Serikali kupitia Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka Dar es Salaam (DAWASA) inatekeleza mradi wenye thamani ya bilioni 18 unaolenga kuondoa changamoto ya upatikanaji wa maji katika Jiji la Dar es salaam.
Kauli hiyo imetolewa leo na Mkurugenzi wa ufundi na uendeshaji wa Mamlaka hiyo Bw. Romanus Mwangingo wakati wa ziara ya waandishi wa habari katika eneo la Kimbiji ambako ndipo mradi huo unapotekelezwa .
“Mkandarasi anaendelea na kazi na ameleta mabomba yote na amechimba visima 15 na vitazalisha maji yatakayotumika katika Jiji la Dar es salaam na mradi unatarajiwa kukamilika machi 2017” Alisisistiza Mwangingo. Aliongeza kuwa utekelezaji wa mradi huo umefikia asilimia 85 na utakapokamilika maeneo ya Kigamboni,Temeke,Ilala na Jiji la Dar es salaam kwa ujumla yatanufaika kwa kupata huduma ya maji.
Maji yakitoka kwenye moja ya Kisima Kirefu kilichochimbwa katika eneo la Kimbiji unakotekelezwa mradi mkubwa wa unaolenga kutatua changamoto ya maji katika Jiji la Dar es salaam.
Kwa upande wa miradi mingine kama ule wa ujenzi wa Bomba kutoka Ruvu juu hadi kimara Mwangingo amesema ulikamilika mwezi oktoba 2016 na uzalishaji wa majaribio unaendelea.
Mradi huo wenye thamani ya dola za marekani milioni 59 ni moja ya mikakati ya Serikali katika kuhakikisha kuwa wakazi wa Jiji la Dar es salaam wanapata huduma ya maji safi na salama. na kuondokana na changamoto hiyo. . Aidha mradi huo utawezesha kiwango cha maji kufikia lita milioni 196 kwa siku kutoka lita milioni 82 za awali.
Kwa upande wake Bw.Salum Hamis mkazi wa mbagala amepongeza miradi ya maji inayotekelezwa na Serikali kwa kushirikiana na wananchi kwa kuwa imekuwa chachu ya maendeleo katika maeneo yao. Aliongeza kuwa miradi hiyo imechochea kupunguza tatizo la maji na imewawezesha wananchi kutumia muda mwingi katika shughuli za kiuchumi na hivyo kuchochea ukuaji wa uchumi.
Meneja Uhusiano wa DAWASA Bi Neli Msuya akieleza kwa waandishi wa habari faida za miradi inayoibuliwa na Mamlaka hiyo kwa kushirikiana na wananchi katika kutatua changamoto ya upatikanaji wa maji katika Jiji la Dar es salaam.
Katika kukabilina na tatizo la miundombinu ya maji taka katika Jiji la Dar es salaam mamlaka hiyo iko katika mchakato wa kuanza ujenzi wa mtambo mkubwa wa kuchuja maji taka katika eneo la Jangwani na kuboresha mfumo wa maji taka katikati ya Jiji.
Mradi mwingine ni ule wa upanuzi wa ruvu chini ambao umekamilika kwa asilimia mia moja na utawezesha upatikanaji wa maji kufikia lita milioni 270 kwa siku kutoka milioni 180 kabla ya mradi huo haujatekelezwa.
Majukumu ya DAWASA ni kumiliki miundombinu ya maji safi na maji taka kwa niaba ya Serikali, kusimamia utoaji wa huduma ya maji safi na maji taka Dar es salaam, kugharimia,kupanga mipango na kusimamia upanuzi wa huduma na kuishauri Serikali kuhusu masuala ya huduma ya maji safi na maji taka Jijini Dar es salaam.
Mtambo unaotumika kuchoronga Visima Virefu ukiwa katika eneo la Kimbiji unapotekelezwa mradi mkubwa wa uchimbaji visima virefu.
BOFYA HAPA KWA PICHA ZAIDI.
BOFYA HAPA KWA PICHA ZAIDI.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...