Na Grace Michael, Kigoma

MWENYEKITI wa Bodi ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) Mama Anne Makinda amesema, Mfuko hautamvumilia mtu yoyote mwenye lengo la kuhujumu huduma zake kwa manufaa yake binafsi na badala yake Mfuko huo utanufaisha wanachama na Watanzania kwa ujumla.

Amesema kuwa ni wakati muafaka kwa wananchi wote kuulinda Mfuko na kujiunga na huduma zake kwa kuwa ni mfumo unaorahisisha upatikanaji wa huduma za matibabu na ndio mfumo unaotumika kote duniani.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa NHIF kwa pamoja na Mwenyekiti wa Bodi, Mama Anne Makinda wakimsaidia Mama mlemavu aliyefika hospitalini hapo kwa lengo la kuhudumiwa na Madaktari Bingwa.

Mama Makinda ameyasema hayo mkoani Kigoma wakati akizindua mpango wa huduma za Madaktari Bingwa unaotekelezwa kwa wiki nzima mkoani hapa na mkoani Geita kwa ushirikiano wa Mfuko na Wizara ya Afya, Ustawi wa Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.

“Hakuna mtu binafsi atakayetumia Mfuko huu kwa maslahi yake binafsi na sisi Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya hatutakubali kuona mtoa huduma yoyote akiharibu sifa nzuri ama utendaji ambao umeimarishwa kwa kipindi kirefu kwa ajili ya wanachama na wananchi kwa ujumla…tutasimamia huduma zetu kwa nguvu zote,” alisema Mama Makinda.
Mwenyekiti wa Bodi ya NHIF, Mama Anne Makinda akizungumza na wananchi wa Mkoa wa Kigoma ambao baadhi yao ni wagonjwa waliofika katika uzinduzi wa huduma za Madaktari Bingwa mjini Kigoma. 

Alionya tabia za baadhi ya watumishi wa sekta ya afya ambao wamekuwa wakitumia nafasi zao kunyanyasa wagonjwa na kusema kuwa huduma za afya ni huduma za msingi ambazo hazitakiwi kuchezewa na mtu yoyote ama kutolewa kwa utashi wa mtu binafsi.

Akizungumzia utaratibu unaoendeshwa na NHIF wa kupeleka madaktari Bingwa alisema kuwa, Mfuko uliamua kuchukua uamuzi wa kutoa huduma hizi za kibingwa katika Mikoa ambayo ina upungufu wa huduma hizo ili kuhakikisha kila Mtanzania anajivunia uwepo wa Mfuko huo.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Benrard Konga akitoa maelezo ya awali ya zoezi la huduma za Madaktari Bingwa wakati wa uzinduzi wa huduma hizo.

“Pamoja na huduma hizi Mfuko unazo fursa nyingi hususan za uboreshaji wa huduma za afya kupitia mikopo ya vifaa tiba na ukarabati wa majengo hivyo tumieni hii fursa kujitathmini ili vituo mshirikiane na Mfuko katika uboreshaji wa sekta hii,” alisema Mama Makinda.

Kwa upande wa Mkuu wa Wilaya ya Kigoma ambaye alimwakilisha Mkuu wa Mkoa, Samson Anga aliushukuru Mfuko kwa kutoa kipaumbele cha kupeleka madaktari bingwa kwa Mkoa wa Kigoma  ambao una mahitaji makubwa ya wataalam hao.

“Kwa kweli niushukuru sana Mfuko huu kwa jitihada mnazofanya na kama ambavyo mnaona hali ilivyo wananchi wamefurika hapa kwa ajili ya kupata huduma hivyo zoezi hili litaleta manufaa makubwa ya afya za wananchi wa Kigoma,” alisema Bw. Anga.
 Mkuu wa Wilaya ya Kigoma Bw. Samson Anga akiongozana na Mwenyekiti wa Bodi ya NHIF Mama Anne Makinda wakati wakiingia katika Hospitali ya Mkoa wa Kigoma Maweni.  

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...