Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imekemea vikali vitendo vya ukeketaji
vinavyotaarifiwa kufanyika katika Kata ya Kivule, Manispaa ya Ilala jijini Dar es salaam, na mikoa
mengine ambayo imekaririwa na vyombo vya habari.
Wizara inawaagiza wazazi na walezi kuacha mara moja vitendo vya ukeketaji kwani ni ukatili, husababisha
madhara kwa watoto wa kike na wasichana ni kosa la jinai.
Athari za ukeketaji kwa wahanga ni pamoja na kusababisha majeraha kwa watoto, vifo, vilema, maradhi
kama fistula na mengineyo. Watoto wa kike na wanawake wamekuwa wakifanyiwa ukatili wa vitendo vya
ukeketaji bila ridhaa yao na wakati mwingine ridhaa hiyo huwa imepatikana kwa hila, jambo ambalo ni
ukiukwaji wa haki za binadamu.
Wizara inatoa rai kwa vyombo vya dola kuwakamata wazazi, walezi, mangariba, na wote wanaoendeleza
vitendo vya ukeketaji dhidi ya watoto wa kike na wasichana katika kata ya Kivule na maeneo mengine
nchini, na kuwafikisha mahakamani ili sheria iwezekuchukua mkondo wake.
Wizara itaendelea kupambana na vitendo vya ukeketaji vinavyotaarifiwa katika jamii zetu, na itaongeza
juhudi ya utoaji elimu kwa jamii sambamba na kuwachukulia hatua wote wanaojihusisha na mila potofu
ya ukeketaji.
Wito unatolewa kwa kila mwananchi kushiriki katika kuzuia vitendo vya ukeketaji na hasa kufichua
matukio ya ukeketaji, na kutoa ushahidi mahakamani ili wahusika waweze kuchukuliwa hatua stahiki.
Wizara inatoa rai kwa Maafisa Maendeleo ya Jamii na Maafisa Ustawi wa Jamii katika Mikoa,
Halmashauri na Kata katika maeneo ambako kunaarifiwa kuwepo vitendo vya ukeketaji kuhakikisha kuwa
wanashirikiana na mamlaka husika kuzuia ukatili huo katika nchi yetu.
Erasto T. Ching’oro
Msemaji wa Wizara-Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na watoto
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...