Na Theresia Mwami TEMESA
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Dkt. Mussa Mgwatu
ametembelea na kukagua mradi wa ujenzi wa boti nne za kisasa unaofanywa na
kampuni ya Songoro Marine Boatyard jijini Mwanza. Akiwa katika karakana ya kampuni
ya Songoro, Dkt. Mgwatu amesema kuwa Serikali imepanga kutekeleza mradi huo ili
kutoa huduma za usafiri wa majini kwa wananchi katika maeneo manne tofauti.
Aliyataja maeneo hayo kuwa ni Pangani mkoani Tanga ambako wananchi walimuomba
Waziri wa Ujenzi Uchukuzi na Mawasiliano Mhe. Prof. Makame Mbarawa alipokuwa
akizindua Kivuko cha MV. Tanga kuwaletea boti ndogo itakayokuwa inatumika
kuwasaidia wananchi wanapokuwa na dharura nyakati za usiku wakati ambapo kivuko
cha MV. Tanga kinakuwa kimeegeshwa. Boti ya pili itapelekwa sehemu ya Msangamkuu
mkoani Mtwara na vile vile itatumika kwa nyakati za dharura. Boti hizi mbili zitakuwa
na uwezo wa kubeba abiria 8 kila moja.
Boti ya tatu itapelekwa eneo la Kilambo, Mtwara ambako kivuko cha MV. Kilambo
kinatoa huduma ya kuvusha wananchi kati ya upande wa Tanzania na Msumbiji kupitia
mto Ruvuma. Boti hii itatumika katika vipindi ambavyo maji ya mto ni machache
kuweza kuendesha kivuko cha MV. Kilambo na itakuwa na uwezo wa kubeba abiria 25.
Boti ya nne ambayo inajengwa kwa kutumia chuma itakuwa na uwezo wa kubeba
abiria 40 na itapelekwa kwenye eneo la Utete mkoani Pwani ili kiweze kutoa huduma
wakati wote hata pale maji ya mto yanapokuwa machache. Nae Mkandarasi kutoka
kampuni ya Songoro Marine Boatyard, Bw. Major Songoro amesema kuwa kazi ya
kujenga boti zote nne inatarajia kukamilika mwishoni mwa mwezi huu.
Dkt. Mgwatu alikuwa katika ziara ya kikazi mkoani Mwanza kukagua na kujionea
maendeleo ya ujenzi wa boti hizo nne.
Mtaalamu kutoka kampuni ya Songoro Marine Boatyard Ndugu Mohamed Salim
(alie ndani ya boti) akimuelekeza jambo Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi
na Umeme (TEMESA) Dkt. Mussa Mgwatu (wa kwanza kulia), pembeni yake ni
Major Songoro pamoja na Meneja wa TEMESA mkoani Mwanza Mhandisi
Ferdinand Mishamo. Boti hiyo ni moja kati ya mbili zinazotarajiwa kupelekwa
maeneo ya Pangani mkoani Tanga pamoja na Msangamkuu mkoani Mtwara kwa
ajili ya kutumika nyakati za dharura.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Dkt. Mussa Mgwatu
(alieshika nguzo ya boti) akiangalia moja ya boti kati ya mbili yenye uwezo wa
kubeba abiria nane zinazotarajiwa kupelekwa maeneo ya Pangani mkoani Tanga
pamoja na Msangamkuu mkoani Mtwara kwa ajili ya kutumika nyakati za
dharura.
Sehemu ya chini ya boti inayojengwa kwa ajili ya kutoa huduma mto rufiji
katika eneo la Utete/Mkongo, boti hiyo itakuwa na uwezo wa kubeba abiria 40.
Ujenzi wa boti hiyo unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi huu.
Picha zote na Theresia Mwami TEMESA
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...