Wizara ya Nishati na Madini imetoa mafunzo ya Mfumo wa pamoja wa Kukusanya Maduhuli ya Serikali (GePG) kwa Maafisa Madini na Wahasibu wa Wizara hiyo ili kuboresha shughuli za ukusanyaji maduhuli.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Mhasibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Anthony Tarimo alisema kuwa mafunzo yamelenga kuwawezesha washiriki kuuelewa vyema mfumo huo ili kuwa na ukusanyaji wa maduhuli ya Serikali wenye tija.

Alisema Serikali imeamua kuboresha mfumo wa ukusanyaji wa maduhuli kuwa wa kielektroniki ili kurahisisha ukusanyaji wa maduhuli na vilevile kuongeza uwazi miongoni mwa Wizara na Taasisi mbalimbali za Serikali.

“Kupitia mfumo huu, Serikali inao uwezo wa kujua maduhuli yote yanayoingia kwa wakati mmoja kwa sababu umeunganishwa na Wizara na Taasisi mbalimbali,” alisema Tarimo.

Alibainisha kuwa Mfumo huo wa GePG ulianza kutumika rasmi Julai, 2017 na kwamba kwa upande wa Wizara ya Nishati na Madini mafunzo ya awali yalitolewa kwa watumishi wa Ofisi ya Madini- Kanda ya Mashariki ambayo inahusisha ofisi za madini za Dar es Salaam, Pwani, Tanga, Handeni na Morogoro.
Alisema Mfumo huo ni rafiki na kwamba utaboresha na kurahisisha ukusanyaji wa maduhuli na kwamba mara baada ya mafunzo, washiriki watakuwa na uwezo wa kuutumia ipasavyo. Tarimo alisema mafunzo hayo yanawahusu Wahasibu, Maafisa Leseni pamoja na watumishi wengine ambao kwa njia moja ama nyingine wanahusika na utoaji wa hati za madai za malipo mbalimbali.

Aliongeza kuwa, mafunzo hayo yanahusisha uwasilishaji wa mada mbalimbali kutoka kwa wataalam wa TEHAMA wa Wizara ya Fedha na Mipango na wa Wizara ya Nishati na Madini na pia yatahusisha majadiliano ili kuboresha utendaji kazi wa watumishi wanaohusika na ukusanyaji wa maduhuli.

“Wanasheria pia watawasilisha mada ili kuelewa vyema mabadiliko katika Sheria ya Madini ya mwaka 2010 yaliyofanyika hivi karibuni,” alisema  Tarimo. Mafunzo hayo ya siku nne yanafanyikia katika Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine Morogoro (SUA) na yameanza Agosti 28, 2017 kwa kushirikisha zaidi ya washiriki 100.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...