazungumza  hayo wakati  wa ukaguzi wa utendaji kazi kwa wafanyakazi wa taasisi zilizopo chini ya Wizara hiyo pamoja na miundondombinu ya Barabara, Bandari, Mawasiliano na kiwanja cha ndege cha Kikwetu mkoani Lindi. 

Profesa Mbarawa amesema kuwa ongezeko la ajali zinazosababisha vifo kutokana na uzembe wa madereva, kutofuata sheria na alama zinazowekwa  barabarani zizidhibitiwe ili kuokoa maisha ya watanzania na nguvu kazi ya Taifa. 
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (wa pili kulia) akitoa maelekezo kwa Meneja wa Kiwanja cha ndege cha Kikwetu Mkoani Lindi Bw. Boniface Njanda (Wa kwanza Kulia) wakati alipotembelea uwanja huo.

“Nataka kuona wamiliki wa vyombo vya usafiri na madereva wazembe wanaposabisha ajali na kuua watu wanafutiwa leseni zao vile vile nawataka mfikirie kwanini watanzania wengi wanaendelea kufa kwa ajali za barabarani ili muweze kutafuta ufumbuzi wa namna ya kudhibiti ajali hizo”, amesisitiza Prof. Mbarawa. 

Katika hatua nyingine Waziri Mbarawa amemuagiza Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) Eng. George Sambali kukamilisha kazi ya kupima eneo la kiwanja cha Kikwetu ili kupata hati miliki na kudhibiti uvamizi wa kiwanja hicho.

“Kama kiwanja hiki hakitapimwa watu watavamia eneo la kiwanja na Serikali italazimika kuingia gharama za kulipa fidia hivyo kuchelewesha maendeleo ya uwanja huo”, amesema Prof. Mbarawa.
Mtaalam wa ufundi na Mitambo wa Kampuni ya Simu nchini (TTCL) akifafanua jambo kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa namna ya Mitando ya TTCL inavyofanya kazi, Mkoani Lindi.

Ameongeza kuwa Serikali iko kwenye hatua za mwisho za kutafuta fedha kwa kushirikiana na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) ili kuimarisha miundombinu ya kiwanja hicho na  kuongeza chachu ya maendeleo Mkoani humo.

Naye Meneja wa Uwanja wa Ndege wa Kikwetu, mkoani Lindi Bw. Boniface Njanda amemuhakikishia Waziri Prof. Mbarawa kuwa Mamlaka itafanya tathmini ya Kiwanja hicho kabla ya kuanza ujenzi kwa kiwango cha lami.

Waziri Mbarawa yupo katika ziara ya kukagua utendaji kazi kwa wafanyakazi wa taasisi zilizopo chini ya Wizara na kuangalia maendeleo ya utekelezaji wa miradi katika kanda ya kusini.
Meneja wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) mkoa wa Lindi Eng. Isaac Mwanawima akitoa taarifa ya utendaji wa Wakala huo kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (wa kwanza kushoto) wakati alipotembelea wakala huo.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akitoa maelekezo kwa Meneja wa Wakala wa Majengo (TBA) mkoa wa Lindi Eng. Hillary Msaki, wakati alipotembelea wakala huo,mkoani Lindi.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 1 mpaka sasa

  1. AnonymousJuly 16, 2016

    Waheshimiwa watoa uamuzi na waunda sera naomba tutazame hili;
    Dereva wa chombo cha moto anaendesha kwa umakini na taadhari kama vile alivyofundishwa. Lakini matatizo mengi vilevile huchangiwa na ufinyu wa miundombinu na uzamani wake. Barabara zina mashimo kama mahandaki ambapo wakati wa ukwepaji wa mashimo na mahandaki hayo ndiyo sababu kuu ya ajali. Barabara hazina muangaza wakutosha wakati wa usiku. Barabara na maeneo mengi yana udhaifu wa barabara kutokana na kujengwa chini ya viwango, ni sababu pia za ajali.Vivuko vya majini ni vya zamani na vinajaza watu kupindukia wakati hakuna ajuae ni watu na mali kiasi gani vinasafirishwa kwa wakati mmoja. Itokeapo ajali wa kwanza kutolewa UTU na kutolewa KAFARA anakuwa ni mwendeshaji wa chombo hicho kwa wakati huo. Kwa mtazamo wangu huu si UTU na anayehusika moja kwa moja si dereva au mmiliki wa chombo ila ni mmiliki wa njia!! Na kwa upande wa usafiri wa majini tunaona vivuko karibu vyote ni vya Serikali kwa hiyo ausikaye ni Waziri husika wa nyanja hii. Tumuogope Mungu na tusiwe rahisi kuwakabidhi makosa wasio na nguvu. Kuna kesho jamani baada ya maisha haya hapa duniani. Na Serikali kusema SORRY baada yakupoteza maisha ya watu haisaidii kitu. Hebu turekebishe haya katika usimammizi na pia hii ni dhamana tuliyopewa si na wananchi ila ni Mwenyezi Mungu mwenyewe!!trafic polis hawapo mabarabarani baaada ya saa 12 jioni. Jamaniwahusika watunga sheria na watoa uamuzi hebu tutazameni hili. Sheria kuvunjwa na kutakiwa kwa huduma ni masaa 24 kwa kila nyanja.

    SM-Pate

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...