Rais wa Marekani, Barack Obama amewahimiza wanachama wa chama cha Democratic kupigania sheria yake ya bima ya afya ambayo utawala wa Rais Mteule, Donald Trump umeahidi kuubatilisha baada ya kuingia madarakani.

Akizungumza katika mkutano wa faragha wa saa mbili, Obama aliwahimiza wabunge wa chama hicho kuitetea sheria hiyo, huku wanachama wa Republican nao wakichukua hatua ya kufuta sheria hiyo.

Makamu wa rais mteule wa nchi hiyo, Mike Pence pia alikuwa katika bunge la Congress, ambapo alisema chama chake kitafuta sheria hiyo ambayo hufahamika sana kama Obamacare. Sheria hiyo iliwezesha takriban Wamarekani milioni 20 na zaidi kupokea huduma ya afya.

Hata hivyo, sheria hiyo imekabiliwa na changamoto za kupanda kwa malipo ya wanaopokea huduma ya bima na pia kampuni nyingi za bima zimejitoa kutokana na mpango huo. Hilo limewaacha Wamarekani wakiwa hawana njia nyingine mbadala za kujipatia bima ya afya.
Baada ya Rais Obama kufanya ziara hiyo ya nadra sana makao makuu ya bunge la Marekani Capitol Hill siku ya Jumatano, mbunge wa chama cha Democratic, Elijah Cummings aliwaambia wanahabari kwamba Obama aliwahimiza kupigana kulinda sera hiyo kuu iliyotimizwa na utawala wake.
Baadhi ya waliokuwepo waliwaambia wanahabari Marekani kwamba rais huyo anayeondoka pia aliwahimiza "kuwa na nguvu" huku Republican wakijiandaa kuchukua udhibiti wa ikulu ya White House na mabunge yote mawili ya Congress - Bunge la Wawakilishi na Bunge la Seneti - kwa mara ya kwanza katika mwongo mmoja.
Alisema hayo huku bunge la Seneti likichukua hatua ya kwanza ya kufuta sheria hiyo ya Obamacare.
Walipiga kura 51 dhidi ya 48 kujadili azimio la bajeti ambalo lengo lake ni kunyima ufadhili kwa mpango huo wa Obama.
Chanzo: BBCSwahili

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...