Na Greyson Mwase, Simiyu
Wachimbaji wa madini ya dhahabu katika wilaya ya Maswa mkoani Simiyu
wameiomba Serikali kupitia Wizara ya Madini kufanya utafiti wa madini katika
maeneo yao ili waweze kuwa na uhakika wa uchimbaji wa madini na uzalishaji wao
kuwa na tija.
Wameyasema hayo leo tarehe 29 Oktoba, 2017 katika ziara ya Naibu Waziri wa
Madini, Stanslaus Nyongo katika wilaya ya Maswa mkoani Simiyu yenye lengo la
kukusanya kero za wananchi mbalimbali hususan katika shughuli za uchimbaji
madini.
Akizungumza kwa niaba yao, Sylivester Fundikira alisema kuwa wameunda jumla ya
vikundi 30 ambapo kila kikundi kina mashimo yake na kueleza kuwa wamekuwa
wakipata changamoto ya upatikanaji wa madini ya uhakika kutokana na maeneo
yao kutofanyiwa utafiti kwa muda mrefu.
Akijibu kero hiyo Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo alisema kuwa Wizara
ya Madini kupitia Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST) imekuwa ikifanya tafiti sehemu
mbalimbali nchini na kusisitiza kuwa Serikali kupitia Wizara ya Madini ipo tayari
kuwasaidia.
Alisema Serikali inatambua mchango mkubwa wa wachimbaji wadogo wa madini na
kuongeza kuwa imeweka mikakati ya kuwawezesha wachimbaji wadogo wa madini
kwa kuwapatia vifaa kupitia ruzuku ili uchimbaji wao uwe na mchango mkubwa
katika ukuaji wa uchumi wa nchi.
“ Tuna mpango wa kuhakikisha kuwa rasilimali za madini zinakuwa na mchango
mkubwa sana katika ukuaji wa uchumi wa nchi, hivyo tutahakikisha tunasimamia
ipasavyo kwa kuhakikisha kuwa mazingira ya uchimbaji madini yanakuwa rafiki,”
alieleza Naibu Waziri Nyongo.
Katika hatua nyingine, Nyongo alisema kuwa kazi yake pamoja na Waziri wa
Madini, Angellah Kairuki ni kuhakikisha kuwa sekta ya madini inakua kwa kasi na
kuwa na mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi wa nchi.
Alisema kuwa sekta ya madini imekuwa na changamoto kubwa hususan katika
upotevu wa mapato kutokana na wawekezaji wasio waaminifu na kukwamisha
juhudi za serikali katika ukusanyaji wa mapato.
Aliendelea kusema kuwa tangu Rais John Magufuli ameanza kupambana na wezi
wa rasilimali za madini kumekuwa na mabadiliko makubwa kwa kuwa uzalishaji na
mapato umebadilika kutokana na Serikali kuhakikisha kiwango sahihi kinapatikana
na kulipiwa kodi serikalini.
Alisema Serikali imeweka Sheria Mpya ya Madini ya mwaka 2017 na kuwataka
wachimbaji madini nchini kufuata sheria hiyo pamoja na kanuni zake.
Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo, akijibu kero mbalimbali za wakazi wa
kitongoji cha Mwanguhi kilichopo wilayani Maswa mkoani Simiyu (hawapo pichani)
katika mkutano wa hadhara.
Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Seif Shekalaghe akifafanua jambo mbele ya wakazi wa
kitongoji cha Mwanguhi kilichopo wilayani Maswa mkoani Simiyu (hawapo pichani)
katika mkutano wa hadhara.
Mmoja wa wachimbaji wadogo wa madini, Sylivester Fundikira akiwasilisha kero
yake mbele ya Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo (hayupo pichani).
Sehemu ya wakazi wa kitongoji cha Mwanguhi kilichopo wilayani Maswa mkoani
Simiyu wakifuatilia maelezo yaliyokuwa yanatolewa na Naibu Waziri wa Madini
Stanslaus Nyongo (hayupo pichani) katika mkutano wa hadhara.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...